Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 4 Machi 2015 anatarajiwa
kukutana na kuzungumza na Maaskofu kutoka katika nchi 35 wanaohudhuria Kongamano la
38 unaohusu tasahufi ya maisha ya kiroho ya Chama cha Wafokolari linaloongozwa na
kauli mbiu "Ekaristi Takatifu ni Fumbo la Umoja". Kongamano hili linaratibiwa na Kardinali
Francis Xavier Kriengsak Kovithavanij, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Bangkok, Thailand.
Taarifa
inaonesha kwamba, hili ni kundi la Maaskofu kutoka sehemu mbali mbaloi za dunia ambazo
kwa miaka ya hivi karibuni zimetikiswa na kuguswa na madhulumu, nyanyaso na maonevu
ya kidini. Ni nchi ambazo, vita bado inaendelea kuonesha makucha yake na kwamba, kuna
umati mkubwa wa watu ambao wanaendelea kuteseka kutokana na athari za myumbo wa uchumi
kimataifa. Lakini, pia ni Maaskofu ambao wanatoka katika nchi zenye matumaini na imani
thabiti. Maaskofu katika Kongamano hili ambalo limeanza Jumanne tarehe 3 Machi linatarajiwa
kufungwa rasmi hapo tarehe 6 Machi 2015.
Maaskofu wanashirikishana mang'amuzi,
matumaini na mikakati mbali mbali ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya ustawi na
maendeleo ya Familia ya Mungu katika maeneo yao. Lengo ni kuendeleza mchakato wa majadiliano
ya kidini na kiekumene kama sehemu ya utekelezaji wa dhamana ya Uinjilishaji mpya,
inayovaliwa njuga na Mama Kanisa kwa wakati huu.
Na Padre Richard A. Mjigwa,
C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.