2015-01-30 15:00:13

Shikamaneni kwa ajili ya haki na amani!


Tume ya kitaalimungu kimataifa kati ya Kanisa Katoliki na Makanisa ya Kiorthodox ya Mashariki, ilianzishwa kunako mwaka 2003 kama matunda ya juhudi za pamoja za viongozi wa Makanisa ya Kiorthodox kwa kushirikiana na Baraza la Kipapa la uhamasishaji wa umoja wa Wakristo. Katika kipindi cha miaka kumi ya uhai wake, tume hii, imefanya upembuzi yakinifu wa historia ya Makanisa mintarafu umoja wao katika karne za kwanza kwanza, ili kujenga na kuimarisha umoja wa Kanisa kwa nyakati hizi.

Tume hii katika mkutano wake, uliokuwa unafanyika hapa mjini Vatican imechambua kwa kina na mapana maana na asili ya Sakramenti za Kanisa, lakini kwa namna ya pekee, Sakramenti ya Ubatizo. NI matumaini ya Kanisa kwamba, jitihada hizi zitaweza kuzaa matunda ya pamoja katika tafiti za kitaalimungu, ili kuwawezesha Wakristo kuishi daima katika udugu na urafiki.

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 30 Januari 2015 alipokutana na kuzungumza na Tume ya Kitaalimungu kimataifa kati ya Kanisa Katoliki na Makanisa ya Kiorthodox ya Mashariki, baada ya kuhitimisha mkutano wao mjini Roma. Baba Mtakatifu anawashukuru viongozi wakuu wa Makanisa haya kwa juhudi na jitihada zao katika kukuza na kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene.

Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu amemkumbuka na kumwombea Patriaki Ignazio Zakka Iwas wa Kanisa la Siro la Antiokia na Mashariki ya Kati, kutokana na juhudi zake katika kukuza na kudumisha majadiliano ya kiekumene. Anamwombea amani na furaha katika maisha ya uzima wa milele.

Baba Mtakatifu anasema, wakati huu, Wakristo wote wanashirikishana mateso na mahangaiko ya Wakristo huko Mashariki ya Kati, hususan Iraq na Syria. Anawakumbuka Wakristo na waamini wa dini nyingine wanaoishi katika kinzani, madhulumu na vita.

Baba Mtakatifu anasema, anaendelea kuungana waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, ili kuweza kupata suluhu ya kudumu, kwa kuomba wema na huruma ya Mungu kwa ajili ya wote walioguswa na kutikiswa na majanga haya. Wakristo wote wanahamasishwa kufanya kazi kwa pamoja, kwa kukubaliana pamoja na kuaminiana kwa ajili ya mchakato wa ujenzi wa haki na amani.

Mashahidi na watakatifu wengi waliojisadaka kwa ajili ya kumshuhudia Kristo katika Makanisa yote, waenzi na kuimarisha Jumuiya za Kikristo. Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwatakia kheri na baraka tele katika maisha na utume wao na kuwaomba kuendelea kumkumbuka katika sala.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.