Mpendwa msikilizaji wa kipindi chetu cha Kanisa la Nyumbani, Tumsifu Yesu Kristo!
Karibu kwa mara nyingine tena katika Kipindi chetu cha Kanisa la Nyumbani, tuendelee
kuchota na kuneemeka kutoka katika Hazina ya mafundisho ya Mtaguso Mkuu wa II wa Vatican.
00:12:44:38
Kwa wakati
huu, kukukumbusha mpendwa msikilizaji, tunapitia hati zote za mtaguso wa pili wa Vatikani,
moja baada ya nyingine. Lengo letu: tunataka Mafundisho ya Mama Kanisa kwa njia ya
Mtaguso wa II wa Vatican, yajulikane kwetu sote, ili maisha yetu ya imani, ya kiutume
na ya kijamii kwa ujumla, viwe na mkong’osio unaokubalika.
Leo tunaitupia jicho
hati ile inayohusu malezi ya mwanadamu katika ujumla wake. Hati hii ambayo ni Tamko
kati ya matamko matatu ya mababa wa Mtaguso Mkuu wa II wa Vaticani, kwa lugha ya
Kilatini inajulikana kwa jina la Gravissimum Educationis, ikiwa na maana, Uzito wa
Malezi. Mwangwi wa jumla tunaoupata katika hati hii ni kwamba Jamii nzima ya mwanadamu
inahusika sawia katika suala la malezi.
Lengo la hati hii ni kumwalika zaidi
mwanadamu kuongeza juhudi katika kuelewa umuhimu wa malezi kwa watoto, kwa vijana
na watu wazima pia, ili kuweza kuwaunda watu kiroho na kimwili, wanaoweza kuyamudu
malimwengu na kuyaratibisha sawia mahusiano yao kijamii. Sote tunaalikwa sana kutekeleza
mipango ya malezi kwa mbinu sahihi zenye kuleta mafanikio mema, kwa ajili ya sasa
na kesho iliyo bora zaidi.
daima linataka kuchangia juhudi hizo kufuatana
na wake kwa watu wote, kwanza kabisa kama Mama na Mwalimu wa watu wote na kwa nyakati
zote, na pili, kama Sakramenti ya jumla ya ukombozi kwa ajili ya kumkomboa mwadadamu
kiroho na kimwili.
Gravissimum Educationis, inasisitiza ya kila mtu kupata
malezi ya kumfaa. Huu kwanza ni wajibu wa wazazi katika familia na wote wanaoshika
dhamana ya malezi katika maisha-jamii; zikiwemo taasisi za elimu kwa ngazi zote, kuhakikisha
kwamba jitihada makini zinakuwepo za kumlea mwanadamu, kimwili, kiroho, kiakili na
kiutashi, ili kumwandaa awe raia mwema na zawadi kwa jamii atakayoishi nayo mahali
popote.
Gravissimum Educationis, inasema kwa msisitizo mkubwa kwamba, wazazi
ndio walezi wakuu kwa watoto wao. Wasipoutimiza wajibu huo mkubwa, sio rahisi kwa
taasisi nyingine kurekebisha aina hiyo ya mtu anayefanana na samaki mkavu, ambaye
hakukunjwa akingali mbichi. Ndipo hapo, tunasema kwamba; kuwa na watoto tu haitoshi!
Suala la msingi, ni watoto wa aina gani. Kama wazazi na jamii nzima tunahitaji watoto
bora, basi, na tujifunge kibwebwe katika kuwalea vema.
Gravissimum Educationis,
inaalika msaada kwa Kanisa na jamii kwa ujumla kuzisaidia familia katika suala la
malezi ya watoto, na sio familia tu, bali kuchangia katika suala la malezi ya mwanadamu
kwa ngazi zote kiroho na kimwili. Na Kanisa linatekeleza wajibu huo kwa njia mbali
mbali zinazoonekana wazi, zikiwemo taasisi za elimu kwa viwango mbalimbali, warsha,
makongamano, mafundisho jamii ya Kanisa, Mafundisho Mbalimbali ya Kanisa yenye lengo
la kumkomboa mwanadamu, na pia kwa njia ya utendaji unaoonekana katika huduma za jamii.
Ni jukumu la kila mwamini na watu wote, kutumia fursa hizo zinazotolewa na Kanisa
katika kujiunda.
Ndani ya Gravissimum Educationis, Waalimu nao mashuleni wamepewa
rai ya kuipokea kazi ya ualimu kama wito, na sio tu kama kitafutia fedha. Mwalimu
wa ngazi yoyote ile, ana nafasi kubwa sana ya kujenga au kubomoa jamii. Mwalimu aliye
makini katika kufikiri, kusema na kutenda, naye pia atatoa watu makini wenye kufikiri
sawasawa, kusema kwa ufasaha na kutenda kwa ufanisi. Mwalimu mpigamiayo, mzembe na
msinziaji katika fikra, daima atatoa watu wazembe katika jamii, waliojaa uvivu na
kila aina ya uzembe kazini, ruhusa nyingi na malalamiko tele.
Mwalimu ni Kioo
cha jamii. Mwalimu anafundisha darasani na nje ya darasa pia. Daima mwalimu aunganishe
taaluma yake, uadilifu wake na maisha yake halisia katika jamii. Na hiyo ndio maana
ya wito. Wito una mmyambuliko unganifu. Na kwa njia hiyo, mwalimu darasani, hawi
tu ni msimulizi wa mambo ya vitabuni na ya zamani, bali ni mwalimu pia wa mtu-mkamilifu
kwa nyakati zote na mahali pote.
Hati hii, Gravissimum Educationis, maana
yake Uzito wa Malezi, inawalika wazazi nao kushirikiana na juhudi za waalimu pia
katika kuwalea watoto. Wazazi, wasiwatupie au kuwazilia waalimu watoto wao, na hasa
watoto wakorofi na watundu nyumbani. Hutokea mazingira fulani, wazazi huwapeleka watoto
shuleni kwa sababu ni wasumbufu na waharibifu nyumbani, na hivyo kuondoa kero nyumbani,
furushi la kero linapelekwa mbali sana katika shule ya bweni.
Na huko uzito
wote unaachwa mikononi mwa waalimu au walezi bila kuwapa ushirikiano. Huko ni kukwepa
wajibu na madhara yake ni kuzidi kuongeza ukuta wa mgawanyiko kati ya watoto na wazazi.
Pawepo na ushirikiano, Gravissimum Educationis, inaelekeza. Na hati hii, inaongeza
kusema, ni juu ya wazazi kuchagua kwa aina ya shule inayohakikisha watoto wao wanalelewa
katika misingi sahihi ya utu na uadilifu kiroho na kimwili.
Na pia hati hii
inasisitiza kwamba waamini wote wana haki ya kupata , hasa vijana wawapo mashuleni
na nje ya shule, kwani wao ndio hazina na nguvu kazi-hai ya Kanisa na la Kanisa
la leo na Kesho. Gravissimum Educations, inakaza kusema, Serikali haina haki ya kulazimisha
watu wote kupata malezi ya aina moja, bali inapaswa kusaidia shule za watu binafsi
na za kidini katika mchango wao kwa malezi ya watu.
Kwa jicho karimu la kichungaji,
tukiangaziwa na Gravissimum Educationis, yaani Uzito wa Malezi, tunapenda kuangalisha
kwamba, kikwepwe kishawishi cha nyakati zetu cha kubiasharisha elimu. Wapo watu binafsi
wanaoanzisha shule kwa sababu wana fedha na wanapenda kujipatia fedha zaidi. Au hawana
lengo la kutoa elimu sahihi, baliwana lengo la kupenyeza ajenda zao za siri. Hiyo
ni hatari kwa Kanisa na Taifa.
Na pia, kuna kishawishi cha fasheni kwa baadhi
ya wazazi na walezi, kupenda kupeleka watoto kwenye shule za gharama kubwa mno, bila
kujali wanapata huko elimu ya namna gani. Ila mzazi anajisikia tu fahari kwamba ‘watoto
wangu wanasoma shule za gharama, kuliko wote, tena mbali’. Hizo ni sifa na fahari
zisizo na mshikio. Fasheni hizo ni hatari nazo kwa makuzi ya watoto wetu kiroho na
kimwili. Tupeleke watoto shule, ambako tunauhakika watapata malezi bora ya kitaaluma,
kumaadili, kiroho na kijamii.
Hati yetu, Gravissimum Educationis yaani, Uzito
wa Malezi inatutakia sote uwajibikaji makini katika malezi ili tuunde kizazi cha sasa
kilicho bora na kuijenga vyema yamii ya kesho. Kesho iliyo njema, ipo mikononi mwako
na mwangu!
Kutoka katika Studio za Radio Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin
Mkorwe, OSB.