Baba Mtakatifu Francisko amefanya mabadiliko juu ya utaratibu wa Maaskofu wakuu wapya
kuvikwa Pallio Takatifu, mabegani mwao, kielelezo cha Yesu Kristo Mchungaji mwema,
kwamba, kuanzia tarehe 29 Juni 2015, hawatavikwa tena na Baba Mtakatifu na badala
yake, watavikwa na Mabalozi wa Vatican kwenye nchi husika.
Kadiri ya Mapokeo
ya Kanisa Katoliki, Maaskofu wakuu walikuwa wanavikwa Pallio Takatifu katika Ibada
ya Misa Takatifu ya Mitume Petro na Paulo, miamba wa imani, inayoadhimishwa na Mama
Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 29 Juni. Tukio hili sasa litafanyika kwenye Majimbo
makuu na kazi hiyo itafanywa na Mabalozi wa Vatican, lengo ni kuhakikisha kwamba,
Familia ya Mungu na hususan Maaskofu wa Majimbo mahalia wanaounda Jimbo kuu, wanashiriki
kikamilifu katika tukio hili la neema na baraka ya Mungu.
Monsinyo Guido Marini,
Mshereheshaji mkuu wa Ibada za Kipapa katika mahojiano maalum na Radio Vatican anabainisha
kwamba, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kukazia uhusiano uliopo kati ya Maaskofu
wakuu ambao wameteuliwa katika kipindi cha mwaka na Makanisa mahalia, ili kutoa nafasi
hata kwa waamini katika Majimbo haya kushiriki katika matukio muhimu kama haya ndani
ya Kanisa.
Kwa mantiki hii, bado kuna mwendelezo wa umoja na mshikamano kati
ya Khalifa wa Mtakatifu Petro na Maaskofu wakuu pamoja na kuonesha mshikamano wa dhati
na Kanisa mahalia. Mabadiliko haya yanatajirisha tukio la kuwavika Maaskofu wakuu
Pallio Takatifu, kielelezo cha mshikamano wao na Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.