Jumuiya ya Kimataifa imepiga hatua kubwa katika mchakato wa kuhakikisha kwamba, watu
wengi zaidi wanashiriki kikamilifu katika haki ya maendeleo, wakati huu Jumuiya ya
Kimataifa inapofanya kumbu kumbu ya miaka thelathini, tangu Umoja wa Mataifa ulipotoa
Azimio la Haki ya Maendeleo.
Lakini ikumbukwe kwamba, Jumuiya ya Kimataifa
hadi leo hii inakabiliwa na changamoto kubwa za maendeleo kutokana na umaskini mkubwa
wa hali na kipato, unaoendelea kunyanyasa utu na heshima ya binadamu wapatao billioni
2.2, sawa na asilimia 15% ya idadi ya watu duniani.
Bado kuna umati mkubwa
wa watu ambao hawana huduma bora za afya, elimu na kwamba, wanaishi katika mazingira
magumu, kiasi kwamba, kuna pengo kubwa kati ya matajiri na “akina yakhe pangu pakavu
tia mchuzi”. Kuna vitendo vya kigaidi vinavyoendelea kutishia usalama wa maisha na
mali za watu bila kusahau athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na myumbo wa uchumi
kimataifa. Kimsingi, haya ni mambo yanayochangia kukwamisha mchakato wa kudumisha
misingi ya haki, amani na utulivu duniani.
Haki ya maendeleo kadiri ya Mafundisho
Jamii ya Kanisa haina budi kujikita katika umoja, mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa
kwa kutambua kwamba, wote wanaunda familia ya binadamu; usawa, utu na heshima ya binadamu;
matumizi sahihi ya rasilimali ya dunia kwa ajili ya mafao ya wengi; maendeleo yanapaswa
kumshirikisha mtu mzima: kiroho na kimwili na kwamba, binadamu anapaswa kuwa ni dira
ya mipango na mikakati ya maendeleo kiuchumi na kijamii. Ili kuwa na uwiano mzuri
wa maendeleo, kuna haja ya kujikita katika kanuni ya auni na mshikamano.
Mambo
haya yanategemeana ili kusongesha mbele mchakato unaopania kumletea mwanadamu maendeleo
endelevu: kiroho na kimwili. Huu ni mchango wa kina uliotolewa hivi karibuni na Askofu
mkuu Silvano Maria Tomasi, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican katika Ofisi za Umoja wa
Mataifa zenye makao yake makuu mjini Geneva, katika mkutano wa kumbu kumbu ya miaka
thelathini tangu Umoja wa Mataifa ulipotoa Azimio la Haki ya Maendeleo. Utu, heshima
na haki msingi za binadamu ni mambo msingi sana katika mchakato wa maendeleo endelevu
kama anavyobainisha Baba Mtakatifu Francisko.
Ukosefu wa usawa kati ya watu
ni kati ya mambo yanayoendelea kusababisha chuki na kinzani nyingi za kisiasa na kijamii.
Utu na heshima ya binadamu viwe ni dira katika utekelezaji wa mikakati ya maendeleo
kiuchumi na kisiasa duniani, changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa na kwa wadau mbali
mbali, vinginevyo, uchoyo na ubinafsi vitatawala na hivyo kusababisha majanga katika
maisha ya watu. Mshikamano ni mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kufanya kazi kwa pamoja
kwa ajili ya mafao ya wengi, ili kuondoa vikwazo vinavyokwamisha mchakato wa maendeleo
na mafao ya wengi. Hiki ni kielelezo makini kinachotoa kipaumbele cha kwanza kwa maisha
ya binadamu na wala si vitu, ili kuondokana na tabia ya uchu wa mali inayopata chimbuko
lake katika ubinafsi na uchoyo.
Ikumbukwe kwamba, kila binadamu ana haki na
wajibu wa kujipatia maendeleo, kwani hii ni sehemu ya haki yake kama inavyobainishwa
na Umoja wa Mataifa; kwa kuheshimu usawa, huku mwanadamu akipewa kipaumbele cha kwanza
katika mikakati yote hii, hasa wakati huu, Jumuiya ya Kimataifa inapokabiliana na
changamoto ya ukosefu wa ajira na uwepo wa wimbi kubwa la wahamiaji linalotafuta nafuu
na ubora wa maisha.
Mikakati ya maboresho katika biashara ya kimataifa inaweza
kusaidia kupunguza baa la umaskini duniani pamoja na kuendeleza mchakato wa maboresho
ya hali ya maisha ya watu katika Jamii. Kumbe, mikakati ya maendeleo kwa siku za usoni
haina budi kuvalia njuga mambo ambayo yanaendelea kusababisha baa la umaskini, njaa
na maradhi duniani; kwa kulinda na kutunza mazingira; kwa kuboresha nguvu kazi ili
kuzalisha kwa tija, ubora na viwango; kwa kulinda na kuendeleza familia kama kikolezo
muhimu katika mchakato wa maendeleo ya binadamu: kiuchumi na kijamii.
Jumuiya
ya Kimataifa anasema Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi, haina budi kujenga na kudumisha
utandawazi wa mshikamano na kuondokana na na mwelekeo wa sasa wa sera na mikakati
ya kiuchumi isiyojali wala kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya watu wengi duniani.
Na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahii ya Radio Vatican.