Nembo ya maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, utakaozinduliwa rasmi Jumapili ya
kwanza ya kipidni cha Majilio kwa mwaka 2014 inaonesha kwa kina na mapana tunu msingi
zinazofumbatwa katika maisha ya kitawa, mwendelezo wa kazi ya Roho Mtakatifu, ambaye
daima analitajirisha Kanisa kwa karama na tunu mbali mbali zinazojidhihirisha katika
mashauri ya Kiinjili. Kwa njia hii, Roho Mtakatifu analiwezesha Kanisa kuendelea kuonesha
Fumbo la uwepo wa Kristo ulimwenguni.
Nembo hii
inamwonesha njiwa, ambaye kimsingi ni alama ya amani, changamoto kwa watawa kuwa kweli
ni vyombo vya upatanisho, haki na amani ndani ya Kristo. Njiwa kadiri ya Mapokeo ya
Mama Kanisa anaonesha uwepo wa Roho Mtakatifu, chemchemi ya maisha na mwendelezo wa
kipaji cha ugunduzi. Njiwa anawakumbusha walimwengu kuhusu kazi ya uumbaji iliyofanywa
na Mwenyezi Mungu, mwaliko wa kulinda na kutunza mazingira, kazi ya uumbaji, kwa ajili
ya mafao ya kizazi cha sasa na kile kijacho.
Roho Mtakatifu anaonesha maisha
mapya ambayo kwa njia ya Maji na Roho Mtakatifu, waamini wanaifia dhambi na kuzaliwa
upya katika Fumbo la Pasaka, kumbe, Roho Mtakatifu anawaweka walimwengu wote wakfu
kwa Kristo.
Alama ya maji katika Nembo ya Mwaka wa Watawa Duniani ni mwaliko
kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutafakari kwa kina kuhusu zawadi ya uumbaji
na dhamana ambayo mwanadamu amekabidhiwa na Mwenyezi Mungu. Watawa waliowekwa wakfu,
wanatumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia; kwa kuwashirikisha
karama za Mashirika yao, wale wote wanaowahudumia kiroho na kimwili.
Watawa
wanakumbushwa kwamba, wao ni wahudumu wa karama mbali mbali katika maisha ya watu,
hata kiasi cha kujisadaka kama ushuhuda makini wa imani tendaji kwa Kristo na Kanisa
lake, kama ambavyo imejionesha katika historia ya Kanisa. Watawa wanaalikwa kukumbatia
Msalaba, kielelezo cha upendo na hekima ya Mungu kwa binadamu. Kanisa ni chombo cha
wokovu na huruma ya Mungu, linapenda kuganga na kuponya, wale wote wanaokimbilia huruma
na upendo wa Mungu katika maisha yao.
Nyota tatu ambazo zinajionesha katika
Nembo hii ni kielelezo kwamba, Watawa wamewekwa wakfu katika Fumbo la Utatu Mtakatifu,
kumbe wanaalikwa kushuhudia kwa maneno, lakini zaidi kwa njia ya matendo yao, udugu
unaofumbatwa katika huduma kwa Familia ya Mungu. Watawa wanasukumwa kuwaonjesha walimwengu
upendo unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, kama alivyofanya Bikira
Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Bikira Maria ni kielelezo na mfano wa kuigwa na Watawa
katika maisha na utume wao, ni Mama, Msimamizi na Mwombezi wa Watawa wote.
Maisha
ya kitawa kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko yanamwilishwa na watu kutoka katika
kila kabila, lugha na jamaa, changamoto kwa Watawa hao kuonesha kweli ile karama ya
Roho Mtakatifu inayotenda kazi ndani mwao, huku wakisukumwa kwenda pembezoni mwa jamii
ili kuwatangazia Watu wa Mataifa Furaha ya Injili.
Kauli mbiu inayoongoza
maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani ni “Vita Consecrata in Ecclesia hodie. Evangelium,
prophesia spes”, yaani “Maisha ya kuwekwa wakfu ndani ya Kanisa; Unabii na Matumaini”.
Kauli mbiu hii inakazia kwa namna ya pekee kabisa utambulisho wa maisha ya kitawa,
mwelekeo wake, mang’amuzi na uzoefu wao katika maisha na utume wa Kanisa ulimwenguni.
Watawa ni kielelezo cha neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu ndani ya Kanisa,
wanaoendelea kuhamasishwa na Mama Kanisa kuonesha udumifu katika hija yao kwa Watu
wa Mataifa na tamaduni mbali mbali hadi utimilifu wa nyakati.
Na Padre Richard
A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.