2015-01-29 07:49:22

Mwaka wa Watawa Duniani, kipindi cha neema na baraka!


Baraza la Maaskofu Katoliki Angola, Sao Tome na Principè katika Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani uliotangazwa na Baba Mtakatifu Francisko na kuzinduliwa rasmi Jumapili ya kwanza ya Kipindi cha Majilio linasema, hiki ni kipindi cha neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu. RealAudioMP3

Ni sehemu ya kumbu kumbu ya miaka hamsini tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipochapisha Waraka kuhusu Upendo Mkamilifu unaofafanua na kupembua kwa kina na mapana utume na maisha ya watawa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo.

Hii ni changamoto na mwaliko wa kufanya mageuzi ya kina, kwa kusoma alama za nyakati pamoja na kuendelea kujikita katika toba na wongofu wa ndani, ili kushuhudia ile furaha na unabii unaofumbatwa katika Mashauri ya Kiinjili na Maisha ya Kijumuiya. Mwaka wa Watawa utafungwa rasmi hapo tarehe 2 Februari 2016, wakati wa Maadhimisho ya Siku kuu ya kutolewa Bwana Hekaluni, sanjari na Siku ya Watawa Duniani, iliyoanzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II.

Maaskofu wanakumbusha kwamba, watawa wanapaswa kutambua kwamba, wao ni sehemu ya maisha na utume wa Kanisa mahalia na wala si kiraka katika Kanisa. Wanawajibu na utume usiokuwa na mbadala. Wanaitwa kushiriki katika maisha na utakatifu wa Kanisa. Kutokana na mwelekeo kama huu, Maaskofu wanawaalika Watawa na waamini wote kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya matukio mbali mbali kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani.

Maaskofu kwa namna ya pekee, wanawataka watawa kutoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia matendo makuu ya Mungu katika maisha yao kwa kuadhimisha Jubilee ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, kwa kukumbuka historia, changamoto na fursa mbali mbali zilizokuwepo, tayari kusonga mbele kwa imani na matumaini kwa Kristo na Kanisa lake, licha ya magumu na changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza.

Maaskofu wanatambua na kuthamini mchango mkubwa unaotolewa na watawa katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili; katika sekta ya elimu, afya na maendeleo endelevu ya binadamu. Kumbe, Mwaka wa Watawa Duniani ni kipindi cha kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa zawadi ya maisha ya kitawa ndani ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake.

Watawa wanahamasishwa kuendelea kuwa mstari wa mbele, kwa kuonesha uwepo wao pembezoni mwa jamii, ili kuwahudumia maskini na wote wanaotelekezwa na jamii, kama anavyohimiza Baba Mtakatifu Francisko.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.