Tofauti si tija! Jengeni madaraja ya watu kukutana!
Kardinali Antonio Maria Veglio', Rais wa Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji
kwa wahamiaji na wakimbizi katika maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani
kwa Mwaka 2015 inayoadhimishwa na Mama Kanisa, Jumapili, tarehe 18 Januari 2015 anasema,
ushirikishwaji wa watu katika jamii ni changamoto endelevu inayopaswa kufanyiwa kazi
na Jumuiya ya Kimataifa kwa kujikita katika ushirikiano.
Tofauti kati ya watu
ndani ya jamii zinapaswa kuwa ni daraja la watu kukutana ili kuendeleza majadiliano
yaanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu. Ikumbukwe kwamba, maeneo ya kazi
na shule ni sehemu murua kabisa zinazowakutanisha watu mbali mbali changamoto kubwa
ni watu kufahamiana, kushirikiana na kusaidiana katika hija ya maisha ya kila siku,
kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa utandawazi unaojali utu na heshima ya binadamu.
Kardinali
Antonio Veglio' anasema, sera na mikakati inayoamriwa na Jumuiya ya Kimataifa haina
budi kuepuka tabia ya ubaguzi na kutowatambua watu katika utu na heshima yao, mambo
amabayo wakati mwingi yamekuwa ni sababu ya chuki na kinzani zisizokuwa na mashiko.
Watu wengi wanahama au kukimbia kutoka katika nchi zao ili kutafuta maisha bora zaidi
na fursa za ajira. Lakini kwa bahati mbaya, sera nyingi zimekuwa zikiamsha hasira,
chuki, vizuizi na hali ya watu kutothaminiana, mambo ambayo ni hatari kwa amani, utulivu
na mfungamano wa kijamii.
Maeneo yaliyoko pembezoni mwa miji mikuu duniani,
yanaonekana kusahauliwa na wanasiasa katika sera na mikakati yao; mambo ambayo yanachangiwa
pia na athari za myumbo wa uchumi kimataifa pamoja na kumong'onyoka kwa tunu msingi
za maisha ya ndoa na familia; matokeo yake, maeneo haya yamekuwa ni chanzo cha chuki,
kinzani na ubaguzi dhidi ya wahamiaji na wageni.
Baba Mtakatifu Francisko katika
ujumbe wake katika Maadhimisho ya Siku ya Wahamiaji na Wakimbizi Duniani kwa Mwaka
2015 anasema Kanisa halina mipaka kwani ni Mama wa wote! Hii ni changamoto ya kuheshimu
na kuthamini utu wa binadamu na haki zake msingi. Tofauti za kidini na kiimani kisiwe
ni kisingizio cha vita na kinzani za kijamii zisizokuwa na mashiko. Watu wajifunze
na kudumisha utamaduni wa majadiliano, kwa kuheshimiana, katika ukweli na uwazi, mambo
msingi yanayotiliwa mkazo na Baba Mtakatifu Francisko.
Dhana ya uhamiaji imekuwa
ni chanzo cha majanga na vifo kwa watu wengi anasema Kardinali Antonio Veglio'. Katika
miaka ya hivi karibuni, kumekuwepo na udhaifu mkubwa katika kulinda na kudumisha haki
msingi za binadamu kwa kisingizio cha usalama wa taifa. Kuna wahamiaji wengi wanaodhulumiwa
na kunyonywa; kundi kubwa la watu linalotumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu
na utumwa mamboleo! Haya ni mambo yanayopaswa kufanyiwa kazi mintarafu Sheria na Protokali
za Kimataifa.
Kila mtu ana thamani mbele ya Mungu na jamii, changamoto ya kujenga
na kudumisha mshikamano wa upendo na udugu; kila mtu akipewa haki zake msingi; ili
kujenga na kuendeleza mafao ya wengi ndani ya jamii. Inasikitisha kuona kwamba, kuna
baadhi ya wafanyakazi Serikali na katika Mashirika ya Misaada Kimataifa wanaojitajirisha
kutokana na magumu ya wakimbizi na wahamiaji.
Kardinali Veglio' anasema kuna
haja ya kuwa na mwelekeo mpya unaothamini na kujali wahamiaji na wakimbizi kuwa ni
sehemu ya rasilimali watu, inayoweza kuchangia katika ustawi na maendeleo na nchi
na kwamba, rasilimali hii si tishio kwa usalama wa taifa.
Vita inayoendelea
Syria, Iraq na huko Mashariki ya Kati katika ujumla wake, imepelekea uwepo wa wimbi
kubwa la wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi na msaada kutoka kwa Jumuiya ya
Kimataifa. Ni maeneo yanayopaswa kusaidiwa ili amani, usalama na utulivu viweze kurejea
tena. Watu wanaotafuta hifadhi, wahakikishiwe usalama wa maisha yao; tabia ya kufumbia
macho mahangaiko ya watu ni hatari sana!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.