Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya IV ya Kipindi cha Mwaka wa B wa Kanisa
Mpendwa msikilizaji wa Neno, tukiwa pamoja tokea Radio Vatican, tunatafakari Neno
la Mungu Dominika ya 4 ya mwaka B wa Kanisa. Mama Kanisa atualika kusadiki kina kuwa
Bwana tuliyemtarajia, yu pamoja nasi na hivi kumfuata ndio wito wetu, ndio mwaliko
wa Kikristo.
Mwandishi
wa kitabu cha Kumbukumbu la Torati ambamo tunapata somo la kwanza anatualika kutambua
kuwa Mungu haachi kutimiza ahadi yake ya kale kwamba atamtuma Nabii atakayetangaza
hukumu zake kwa haki, atakayesema yale ya Bwana na kama atasema kinyume atakufa. Manabii
wengi walitangaza ujumbe wa Mungu lakini hasa katika zama zetu Mungu anasema nasi
kwa njia ya Masiha kama ambavyo Wayahudi walielewa ujumbe huo wa Neno la Mungu.
Masiha
yaani mkombozi ametufundisha yote na kutujalia Ubatizo na sakramenti nyingine. Kwa
njia hiyo kama wana wa Pentekoste tunaalikwa kutangaza yaliyo ya Mungu na kama ni
kinyume basi tutapotea katika njia zetu.
Mtume Paulo anapowaandikia Wakorinto
katika barua yake ya I sura ya saba, anaweka wazi miito mbalimbali katika Kanisa na
anataka kila mmoja afahamu kwa uhuru kamili, wajibu wake mbele ya wito huo katika
kutekeleza mapenzi ya Mungu. Wito wa ndoa ni wito mtakatifu ambao wamweka mtu katika
wajibu wa familia yaani kuhudumu familia na yote yahusuyo maisha ya ndoa.
Kwa
jinsi hiyo, Mtume Paulo anaona wajibu huo usipotendwa kwa unyenyekevu na hekima waweza
kumfanya mwanafamilia azame huko na kusahau wito wake wa kushughulikia masuala ya
uinjilishaji. Suala muhimu ni kuwa makini kutambua kuwa ndoa ni kwa ajili ya huduma
ya familia, Kanisa na Mungu mpaji.
Anatafakari juu ya wito wa upadre na maisha
ya kitawa akisema kwa wito huu mmoja aweza katika umakini wake kushughulikia zaidi
maisha ya missioni yaani kupeleka habari njema kwa mataifa. Awaalika wenye wito huu
kuona kuwa wanawajibika zaidi kufungua mioyo yao kwa Mungu kwa ajili ya wokovu wa
watu na wao wenyewe. Wakumbuke useja unatoa zaidi nafasi ya uwajibikaji katika shamba
la mizabibu na hivi madai kwao ni makubwa zaidi kuliko wengine.
Mpendwa unayenisikiliza
yafaa kukumbuka jambo moja, ikiwa mmoja atakuwa na mashaka upi ni wito mzuri au wa
juu! Toka ndoa twampata Padre na mtawa na hivi Kristu ameweka Sakramenti zote katika
uwiano mkamilifu akitakatifuza maisha ya watu kadri ya wito wa kila mmoja, yaani kadri
ya karama na vipaji alivyomjalia.
Mwinjili Marko anaweka mbele yetu yule Nabii
tuliyehaidiwa katika somo la kwanza atakayetangaza kazi ya Bwana. Bwana yuko katika
utume na anawaponya wagonjwa, si kwa nguvu ya mazingaombwe bali kwa nguvu ya mkono
wa Mungu. Anatangaza vita kinyume na pepo ambapo kwa kawaida ni ile hali ya kutokuwa
na roho wa kweli na hivi wenye pepo wanakuwa bado hawajakutana na Bwana.
Anataka
wana wa Mungu wasibaki chini ya utawala wa shetani bali wawe huru katika yeye. Kwa
jinsi hiyo mara wakutanapo na Bwana lazima pepo wakimbie kwa sababu yupo aliye Mungu
mwenye nguvu, mwenye ufalme mabegani mwake. Bwana anatoa sauti kali “fumba kinywa
chako umtoke” hii yamaanisha ugomvi uliopo katika ya pepo wachafu na maisha safi ya
Kikristo.
Basi mpendwa mwana wa Mungu tekelezeni mausia ya Bwana wakati wote
ili kukaa katika wito wako kwa furaha na matumaini ukikumbuka kuwajibika kadiri ya
wito huo katika kutenda yaliyo ya Mungu. Tumsifu Yesu Kristo.
Tafakari hii
imeletwa kwako na Pd. Richard Tiganya C.PP.S