Hivi karibuni, Askofu mkuu mstaafu James Odongo wa Jimbo kuu la Tororo, Uganda aliadhimisha
Jubilee ya miaka 50 tangu alipowekwa wakfu kuwa Askofu, sherehe ambazo zimehudhuriwa
na umati mkubwa wa Familia ya Mungu nchini Uganda. Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu
mstaafu Odongo ni Askofu wa nne mzalendo kutoka Uganda kupewa dhamana ya kuliongoza
Kanisa kama Askofu.
Askofu mkuu mstaafu Odongo ni matunda ya maadhimisho ya
Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, kumbe katika maisha na utume wake, alipenda kuhakikisha
kwamba, waamini walei wanapewa nafasi kubwa zaidi katika maisha na utume wa Kanisa.
Ni kati ya Mababa wa Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo, shule ya Neno la Mungu, maisha
ya Kisakramenti na matendo ya huruma. Ni Kiongozi wa Kanisa ambaye ameyakita maisha
yake katika: Fumbo la Ekaristi, Neno la Mungu na Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu
na Kanisa.
Katika maisha yake, amejitahidi kuwa kweli ni Baba mwenye huruma
na mapendo, aliyetaka kuhakikisha kwamba, waamini wa Jimbo Kuu la Tororo wanajenga
na kudumisha mshikamano wa udugu na upendo ili kuondokana na ukabila usiokuwa na mvuto
wala mashiko kwa ustawi na maendeleo ya watu.
Askofu mkuu mstaafu anasema,
enzi ya ujana wake alikuwa ni moto wa kuotea mbali si tu katika ujenzi wa Jumuiya
Ndogo ndogo za Kikristo miongoni mwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana,
bali pia alikuwa anatandaza kabumbu ile mbaya! Makali yake anasema, hata Kardinali
Francis Arinze anayatambua. Ni kiongozi ambaye alitoa kipaumbele cha kwanza kwa maendeleo
na ustawi wa Familia ya Mungu AMECEA na leo hii, Kanisa linafurahia matunda ya mchango
wake!