Kwa mara ya kwanza Kanisa Katoliki nchini Angola litaadhimisha Siku ya Vijana Kitaifa
itakayoanza kutimua vumbi hapo tarege 26 hadi tarehe 30 Agosti 2015, kwa kuwahusisha
vijana zaidi elfu tatu kutoka katika Jimbo la Huambo. “vijana ni mashuhuda wa upendo
wa Kristo” ndiyo kauli mbiu inayoongoza maadhimisho ya siku ya kwanza ya vijana kitaifa
nchini Angola.
Padre Armando Alberto Pinho, Katibu wa Idara ya utume wa vijana,
Baraza la Maaskofu Katoliki Angola, Sao Tome na Principe anasema kwamba, tukio hili
litakuwa ni fursa kwa vijana wa Angola kuonja cheche za maadhimisho ya Siku ya Vijana
Kimataifa katika ngazi ya kitaifa. Lengo ni kuamsha, kuchochea na kukoleza upendo
wa vijana kwa Kristo na Kanisa lake, ili kuwasaidia vijana kuonesha na kuchangia nguvu
zao katika ustawi na maendeleo ya jamii kwa kuleta mageuzi ya kina katika maisha na
vipaumbele vyao.
Maaskofu wa Angola wanapania pia kuwahamasisha vijana ili
kujisadaka na kujitoa kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake kwa njia ya maisha ya Kipadre
na Kitawa, hasa wakati huu Mama Kanisa anapoendelea kuadhimisha Mwaka wa Watawa Duniani,
uliotangazwa na Baba Mtakatifu Francisko. Katika maadhimisho ya siku ya vijana kitaifa
nchini Angola, vijana watajengewa uwezo wa kujikita katika majadiliano katika medani
mbali mbali za maisha na utume wa Kanisa. Ni fursa kwa vijana wa kizazi kipya nchini
Angola kukutana na Mwenyezi Mungu katika maisha yao ya ujana kwa njia ya imani.
Na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.