Baraza la Maaskofu Katoliki Croazia kwa kushirikisha na Shirikisho la Wakuu wa Mashirika
ya Kitawa na Kazi za Kitume, wameandika barua ya kichungaji kwa ajili ya Maadhimisho
ya Mwaka wa Watawa Duniani, uliotangazwa na Baba Mtakatifu Francisko na kuzinduliwa
rasmi Jumapili ya kwanza ya Kipindi cha Majilio.
Mwaka wa
Watawa utafungwa rasmi hapo tarehe 2 Februari 2016, Mama Kanisa atakapokuwa anaadhimisha
Siku kuu ya kutolewa Bwana Hekaluni, sanjari na Siku ya Watawa Duniani, iliyoanzishwa
na Mtakatifu Yohane Paulo II.
Katika Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani,
watawa kwa namna ya pekee wanahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba wanaishi
na kumwilisha furaha ya Injili katika maisha yao, huku wakiendelea kuishi wito ambao
ambao ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu
na ustawi wa maisha ya binadamu.
Ni changamoto ya kuendelea kumwilisha karama
za mashirika haya katika maisha na utume wa kwa Kanisa mahalia, kwani hii ni zawadi
kubwa kutoka kwa Roho Mtakatifu kwa ajili ya Kanisa. Mwaka wa Watawa Duniani iwe ni
fursa kwa watawa kusoma alama za nyakati na kusikiliza kwa makini sauti ya Roho Mtakatifu,
ili kuepuka kinzani zinazoweza kujitokeza katika nadharia na uhalisia wa maisha; kwa
kujifunga katika mitazamo yao na kusahau kile ambacho Roho Mtakatifu anawataka kutenda
kwa wakati huu.
Maaskofu wanatambua kwamba, watawa wanakabiliwa na kinzani
za ukosefu wa miito katika Mashirika yao, hali ambayo inakatisha tamaa kwa ajili ya
uhai wa Mashirika haya kwa siku za usoni. Kinzani hizi ziwe ni changamoto ya kufanya
tafakari ya kina kuhusu maisha na utume wao, tayari kukubali kufanya mabadiliko makubwa
yatakayoleta mvuto na mguso kwa vijana wa kizazi kipya; maisha ambayo yanajikita katika
ushuhuda wa mashauri ya Kiinjili.
Watawa waoneshe moyo wa toba na wongofu
wa ndani, kama mtu binafsi na jumuiya, ili kweli waweze kukumbatia neema na baraka
zinazotolewa na Kristo pamoja na Kanisa lake, wanapojitahidi kumfuasa kwa uaminifu
na udumifu bila ya kumezwa na malimwengu.
Watawa wanahamasishwa kuendelea kumwamini
na kumtumainia Mwenyezi Mungu katika maisha yao, ili kuishi na kutenda mintarafu mwanga
wa imani, kama kielelezo makini cha uwepo endelevu wa Mungu kati ya watu wake. Watawa
wawe ni mashahidi amini katika mapambano dhidi ya umaskini, ukosefu wa imani na migawanyiko
kati ya watu.
Mwaka wa Watawa Duniani, uwe ni kikolezo cha thamani kubwa ya
maisha ya kitawa nchini humo. Watawa waendelee kuwa ni watu wa sala na tafakari ya
Neno la Mungu; watu wanaomwilisha imani katika huduma kwa Mungu na jirani. Baraza
la Maaskofu Katoliki Croatia linasema kwamba, tarehe 14 Machi 2015 watawa nchini humo
watafanya hija ya maisha ya kiroho, itakayowakutanisha kwenye Madhabahu ya Bikira
Maria wa Bistrica.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili
ya Radio Vatican.