Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania, limehitimisha mkutano wake maalum uliojadili
kwa kina mapana kuhusu Sinodi ya Maaskofu kuhusu Familia itakayoadhimishwa mjini Vatican
kuanzia tarehe 4 hadi tarehe 25 Oktoba 2015. Maaskofu wamepokea taarifa ya Tume ya
Familia Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania kuhusiana na majibu ya maswali dodoso
yaliyotumwa kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, tayari kuyatuma kwenye Sekretarieti
kuu ya Sinodi mjini Vatican. Mwisho wa kutuma majibu ya maswali dodoso yatakayotumika
kuandaa hati ya kutendea kazi ni hapo tarehe 15 Aprili 2015. Itakumbukwa kwamba, Sinodi
ya Maaskofu inaongozwa na kauli mbiu “Wito na utume wa Familia ndani ya Kanisa na
katika ulimwengu mamboleo”. Maswali dodoso ni mchango uliotolewa na Mababa wa Sinodi
maalum ya Maaskofu iliyofanyika mwezi Oktoba, 2014 hapa mjini Vatican. Baraza la
Maaskofu Katoliki Hispania linasema kwamba, Familia ya Mungu nchini humo inaendelea
kuadhimisha Jubilee ya miaka 500 tangu alipozaliwa Mtakatifu Theresa wa Avila, kumbukumbu
ambayo itafikia kilele chake hapo tarehe 25 Machi 2015. Maaskofu Katoliki Hispania
wataanza mkutano wao wa mwaka tarehe 20 Aprili na tarehe 24 Aprili 2015 watafanya
hija ya maisha ya kiroho kwa kutembelea Monasteri ya Fumbo la Umwilisho na kuadhimisha
Ibada ya Misa Takatifu, mahali alipoishi Mtakatifu Theresa wa Avila. Itakumbukwa
kwamba, Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania limeandaa kongamano la kimataifa la vijana
kutoka Barani Ulaya litakalofanyika mjini Avila kuanzia tehe 5 hadi tarehe 9 Agosti
2015. Maaskofu wanaandaa mbinu na mikakati itakayoliwezesha Kanisa nchini humo kuwa
ni chombo cha huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Wanaangalia
jinsi ya kuwa na mgawanyo bora zaidi wa Mapadre kwa ajili ya huduma kwa Familia ya
Mungu nchini Hispania sanjari na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa mwaka 2016
– 2020. Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.