2015-02-26 08:50:44

Yaani, sipati picha!


Waafrika wana imani kubwa sana kwa Mungu na kwa mahoka. Mahali wanapokutana na Mungu kwa njia ya kutambika au kuteta mahoka panatofautiana kati ya kabila na kabila. Wako wanaotambika chini ya mti fulani wa pekee au ndani ya kichaka fulani au hata msituni, wengine karibu ya mto mkubwa au penye bwawa. Makabila mengi wanatambika chini ya kichuguu, au mlima mrefu unaojitokeza peke yake sehemu iliyolala tambarare. Mahali hapo pa tambiko ni pa kukutana binadamu na Mungu kwa njia ya mahoka.

Wakati wa matambiko ni mwafaka ambapo mwafrika anatafakari hali halisi ya maisha yake na kutafuta kuyaelewa mawazo ya Mungu juu ya maisha yanayomsibu hasahasa akizungumza na mahoka yake. Mahali pa namna hiyo tungeweza kupaita patakatifu.

Leo tutasikia kituko kilichotokea kwenye mlima mrefu uliokuwa unajitokeza peke yake katika uwanda tambarare huko Galilea. Wenyeji waishio kandokando ya mlima huo walikuwa na utamaduni kama wa waafrika, ule wa kwenda kutolea sadaka kwa Mungu chini ya mlima huo ili kuomba mvua na rutuba ya ardhi kwa ajili ya mazao yao na baraka kwa mifugo yao. Kwa hoja hiyo mlima huo ukaja kuitwa mlima mtakatifu. Injili haitaji jina la mlima huo, bali inautaja kuwa ni mlima mrefu.

Labda kwa hoja kwamba mlima pekee uliokuwa umeinuka zaidi katika uwanda ule ulikuwa ni Tabor basi ukaunganishwa na masimulizi ya kugeuka sura kwa Yesu. Leo Mwinjili anatuletea mandhari ambayo umwandani wa fikra ya kibinadamu unafikia hatima ya pekee ya kuungana na kuweza kutawaliwa na kufikiri kadiri ya fikara za kimungu. Kwa hiyo, masimulizi hayo ni ya kiteolojia siyo ya kihistoria, hivi yanataka kutupatia ujumbe na fundisho maalumu la maisha kwa wakati huu wa Kwaresima. Hebu endelea kufuatia.

Injili inaanza na sura ya tisa aya ya pili, yenye maneno haya muhimu, “Hata baada ya siku sita,” Yaonekana siku hiyo imetajwa kutokana na umuhimu wa tukio lililokuwa limetokea kabla yake. Nalo ni kuwa, kabla ya siku hizo sita Yesu alizungumza juu ya hatima ya maisha yake. Kwamba, “Imempasa Mwana wa Adamu kupatwa na mateso mengi, na kukataliwa na wazee, na wakuu wa makuhani, na waandishi na kuuawa, na baada ya siku tatu kufufuka.” Lugha hii ya Yesu haikueleweka kwa mitume hadi ikamsababishia Petro kuitwa shetani.

Hata hivyo, ujumbe huo mzito wa Yesu, haukuachwa tu upite bila kufanyiwa kazi ya kuutafakari hasahasa kwa upande wa Petro aliyeambiwa waziwazi kuwa ni shetani. Kadhalika kwa wanafunzi na wafuasi baada ya kuishi na Yesu kipindi cha takribani miaka mitatu wakimfuatilia nyendo na mahubiri yake, hivi walipomsikia maneno hayo wakayatafakari na kwa vyovyote yalieleweka na yakaanza kufanya mageuzi mioyoni mwao, yaani sasa wanafunzi wameanza kuelewa kwa akili ya kimungu maneno aliyokuwa ameyasema mwalimu wao.

Katika kipindi hiki cha pakee Yesu yuko pamoja na mitume watatu tu, waliopata fursa ya kushiriki kupata kwa kina tafakari mpya, ya kuwa katika mang’amuzi hayo ya arkana (fursa ya kutambua siri ya mafumbo makuu), yaani kutafakari uso wa Mungu (Yesu) kule mlimani.

Hatimaye, baada ya siku sita Yesu akawatwaa Petro na Yakobo na Yohane akawaleta juu ya mlima mrefu faraghani peke yao.” Hata wakati wa manabii wanapotaka kuteta jambo la pekee na wanafunzi wao walikuwa wanaenda pahala pa faragha. “Akageuka sura yake mbele yao.” Neno hili “kugeuka” kwa kigiriki ni metamorfos linatumika pia katika somo la jiografia kumaanisha kubadilika kwa mwamba kutokana na moto mkali sana na mkandamizo unaogeuza mawe chini ya ardhi hadi yanakuwa almasi au dhahabu nk.

Kwa hiyo sasa mambo katika Kristo yanageuka na kuonekana kuwa tofauti na jinsi inavyoweza kuonekana kwa macho ya kawaida. Macho ya watu wanaoishi katika tambarare ni tofauti na watu wanaoangalia kutoka juu mlimani. Watu wa tambarare wanamwona Yesu kuwa kama mwenzao tu, au kama mtu aliyelaanika au aliyekosa mwelekeo na maisha yamemshinda. Kumbe Yesu anageuka, anabadilika. Hii yaweza kuwa fikara kwetu kwamba huwezi kukaa na Kristu au ukajidai kuwa ni mkristu bila kuwa na mtazamo wa mabadiliko au mageuzo ya maisha. Unapoingia katika fikra za Kimungu unaingia katika metamorfosi na fikra zinabadilika.

“Mavazi yalimeremeta, yakawa meupe mno,” yaani nguo au mwili wa mtumwa alioutwaa wa kibinadamu, ulioonekana kama ni udhaifu na kushindwa kwa bure, sasa ni metamorfosi, umeangazwa na mwanga wa Mungu. Katika sifa hii ya weupe, Marko peke yake anatia chumvi na kusema kwamba “mavazi yalikuwa meupe kiasi kwamba hakuna dobi duniani yeyote anayeweza kuyafanya meupe hivyo.” Akimaanisha kuwa katika nafsi ya Yesu kuna mwanga wa hali ya juu kabisa, kwa sababu unamwakisi Mungu mwenyewe. Hakuna mtu mwingine anayeweza kuwa mweupe hivyo isipokuwa Kristu peke yake.

“Wakatokewa na Eliya na Musa, nao walikuwa wakizungumza na Yesu.” Manabii hawa wanawakilisha Neno la Mungu katika Agano la Kale, yaani Torati (amri) na Manabii. Wanafunzi wale watatu walishuhudia kubadilika huko kwa yule aliyetabiliwa na Neno la Mungu Torati na manabii. Mabadiliko hayo yamedhihirika katika Yesu aliyetoa maisha yake msalabani kwa ajili ya metamorfosi, yaani kufufuka. Katika kutafakari fumbo la mateso ha kifo cha Msalaba mlimani Golgota unaweza kufahamu maana ya ufufuko.

Petro hakuwa amefahamu kinaganaga kilichokuwa kinatokea akabaki kuweweseka: “Rabi ni vizuri sisi kuwapo hapa; na tufanye vibada vitatu, kimoja chako, wewe, kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya”. Haieleweki kidhahiri alitaka kumaanisha kitu gani. Labda alitaka kuturudisha kwenye hema au banda lile la jangwani Waisraeli walipokuwa wanasafiri, lakini kwao ilionesha watu walio safarini na wamechoka wanataka kutulia au kupumzika.

Kumbe mang’amuzi yetu ya kiroho yanaweza kutusaidia kuelewa zaidi maana ya mabanda hayo matatu ya Petro, yaani baada ya kulisikia Neno la Mungu, hatuwezi haturudi mara moja kwenye maisha ya kila siku yaani maisha ya kifamilia kwani yanaonekana kama kutuogopesha. Mathalani, baada ya kusikia mahubiri mazuri ya jumapili yanayotufanya tujisikie tuko paradisini, hapo tunapata woga inapotubidi turudi katika maisha ya kawaida yasiyolingana na mahubiri tuliyosikia. Kumbe Yesu aliwapandisha wanafunsi wake mlimani, ili baadaye aweze kuwarudisha tena bondeni kwenye ulimwengu ili waweze kuubadili ulimwengu.

Kisha “kukasikika sauti ikatoka katika winguni.” Hapa wingu lamaanisha ulimwengu wa Mungu. Kutoka kwa Mungu mbinguni kuna mwonekano wa ukweli wa mambo. Sauti ya kweli toka mbinguni inasema: “Huyu ni Mwanangu mpendwa wangu msikieni yeye.” Hiyo ni sauti pekee inayotudai kumsikiliza Mwana pekee anayeongoza kwenye maisha ya kweli.

Hapo wanafunzi wanashuka bondeni na wako peke yao na Yesu tu, kisha, “akawakataza wasimweleze mtu waliyoyaona hata Mwana wa Adamu atakapokuwa amefufuka katika wafu.” Wanakatazwa kwa sababu watu hawataelewa wakiambiwa. Hata sisi tunaweza kuwa na wakati mgumu wa kuweza kushirikisha mang’amuzi ya metamorfosi ya binafsi. Unaposhuka toka mlimani na kupambana na maisha ya kawaida. Tunaalikwa kufanya mang’amuzi na Neno la Mungu.

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.