2015-03-02 15:34:43

Papa - hekima ya Mkristo si kuhukumu wengne


Ni rahisi kuhukumu wengine, lakini hekima ya Kikristo inamtaka Mkristo, kwanza ayatazame makosa yake mwenyewe kabla ya kuhukumu wengine. Baba Mtakatifu alieleza mapema Jumatatu hii, wakati wa Ibada ya Misa ya asubuhi katika Kanisa dogo la Mtakatifu Marta mjini Vatican.

Papa alirejea masomo ya siku ambayo yaliangalisha katika mada ya huruma. Papa, alisema, sisi sote ni wenye dhambi, si kinadharia lakini ndiyo hali halisi. Na tunaonyeshwa fadhila za Kikristo, katika nguvu za kweli zaidi kwenye uwezo wa kujikosoa mwenyewe. Papa ameitaja hii ni hatua ya kwanza kwa wote wanaotaka kuwa wafuasi wa Kristo.

Papa amekiri kwamba, sisi sote ni walimu, sisi sote ni madaktari wa kujua kasoro zetu na kujihukumu wenyewe. Na akatahadharisha juu ya kosa la kufumbia macho mapungufu yetu wenyewe na kutazama zaidi mapungufu ya wengine, tabia za kusukumia daima makosa kwa wengine na sisi kujikosha kama hatuna hatia. Tabia za majigambo kwamba mimi sijakosea kitu aliyekosa ni yule, mimi ni safi, huyu ndiye mwenye makosa, n.k Lakini kumbe sisi wote tuna mapungufu kidhamira, tuna dhambi zetu, na pengine kwa mara nyingi tunafanya makosa, na bado tunasema mimi sijakosa. Tumejijenga katika tabia za kuwafanya wengine wawe na hatia, na si mimi.

Papa ameuita unafiki huo wa kujiona si mdhambi kuwa hayo si maisha ya Mkristo, na kuongeza, kwa hakika ni rahisi sana kulaumu wengine. Ha hata wakati mwingine huonekana kama jambo la kushitusha, kwa wale wanao jaribu kuishi katika njia tofauti na hiyo ya kusukumia makosa kwa wengine. Papa anasema, tunao uwezo wa kukiri makosa yetu, ingawa mwanzoni tunaweza jisikia vibaya , kusikia upinzani fulani katika kujishusha na kukiri kosa , lakini baadaye kufanya hivyo humfanya mtu ajisikie kuwa na amani zaidi. Papa alieleza kwa kutoa mfano wa wivu na chuki zinazoweza kujaa moyoni, ambavyo huwa na uwezo wa kudhuru wengine , na hata kuua kimaadili. Papa alihimiza wakristo kutambua hilo na kwamba utambuzi wa kujihukumu mwenyewe kabla ya kuhukumu wengine , hiyo ndiyo hekima ya Mkristo. Na kama Mkristo hawezi kujifunza hatua hii ya kwanza ya maisha, kamwe hawezi kupiga hatua mbele katika njia ya maisha ya Kikristo, maisha ya kiroho.

Kujihukumu au kujikosoa mwenyewe ni hatua ya kwanza, katika kutembea na Kristo. Bila kusema hapana kuhukumu wengine, kuisikiliza dhamiri ya kweli ya moyo, na kukiri kosa ni vigumu kuitembea njia ya Kristo Papa alisisitiza. Ni vingumu kusonga mbele katika njia hiyo , na kusimama mbele ya malango ya gereza la kiroho na kusema ninastahili kufungwa. Papa alieleza na kusema, pengine hatuna hata utambuzi kwamba kama si neema ya Mungu , pia tungekuwa kifungoni . Na pengine kwa makosa yaliyo makubwa zaidi ya wale walio kifungoni. Katika kujihukumu mwenyewe, na kufichua mzizi wa dhambi tunaoupalilia ndani mwetu, mengi tunayoweza kuyafanya , hata kama hayaonekani.

Papa aliendelea kutia shime katika kuyaishi maisha matakatifu akitaja pia ukweli mwingine, wa kuona aibu mbele ya Mungu, kutaja dhambi zetu katika mazungumzo kuona aibu mbele ya ukuu wa neema ya Mungu. Lakini hatupaswi kuona aibu bali kusema, kwako Bwana , Mungu wangu mwenye huruma na Msamaha, naja kwako nihurumie mimi mdhambi. Papa ameitaja aibu yako na aibu yangu, kwamba vinahitaji huruma ya Mungu, yenye msamaha.

Papa alieleza na kuomba ili kwamba, ibada na kumcha Bwana, hasa katika kipindi hiki cha Kwaresima, kutuwezeshe kuyaona makosa yetu zaidi na kujihukumu wenyewe. Na tuombe zaidi huruma hii ya Mungu kama somo la Injili lilivyoweka wazi: 'Muwe na huruma kama Baba yenu alivyo na huruma. Na tufuate mafundisho yake Yesu: Msiwahukumu wengine, msije hukumiwa; msiwalaumu wengine, na kuwatia hatiani ; lakini msamehe , kama pia mnavyo samehewa.
Papa alikamilisha homilia kwa kumwomba Bwana, wakati huu wa Kwaresima , atujalie neema ya kujifunza namna ya kujikosoa, namna ya kujihukumu wenyewe, kutambua kwamba, mimi ni mwovu kuliko wote, unirehemu, Bwana, unisaidie kuwamtu mnyenyekevu na mtiifu, nipe moyo wa huruma, ili niweze kuwa na huruma kwa wengine.








All the contents on this site are copyrighted ©.