2015-01-29 10:42:34

Amewatibua nyongo!


Kizungumkuti! Mtu kugeuzwa kuwa kiti cha kukalia. Ndugu yangu usishangae kusikia kwamba kuna binadamu kwa hiari yake na kwa kujua na kutaka mwenyewe anawakaribisha wageni kisha wanamgeuza kuwa kiti na kumkalia.


Yasemekana kuwa wageni hao hawaonekani kwa macho ya kawaida na wakitaka kusikika na kuonekana wanamtafuta mtu hasa aliye matatizo mazito ya maisha, wanamwingia na wanamgeuza kuwa koloni lao. Wakoloni hao wakisha kuingia mtazeeka pamoja kwani hawatoki wala hawawezi kutolewa na mtu yeyote. Hata mjuzi au fundi anayewafahamu wageni hao naye budi awe amekaliwa nao. “Ama kweli Belzebuli hawezi kumtoa Belzebuli mwenzake.” Anachofanya fundi huyo ni kuandaa ibada fupi ya kuwakaribisha wageni hao ili watengeneze urafiki na mtu huyo wanayemtaka kumkalia.


Katika ibada hiyo fundi atawapa wageni hao mambo wanayopenda kama vile ubani na vikorombwezo vingine vinavyonukia, mradi tu waweze kufika kumkalia na kutumia mdomo wa mtu huyo ili kujitambulisha majina yao, wanakotoka na wangetamani kufanyiwa nini. Waalikwa wengine kwenye ibada hiyo, wanakuwa wale waliokaliwa tayari na wageni kama hao, nao watabaki kutikisa vichwa vya kukubali kuwa wanawafahamu wageni hao na wanakotoka. Mtu huyo waliyemkalia wageni hao anaitwa kiti. Ili kuwafurahisha wageni, wakati mwingine kunafanyika ibada kuu yenye madhehebu ya kupiga ngoma na kucheza wiki mzima.


Ndugu zangu wageni hao si wengine bali ni mapepo, yanaitwa pia majini au masheitani. Inasikitisha lakini ni kweli kwamba kuna watu, kuna vijiji, miji na nchi nyingine zimeridhika kutawaliwa na madudu hayo. Mzaburi anasema: “Mbingu ni mbingu za Bwana, bali nchi amewapa wanadamu.” (Zaburi 115:16) Kumbe dunia hii aliyopewa binadamu na Mwenyezi Mungu ili aitawale imegeuzwa kuwa koloni linalotawaliwa na mapepo na binadamu mwenyewe amebaki mtupu na ameridhika. Iko kazi nzito na ya kudumu ya kupigania uhuru hasa katika mazingira ya watu wenye utamaduni kama huo wa mapepo. Kadhalika “Mwili umeumbwa na Mungu na ni makao au Hekalu la Mungu Roho Mtakatifu” siyo makao na kiti cha mapepo.


Leo tutaona patashika la namna yake tena la mara ya kwanza, pale Mganga mmoja atakapopambana uso kwa uso na mapepo hayo. Lengo lake ni kutuletea kwa ufupi mfumo au sera nzima ya mapinduzi anayotaka kuyapitisha kwa watu wote hapa duniani dhidi ya mapepo hayo. Yesu ndiye anayepigania uhuru wa koloni hilo lililomilikiwa na mapepo.


Tupo Kafarnaumu ambako Yesu aliweka makazi ya kudumu kwa miaka mitatu baada ya ubatizo wake. Aidha, ilikuwa ni siku ya Jumamosi (Sabato) siku ambayo wayahudi wanaabudu. Kwa kawaida ibada ya sinagogi ilikuwa ni kusoma Neno la Mungu kutoka mojawapo ya vitabu vitano vya Musa na toka moja ya sura za kitabu cha manabii, kishapo Rabi huitolea maelezo sura iliyosomwa kwa kunukuu kile kilichoishasomwa. Mathalani Rabi aliweza kusema: “katika sura hii Nabii alisema hivi au Musa aliandika vile,” na baada ya kumnukuu Rabi aliweza kuhitimisha hivi: “mwisho wa kunukuu.” Kwa hiyo watu waliridhika kwamba wamesikiliza Msahafu Mtakatifu na kujisikia wamesali.


Waamini aina hiyo hawawezi kamwe kubadilika, bali watabaki kuridhika tu kwamba wanashika Torati na Manabii. Hivi ndivyo wanavyofanya wahubiri wetu wa dini au wanasiasa na serikali. Wanazungumza kiushabiki na hotuba zao hazihamasishi wasikilizaji ili waweze kuchukua hatua ya kujikomboa na kutumikia jamii kwa haki na upendo. Mapato yake uovu unaendelea kuwakalia watu kama mapepo machafu.


Yesu anaingia kwenye Sinagogi na baada ya kusoma Msahafu Mtukufu alitegemewa naye atoe maelezo kama Marabi wote walivyokuwa wanafanya. Kinyume chake, Yesu anaanza kufundisha kwa mamlaka kama vile angekuwa mtunzi wa Msahafu aliosoma. “Mmesikia imesomwa hivi lakini mimi ninasema hivi,” au “Leo Maandiko haya yametimilika machoni penu.” Mtindo huu wa kuhubiri uliwaacha watu midomo wazi: “Wakashangaa mno kwa mafundisho yake; kwa maana alikuwa akiwafundisha kama mtu mwenye amri, wala si kama waandishi.” Namna hii ya kuongea ndiyo iliyowachokoza na kuwahamasisha watu kufanya mapinduzi na mabadiliko licha ya kushangaa. Mahubiri ya Yesu yaliwakurupusha mapepo yaliyomkalia mtu mmoja aliyekuwa kwenye Sinagogi akijidai kusali hadi yakaanza kupandisha.


Kizungumkuti unachoweza kuona hapa ni kwamba kwa miaka yote mapepo hayo yalikuwa yanahudhuria ibada katika Sinagogi ile pamoja na waumini wengine kama kawaida na kwa utulivu, labda pengine kwa sababu yalishajipatia kiti cha uvivu na kustarehe katika mtu huyu. Kwa mantiki hiyo yawezekana hata leo katika nyumba zetu za ibada kunaweza kukawa na watu wenye mapepo. Licha ya matendo yote ya ibada takatifu yanayoweza kufanyika humo Kanisani ikiwa ni pamoja na kusali, moshi wa ubani, mishumaa, maji ya baraka, ibada ya Rozari takatifu na ya Njia ya Msalaba pamoja na mahubiri ya mapadre, matendo hayo hayawagusi chochote, wao wanaendelea kupeta tu na pengine wanaona kuwa hiyo ndicho chakula hasa ubani na mishumaa iliyowashwa.


Kumbe leo tunaona maneno ya Yesu ndiyo yanawachefua nyongo pepo hao, wanang’aka na kugumia kama tunavyosikia: “Na mara moja palikuwapo ndani ya Sinagogi lao mtu mwenye pepo mchafu; akagumia kwa sauti. Umekuja kutuangamiza? Nakutambua u nani, Mtakatifu wa Mungu.” Maneno hayo!

Yesu anafaulu kuyatoa mapepo kwa tamko moja tu fupi: “Fumba kinywa umtoke.” Kumbe, kizungumkuti kingine unachoweza kukishuhudia kwa wanaotoa mapepo kwa kutumia jina la Yesu, wanavyohaha. Utawasikia wanavyogumia: “Kwa jina la Yesu nakuamrisha wewe pepo wa ulevi, pepo wa uwongo, umtoke mtu huyu.” Wanaorodhesha mapepo wote lakini wanaogopa kumkemea na kumtoa “pepo wa homa ya kutamani fedha, pepo wa homa ya madaraka, pepo wa kutamani sifa, pepo wa rushwa, pepo wa uasherati” kwa sababu hata mtoaji mwenyewe amepagawa na kukaliwa nao, hivi wanachofanya ni kuyahimiza mapepo hayo yazidi kumkalia mtu huyu. Kumbe Yesu hana pepo hata mmoja bali amepagawa na upendo wa Mungu Baba yake na anafaulu kuyafukuza mapepo kwa Neno fupi tu.


Mwinjili anataka kuonesha kwamba Neno la Yesu linatosha kumgeuza mtu anayeishi kinyama, aweze kuishi kiutu. Neno la Yesu limeyachokonoa mapepo wachafu waliomkalia mtu huyu hadi wanajiumbua wenyewe na kuweweseka: “Umefika ili kutuangamiza.” Kwa maneno hayo yaonekana pia kwamba katika ulimwengu wa mapepo kuna nguvu chafu za aina nyingi ndiyo maana wanaongea katika uwingi na nguvu hizo zinagongana na nguvu za dola ya Mungu.


Neno la Yesu ni la mapinduzi ya kweli, linachokoza, linakereketa, linaleta pendekezo jipya linalokudai kuchukua hatua mara moja. Watu wanashangaa siyo kutokana na muujiza, bali kutokana na maneno yake yanayomfukuza mtu huyu wa kale hadi wanasema: “anaamrisha hata pepo wachafu na wanakubali.” Kwa hiyo alama kwamba Yesu ameanza mapinduzi ni tendo lile la kumweka mtu huru toka tabia za kinyama na kishetani, nguvu zilizomkalia kama kiti.


Swali la mshangao “Ni nani huyo? Ni elimu mpya!” laweza pia kuwa swali kwetu la kulijibu, yaani kutoa uamuzi wa kumwaminia na kumfuata Yesu. Tunao bado mwaka mzima kuanzia sasa ambapo Yesu ataendelea kujiweka dhahiri jinsi alivyo na kututaka kufanya mapinduzi. Neno lake tu ndilo litakalotufanya turudishiwe uhuru wa utu wetu na nchi yetu! “Mbingu ni mbingu za Bwana, bali nchi amewapa wanadamu.” Kadhalika, “Mwili wako ni makao ya Roho Mtakatifu na siyo kiti cha mapepo.”

Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.