2015-03-02 08:56:06

Acha woga!


Mpendwa msikilizaji wa kipindi chetu cha Kanisa la nyumbani, Tumsifu Yesu Kristo!! Kwa mara nyingine tena tunakukaribisha katika kipindi chetu kizuri sana cha Kanisa la nyumbani, kipindi ambacho tunajaribu kuchachafyana yale yenye kutukumbusha na kutuhamasisha juu ya Ukristo hai, Ukristo muwajibifu, Ukristo wa vitendo, Ukristo wenye mashiko, maisha hai ya imani yenye kushuhudia upendo wa Mungu kwa maneno na matendo. RealAudioMP3

Mtaguso Mkuu wa II wa Vatican, umeliunda, ukulifunda na kulijenga Kanisa katika sura ya kimisionari yenye kukidhi mahitaji ya nyakati zetu hizi. Kanisa linalowakumbatia wote kama familia mmoja, Kanisa linalojali maisha ya mtu mzima kiroho na kimwili. Ni kwa mtazamo huo, pamoja na kushughulikia mambo yale ya kiroho kama maisha ya sala na Ibada, toba na wongofu; Kanisa pia linajituma sana katika kutoa huduma za kijamii kwa watu. Na kanisa letu hili, kama Mama na Mwalimu, anawakumbatia na kuwagusa binadamu wote. Sio Mama wa Wakristo tu au wakatoliki tu. Ndiyo maana Mama Kanisa katika mafundisho na huduma zake, hulenga kumjenga, kumsaidia, kumwinua, kumlinda na kumwongoza kila binadamu.

Na sisi sote tulio waana wa Kanisa, wana familia ya Mungu, tunatekeleza utume huu pamoja na Kanisa zima. Tunaalikwa kujenga na kuimarisha sana ile tabia ya kumtazama na kumsaidia jirani awaye yeyote. Haijalishi anaabudu nini au anaamini nini au amegeukia wapi. Hati za Mtaguso Mkuu wa II wa Vatikani ambazo tumekwisha kuzipitia hivi karibuni, zimetuelekeza tuweje na tutende namna gani; ili sote tunaofundishwa na Mama Kanisa, tufanane na namna Kanisa linavyofundisha na kutenda.

Baada ya kuyasikia mafundisho yote kutoka katika hati 16 za Mtaguso Mkuu wa II wa Vaticani, sasa ni bidii kwetu kuyamwilisha mafundisho yale katika maisha yetu ya kila siku. Kusoma au kujifunza tu haitoshi, yapaswa pia kuishi kile ambacho tumejifunza. Sasa ili tuyaweke katika vitendo mafundisho yetu, tunahitaji nyenzo zifuatazo. Sikia!

Ya kwanza ni Imani. Nyakati zetu hizi na nyakati zote ambapo kuna kelele nyingi za yule mwovu anayetaka kutuvuruga na kulivurug Kanisa, tunahitaji kujiimarisha zaidi katika Imani. Tumwamini Mungu, kwa njia ya Mwanaye Kristo Yesu, ndani ya Kanisa. Hata tunapopata au kusikia vitisho na mitikisiko ya kiimani, au tunapokuwa katika miyumbo ya kimaisha, tuendelee kukipokea kikombe cha Wokovu na kuliitia jina la Bwana; Tumkazie macho Kristo Yesu anayetualika daima akisema ‘njoni kwangu ninyi mnaosumbuka na kulemewa na mizigo nami nitawapumzisha’. Tunahitaji silaha ya sala ya kweli, sala kunjufu ili tuwe salama katika mambo yote. Wengi wetu huwa tunaasi imani yetu kwa siri au kwa uwazi pale tunapohisi mitetemeko ya maisha. Imani huokoa!

Ya pili ni Usikivu! Mama Kanisa Mtakatifu kwa njia mbalimbali hutuandalia mafundisho mazito yaliyosheheni hekima kubwa, yenye lengo la kuturutubisha sisi watoto wa Kanisa kiroho na Kimwili. Tena Mafundisho ya Mama Kanisa yanagusa kila kona ya maisha na kwa kila rika la watu. Ni jukumu letu kujenga utamaduni wa kuwa wasikivu. Tuisikie sauti pole ya Mama Kanisa, anapotuelekeza mambo mbalimbali.

Mara nyingi Mama Kanisa amehuzunishwa na ukaidi wa watoto wake mwenyewe. Na pengine kumekuwa na utamaduni wa upuuziaji wa mambo, ambapo baadhi ya waana Kanisa wamekuwa mstari wa mbele kulipinga Kanisa waziwazi au kwa siri, hawajawa tayari kumsikia Mama Kanisa anafundisha na anataka nini, badala yake kumekuwa na kushabikia, kutetea au kuanzisha mifumo ya aibu na angamizi kwa familia ya binadamu. Mpendwa msikilizaji, mwaliko ni huu: tufikiri pamoja na Kanisa, tutende pamona na Kanisa, kaza mwendo, tushikane mikono: twende pamoja!!

Nyenzo ya tatu ni Ujasiri! Hilo ni moja ya paji la Roho Mtakatifu. Tunahitaji ujasiri katika kuyaishi mafundisho ya Mama Kanisa. Wakati fulani tunaweza kujikuta tumezungukwa na wapinzani wa Kanisa kiasi hata kwa bahati mbaya tukashawishika kuficha imani yetu. Hapo tutakuwa wanafiki. Kuwa jasiri! Hata wakuseme, wakucheke, wakutukane, wakudharau kwa sababu ya imani yako, wewe kuwa jasiri, acha uwoga. Ukiwa muoga-muoga katika maisha ipo siku utajidhulumu hata wewe mwenyewe. Woga tunaopaswa kuwa nao ni woga wa kumwasi Mungu tu! Katika sala fulani huwa tunamwomba Roho mtakatifu tukisema ‘utujalie woga mwema, tusimwache Mungu wetu’.

Huwa inashangaza nyakati fulani kuona kuwa watu wanaogopa kutenda wema eti wasije wakasemwa na watu. Au mtu anaogopa kusema ukweli unaookoa, ukweli unaoponya, eti asije akachukiwa. Au mtu anaogopa kuishi kiadilifu kinyume cha wengi eti asije akachekwa au akatengwa na wenzake. Woga wa namna hii unatupatia kishawishi cha kujisawazisha na kila mtu. Mwishowe tutajisawazisha na mashetani, kaa chonjo!*. Tunahitaji ujasiri katika kufikiri, ujasiri katika kusema na ujasiri katika kutenda; huku tukiongozwa na Hekima ya ki-Mungu, inayomwilishwa katika mafundisho ya Mama Kanisa. Uwe jasiri mwenye hekima, hapo utawaokoa wengi na utajiokoa mwenyewe pia.

Nyenzo ya mwisho kwa leo ni ‘bidii ya daima’. Mpendwa msikilizaji, kazi ya Ukombozi wa mwanadamu kiroho na kimwili na jambo endelevu. Ni suala la kila sasa na kila siku. Huwa inatokea mara nyingi tunaanza kutenda mambo mema kwa kasi nzuri sana, na hali njema inaoneka wazi. Lakini kwa bahati mbaya, juhudi hiyo inakuwa sio dumifu. Kuna ulegevu-uzembe-baridi fulani katika kudumu katika kutenda mema. Mama Kanisa yeye hachoki, kila siku na daima tunasikia mambo mapya akitufundisha na kutukumbusha, akituelekeza na kutuongoza. Hakati tamaa, bidii kama mwanzoni! Nasi pia tukitaka maendeleo yanayoonekana, tunapaswa kuwa na bidii ya daima katika kuyamwilisha yote tunayofundishwa.

Ninakutakia bidii njema na udumifu, amani na baraka katika kipindi hiki cha Kwaresma, na asante kwa kuisikiliza Radio Vatican!

Kutoka katika Studio za Radio Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.