2015-02-10 07:16:06

Siku ya Wagonjwa Duniani kwa Mwaka 2015


Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya 23 ya Wagonjwa Duniani inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 11 Februari, anawaalika waamini na watu wenye mapenzi mema kuongozwa na hekima ya kiroho wanapowahudumia wagonjwa, kwa kujitoa bila ya kujibakiza. RealAudioMP3

Kauli mbiu ya maadhimisho haya ni “Nalikuwa macho kwa kipofu, nalikuwa mguu kwa aliyechechemea”. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kujisadaka kwa ajili ya wagonjwa, kwa kutambua kwamba, wao pia wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Itakumbukwa kwamba, Siku ya Wagonjwa Duniani ilianzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II yapata miaka ishirini na mitatu iliyopita, ili kuwasaidia watu wanaojitolea maisha yao kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa, waweze kutekeleza dhamana hii kwa unyofu.

Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu anawaalika waamini kufanya tafakari ya kina kutoka katika Kitabu cha Nabii Ayubu, sura ya 29: 15, yaani “Nalikuwa macho kwa kipofu, nalikuwa mguu kwa aliyechechemea” Muda ambao mtu anautumia kwa ajili ya huduma kwa mgonjwa ni muda mtakatifu, ni kielelezo cha sifa kwa Mungu kwa ajili ya faraja kwa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu pamoja na kukumbuka kwamba, Yesu alikuja hapa duniani si kwa ajili ya kutumikiwa bali kutumikia na kutoa uhai wake ili uweze kuwa ni fidia ya wengi.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya 23 ya Wagonjwa Duniani anakazia kwa namna ya pekee hekima ya moyoni kwa ajili ya kuwasindikiza wagonjwa katika shida, mateso na mahangaiko yao, wakati mwingine katika hali ya ukimya na kutokana na uwepo huu wa karibu wanapata faraja na kujisikia kwamba, kweli wanapendwa na kuthaminiwa. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwa uchungu mkubwa aibu inayojificha kati ya watu wanaotaka na kutafuta maisha bora kwa ud ina uvumba, kiasi hata cha kukumbatia utamaduni wa kifo kwa kudhani kwamba, wagonjwa katika mateso na mahangaiko yao ya ndani hawana sababu ya kuendelea kuishi.

Baba Mtakatifu anawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujisadaka kwa ajili ya kuwasaidia wagonjwa, kwa kutenga muda maalum wa kuwatembelea na kuwasaidia bila ya kuwa na haraka ya maisha na visingizio vya kazi nyingi. Kwa kufanya hivi watu wanasahau umuhimu wa mtu kujisadaka kwa ajili ya jirani zake, kama kielelezo makini cha imani tendaji, kwani Yesu anawakumbusha wafuasi wake kwamba, yale yote waliyomtendea mmoja kati ya wadogo hao amemtendea yeye!

Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutoka katika ubinafsi na undani wao, tayari kuwaendea jirani zao kama sehemu ya utekelezaji wa amri ya upendo kwa Mungu na jirani, kanuni maadili na alama makini katika mang’amuzi ya maisha ya kiroho, kwa kujisadaka kwa ajili ya wengine.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kusema kwamba, upendo hauna mipaka ya muda, hakuna mipaka ya kuwahudumia na kuwatembelea wagonjwa. Lakini anaonya kwamba, watu wasifanye kama wale rafiki zake Ayubu waliokuwa wanamtembelea, huku wakiwa na mwelekeo hasi juu ya maisha yake. Wao walidhani kwamba, ugonjwa wake ilikuwa ni adhabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu kutokana na dhambi alizotenda.

Upendo wa kweli unajikita katika umoja na mshikamano bila kuhukumu wala kutaka kumwongoa jirani, bali ni sehemu ya mchakato unaomkomboa mtu kutoka katika unafiki wa kutaka kuonesha kwamba, anampenda jirani yake kwa matendo yake mema, kumbe ni kinyume chake kabisa.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, mateso na mahangaiko ya binadamu yanapata majibu kamili kutoka katika Fumbo la Msalaba wa Yesu, kielelezo cha hali ya juu kabisa cha mshikamano kati ya Mungu na binadamu; sadaka ya hali juu kabisa inayoonesha huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Hili ni jibu makini katika shida na mahangaiko ya binadamu na hasa zaidi kwa watu wasiokuwa na hatia, chapa ya kudumu katika Mwili wa Yesu Kristo Mfufuka; madonda yake matakatifu ni kashfa na ukweli wa imani.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kusema kwamba, hata watu ambao wanaishi katika Fumbo la Mateso na Mahangaiko, wakiyapokea mateso na mahangaiko haya kwa imani na matumaini, wanaweza kuwa kweli ni mashuhuda hai wa imani inayofumbatwa katika mateso na mahangaiko hayo, jambo ambalo haliwezi kueleweka kwa urahisi na akili ya binadamu.

Baba Mtakatifu anawakumbuka Wakristo wengi wanaoendelea kushuhudia imani yao si kwa maneno matupu, bali kwa njia ya maisha yao yanayofumbatwa katika imani makini, ili kuwa kweli ni jicho kwa kipofu na miguu kwa mtu anayechechemea! Hawa ndio wale watu wanaokaa pembeni mwa wagonjwa wanaohitaji msaada wa daima: ili kuoga, kuvaa na kula chakula. Huduma hii hasa pale inapochukua muda mrefu inachosha na kugeuka kuwa ngumu.

Baba Mtakatifu anasema ni rahisi sana kuweza kumhudumia mgonjwa kwa siku chache, lakini kutoa huduma kwa mgonjwa kwa miezi au miaka na hasa pale ambapo mgonjwa hawezi tena kutoa shukrani kwa huduma, yataka moyo na imani thabiti! Baba Mtakatifu anasema, hii ndiyo hija ya utakatifu wa maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.