2015-01-30 09:17:33

Papa kwenda mlimani kuanzia tarehe 22 - 27 Februari 2015


Watumishi na Manabii wa Mungu aliye hai, ndiyo kauli mbiu itakayoongoza tafakari ya maisha ya kiroho kwa Baba Mtakatifu Francisko pamoja na wasaidizi wake kuanzia tarehe 22 hadi tarehe 27 Februari 2015; mafungo yatakayoongozwa na Padre Bruno Secondin, Mkamelitani anayependa kuchambua Waraka wa Nabii Elia.

Ratiba elekezi inaonesha kwamba, mafungo haya yataanza Jumapili saa 12: 00 jioni kwa saa za Ulaya kwa Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu na baadaye Masifu ya jioni. Siku zinazofuata, mafungo yataanza saa 1:30 kwa Masifu ya asubuhi na kufuatiwa na tafakari ya kwanza hapo saa 3: 30 na baadaye maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu kwa pamoja. Saa 10:00 jioni, kutakuwa na tafakari ya pili na kufuatiwa na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu pamoja na Masifu ya jioni.

Ijumaa, tarehe 27 Februari 2015, siku ya mwisho ya mafungo, kutakuwa na adhimisho la Misa Takatifu kuanzia saa 1: 30 asubuhi na baadaye kuhitimisha mafungo hapo saa 3: 30 asubuhi.

Baba Mtakatifu na wasaidizi wake wa karibu, wataanza kutafakari kuhusu tema "Ondoka katika Kijiji chako". Tafakari hii itaendelezwa na kukuzwa kwa kupembua kwa kina na mapana hija ya kweli katika maisha ya mwamini; mizizi ya imani na ujasiri wa kuweza kusema hapana katika mkanganyiko wa mambo. Watatafakarishwa kuhusu njia za ukombozi kutoka katika mambo ya kidunia kwa kujikita katika ibada ya kweli.

Baba Mtakatifu pamoja na wasaidizi wake, watahimizwa kumwachia Mungu nafasi ili aweze kuwashangaza katika maisha na utume wao kwa kuanzisha mchakato wa kukutana na Mwenyezi Mungu sanjari na kuwaachia nafasi maskini, ili waweze kuwainjilisha. Ni tafakari ambayo itajikita pia katika ushuhuda wa haki na mshikamano wa upendo.

Siku ya mwisho, Baba Mtakatifu na wasaidizi wake, watafanya tafakari kuhusu umuhimu wa kupokea joho la Elia, ili waweze kuwa kweli ni Manabii wa udugu. Wakati wote wa mafungo ya maisha ya kiroho, hakutakuwepo na Katekesi wala mikutano ya faragha na Baba Mtakatifu, huu ni wakati wa kupanda Mlimani, ili kusali na kutafakari, tayari kujichotea nguvu katika maisha na utume wao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.