Rais Hifikepunye Pohamba wa Namibia aliyemaliza muda wake ndiye mshindi wa tuzo ya
Mo Ibrahim kutokana na uongozi makini kwa wananchi wake. Tuzo hii inaambatana na kitita
cha Dolla za Kimarekani Millioni 5. Zawadi hii inatolewa kwa viongozi wa Bara la Afrika
ambao wameonesha uongozi bora pamoja na kuboresha hali ya maisha ya wananchi wao wakati
walipokuwa madarakani na muda wao ulipowadia wakaachia ngazi na kuendelea na maisha
kama kawaida pasi ya kung'angania kwenye madaraka kwa kutaka kupindisha Katiba ya
nchi!
Rais Pohamba alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuongoza Namibia kunako
mwaka 2004, akapewa tena dhamana hii kunako mwaka 2009 na hivi karibuni, aling'atuka
kutoka madarakani na kwa sasa Rais mteule Hage Geingob anatarajiwa kusimikwa rasmi
ili kuendeleza mchakato wa uongozi kwa watu wake. Rais Pohamba mwenye umri wa miaka
80 aliteuliwa na Jopo la viongozi wa Afrika kunako mwaka 2014 katika sherehe zilizofanyika
Jijini Nairobi.
Tuzo hii ilianzishwa na Bwana Mo Ibrahim kutoka Sudan ili kuwahamasisha
viongozi wa Bara la Afrika kuwaongoza watu wao kwa hekima na busara na hatimaye, kung'atuka
kutoka madarakani kwa amani na utulivu, huku wakijivunia mafanikio yaliyopatikana
chini ya uongozi wao bila ya kung'ang'ania madarakani kana kwamba, hakuna mtu mwingine
yeyote nchini mwao anayeweza kusukuma mbele Jahazi la maendeleo ya watu. Itakumbukwa
kwamba, kunako mwaka 2007, tuzo hii ilinyakuliwa na Rais mstaafu Joaquim Chisano wa
Msumbiji.
Dr. Salim Ahmed Salim kutoka Tanzania aliyewahi kuwa Katibu mkuu
wa Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika, OAU ndiye Mwenyekiti wa Jopo la majaji wa tuzo
ya Mo Ibrahim.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya
Radio Vatican