2015-03-02 08:44:40

Wanawake wa shoka!


Je, mmeyatambua hayo niliyowatendea mimi niliye Bwana na Mwalimu? Ni maneo ya Yesu Kristo wakati wa Karamu ya Mwisho alipowaosha miguu wanafunzi wake, akiwataka kujikita katika huduma ya upendo. Hii ndiyo kauli mbiu inayoongoza Siku ya Sala ya Kiekumene itakayoadhimishwa na Wanawake Wakristo nchini Ufaransa hapo tarehe 6 Machi 2015 kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, itakayoadhimishwa hapo tarehe 8 Machi 2015.
Siku ya kimataifa ya sala kwa ajili ya wanawake ilianzishwa kunako rasmi nchini Ufaransa kunako mwaka 1902, lakini Chama hiki cha kiekumene ambacho asili yake ni huko Marekani, kilianzishwa kunako mwaka 1887. Kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, wanawake wa Kikristo nchini Ufaransa wataadhimisha Ibada ya Kiuekumene kwa kusali pamoja na kutafakari jinsi ambavyo wanaweza kumwilisha katika matendo changamoto ya Kristo kwa wanafunzi wake, yaani huduma ya mapendo kati ya watu.
Wanawake Wakatoliki nchini Ufaransa kwa mwaka huu wanapenda kuwasaidia wanawake wanaoteseka, kudhulimiwa na kunyanyasika nchini Bahamas, katika sekta ya afya. Wanawake wanataka kuwasaidia pia watoto ili waweze kupata huduma bora za kiafya, ili kuwajengea matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi na kama sehemu ya utekelezaji wa utandawazi wa udugu na upendo.
Wanawake Wakatoliki Ufaransa katika kampeni yao ya mwaka 2015 wanataka kujenga kituo cha kufanya uchunguzi wa Saratani ya matiti, ili kusaidia kutoa taarifa pamoja na kuwapatia tiba muafaka. Kituo hiki pia kitakuwa na dhamana ya kulinda na kutetea haki msingi za wanawake nchini Bahamas sanjari na kuwajengea uwezo wa kiuchumi, ili kuwasaidia wanawake kuchangia ustawi na maendeleo ya familia zao: kiroho na kimwili.
Si haba kwamba, wasichana wengi watafundishwa pia matumizi ya computer ili kuwapatia ujuzi na maarifa katika mawasiliano ya kijamii, ili baadaye, wanawake wa Bahamas waweze pia kuendeleza mchakato huu nchini mwao kwa kuwafunda wasichana na watoto kuhusu huduma ya upendo kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.