Viongozi wa kidini nchini Marekani wamemwandikia barua ya wazi Rais Barack Obama wa
Marekani, kumtaka kuvalia njuga tatizo la ukosefu wa haki na amani huko Mashariki
ya Kati pamoja na kuhakikisha kwamba, kinzani za kivita kati ya Israeli na Palestina
zinafikia ukomo, ili watu waanze tena mchakato wa upatanisho, ujenzi wa amani na maendeleo.
Kuchelewa kupata ufumbuzi wa kudumu wa migogoro hii, kutaendelea kusababisha maafa
na majanga makubwa kwa watu wasiokuwa na hatia.
Viongozi wa kidini wanasema,
suluhu ya kivita haina mashiko, bali jambo la msingi ni kuwawezesha wahusika wa pande
hizi mbili kuketi kwa pamoja na kuanza mchakato wa majadiliano, kwani historia inaonesha
kwamba, vita imeendelea kuwa ni mama wa vita duniani. Viongozi wa Israeli na Palestina
hawana budi kutambuana kama mataifa mawili yanayojitegemea na kwamba, yanapaswa kushirikiana
kwa dhati.
Viongozi wa kidini wanasema, kuna mambo makuu matatu yanayopaswa
kupewa kipaumbele cha kwanza katika mchakato wa majadiliano kati ya wadau wakuu kwenye
mgogoro wa kivita kati ya Israeli na Palestina: amani, usalama na pande hizi mbili
kutambuana kama mataifa mawili huru kabisa. Hapa kuna haja ya kuhakikisha kwamba,
matatizo na changamoto zinazoendelea kujitokeza zinapatia ufumbuzi wa kudumu, lengo
ni kusaidia wananchi wa mataifa mawili kuishi kwa amani na utulivu. Hapa Serikali
ya Marekani na Jumuiya ya Kimataifa vinaweza kutoa mchango wa hali ya juu ili kufikia
malengo ya amani na utulivu huko Mashariki ya Kati.
Viongozi wa kidini wanahitimisha
barua yao ya wazi kwa Rais Barack Obama wa Marekani, kwa kusema kwamba, mchakato wa
amani hauna budi kusindikizwa na juhudi za makusudi kutoka kwa viongozi wa kidini
kwa kushirikiana na Jumuiya za waamini. Viongozi wanashauri kupewa nafasi katika majadiliano
haya, kwani hata wao wanagusa na mateso na mahangaiko ya wananchi wengi huko Mashariki
ya Kati.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio
Vatican.