2015-01-12 11:54:57

Hotuba ya Baba Mtakatifu kwa Mabalozi mjini Vatican!


Amani duniani, utandawazi usiojali utu na heshima ya binadamu; utumwa mamboleo, vita na kinzani sehemu mbali mbali za dunia; vitendo vya kigaidi na athari zake; vita Barani Afrika; vitendo vya ubakaji na unyanyasaji wa kijinsia; umuhimu wa kuwahudumia wagonjwa wa Ebola kwa kuthamini utu na heshima yao kama binadamu; wakimbizi na wahamiaji; kazi na familia; hija ya kitume Barani Asia; matunda ya amani na mahusiano ya kidiplomasia kati ya Marekani na Cuba pamoja na kutunza mazingira kwa kukataa kishawishi cha vita duniani!

Haya ni kati ya mambo muhimu ambayo Baba Mtakatifu Francisko ameyakazia wakati alipokutana na kuzungumza na Mabalozi pamoja na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican, Jumatatu asubuhi, tarehe 12 Januari 2015 kabla ya kuanza hija yake ya kitume Barani Asia. Itakumbukwa kwamba, Vatican ina uhusiano wa kidiplomasia na Nchi 180 duniani.

Baba Mtakatifu ameanza hotuba yake kwa kukazia amani ambayo kimsingi ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, inayodhihirishwa kwa Fumbo la Umwilisho, linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo. Simulizi la kuzaliwa kwa Mtoto Yesu linaloonesha ugumu wa mioyo ya wanadamu, hali ambayo bado inajitokeza hata leo hii, kwani watu wanashindwa kuangaliana na kupokeana kama ndugu, matokeo yake ni kuendeleza utandawazi usiojali unaopelekea kinzani, vita na kifo kama ilivyojionesha huko Paris, Ufaransa.

Hapa anasema Baba Mtakatifu, kunazaliwa ubinadamu ambao umesheheni majeraha kutokana na kuendelea kuwepo kwa kinzani na vita kama alivyofanya Mfalme Herode, kwa kuwauwa watoto wote mjini Bethlehemu. Baba Mtakatifu anasema, inasikitisha kuona kwamba, vitendo kama hivi vimetendeka hivi karibuni huko Pakistan.

Baba Mtakatifu anazungumzia pia kuhusu utumwa mamboleo unaojionesha katika mitindo, madaraka, uchu wa mali na fedha na udini; utumwa mamboleo unaoibuka kutoka katika moyo wa mwanadamu unaoelemewa na dhambi, kiasi cha kushindwa kuona na kutenda mema, ili kulinda na kudumisha amani. Zote hizi ni dalili za utamaduni wa utumwa mamboleo unaoendeleza kinzani kama vita ya dunia inayoendelea kusababisha majanga makubwa.

Baba Mtakatifu anazungumzia vita inayoendelea nchini Ucrain, ambayo kwa sasa imegeuka kuwa ni uwanja wa fujo. Hapa kuna haja ya kujenga utamaduni wa majadiliano ili kuondokana na uadui ambao umejengeka kati ya watu, kwa kuwahusisha wadau wakuu, ili kuanza mchakato wa majadiliano katika hali ya kuaminiana mintarafu sheria za kimataifa.

Baba Mtakatifu Francisko ametumia fursa hii ya kukutana na Mabalozi pamoja na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa kuonesha masikitiko yake kutokana na vita inayoendelea huko Mashariki ya Kati, Iraq na Syria na kwamba, Kanisa kamwe halitachoka kuombea amani, hata kama ule mkutano wa sala uliowashirikisha viongozi wakuu wa Serikali ya Israeli na Palestina uliofanyika mwaka 2014 mjini Vatican haujazaa matunda yanayokusudiwa, bado anapenda kuwaalika viongozi wakuu wa Israeli na Palestina kuishi katika misingi ya amani kwa kutambua itifaki ya mataifa mawili.

Baba Mtakatifu anasikitishwa mno na mateso ya watu huko Iraq na Syria kutokana na vita inayoendelea kiasi cha kuibua vitendo vya kigaidi vyenye mwelekeo wa misimamo mikali ya kidini; vitendo vinavyomkataa Mwenyezi Mungu na binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wake. Haya ni matokeo ya utamaduni usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu.

Vitendo vya kigaidi vimekuwa na madhara makubwa kwa Wakristo, makundi ya kikabila na baadhi ya dini katika Ukanda huu; mambo yanayohitaji jibu makini kutoka kwa Jumuiya ya Kimataifa. Kuna haja ya kusitisha vita, kujenga amani na utulivu; kuganga na kuponya madonda miongoni mwa watu walioathirika vibaya, ili kweli amani iweze kutawala tena na hivyo kuondokana na vita pamoja na madhulumu ya kidini.

Uwepo wa Wakristo huko Mashariki ya Kati ni sehemu ya vinasaba na utajiri wake. Ni wajibu wa viongozi wa kidini, kisiasa, kijamii na wasomi hasa kutoka katika dini ya Kiislam, kulaani vikali misimamo mikali ya kidini inayosababisha vita na madhulumu; mambo ambayo Baba Mtakatifu anasema, yanajionesha pia sehemu mbali mbali za dunia.

Baba Mtakatifu akizungumzia Bara la Afrika, anasema kwamba, kuna nchi kadhaa ambazo kwa sasa zinaendelea na vita kuanzia Nigeria ambako kuna mauaji ya kikatili ya watu wasiokuwa na hatia pamoja na utekaji nyara; biashara haramu ya binadamu kwa kuwafanya wavulana na wasichana kuwa kama biadhaa. Vita bado inaendelea huko Libya, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati hata watu wenye mapenzi mema wanaotaka kujenga misingi ya amani wanatishiwa maisha kutokana na uchoyo pamoja na ubinafsi.

Baba Mtakatifu anasema, hali si shwari sana huko Sudan, Pembe ya Afrika na DRC ambako kuna idadi kubwa ya watu wanaolazimika kuyakimbia makazi yao kutokana na vita. Baba Mtakatifu anawataka wahusika kujikita katika mchakato wa upatanisho, haki na amani kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu. Kuna baadhi ya watu wanatumia ubakaji kama silaha katika vita, jambo ambalo linadhalilisha utu na heshima ya wanawake: kiroho na kimwili; madonda ambayo haitakuwa rahisi kufutika katika maisha yao.

Baba Mtakatifu anaialika Jumuiya ya Kimataifa kuwahudumia kwa heshima na taadhima wagonjwa na waathirika wa Ebola huko Liberia, Sierra Leone na Guinea, kwani hadi sasa kuna zaidi ya watu elfu sita ambao wamepoteza maisha yao. Baba Mtakatifu anawapongeza na kuwashukuru wafanyakazi katika sekta ya afya, watawa na watu wanaojitolea kuwaganga na kuwatibu wagonjwa wa Ebola na kwamba, ni wajibu wa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba inatoa huduma makini kwa wagonjwa wa Ebola pamoja na kuanzisha mikakati ya pamoja, ili kuutokomeza ugonjwa wa Ebola kutoka katika uso wa dunia.

Baba Mtakatifu anasiikitika kusema kwamba, bado Bahari ya Mediterania inaendelea kuwa ni kaburi kubwa la wahamiaji na wakimbizi; wanaodhulumiwa na kunyanyaswa na wafanyabiashara wenye uchu wa fedha. Hata Amerika, bado kuna idadi kubwa ya watoto wakimbizi na wahamiaji, wanaohitaji tiba, uangalizi makini, ulinzi pamoja na usalama. Wote hawa wanakumbana na pazia la chuma kwa kukataliwa, changamoto ya kubadili mwelekeo ili kuwajali, kuwapokea na kuwasaidia pamoja na kuhakikisha kwamba, ufumbuzi wa kudumu kuhusu chanzo kikuu cha wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi linapatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Baba Mtakatifu anasema, hakuna umaskini mkubwa kama mtu kukosa fursa ya ajira, jambo linalodhalilisha utu na heshima ya binadamu, kiasi cha kumgeuza mtu kuwa kweli ni mtumwa. Ukosefu wa fursa za ajira miongoni mwa vijana na kazi za suluba kwa watoto ni mambo ambayo kimsingi ni kinyume cha utu wa binadamu, kwani yanatoa kipaumbele cha kwanza kwa fedha. Utamaduni wa ubinafsi umepelekea idadi ndogo ya watoto wanaozaliwa hali ambayo inachangia pia uwepo wa familia tenge; mambo yanayoathiri tunu msingi za maisha ya kifamilia na jamii katika ujumla wake.

Baba Mtakatifu akizungumzia Nchi ya Italia anasema, myumbo wa uchumi kimataifa umepelekea wananchi wengi kukosa imani kwa Serikali yao na matokeo yake kuna kinzani nyingi za kijamii zinazoendelea kuibuka; kiasi cha kuwafanya watu wengi kuishi katika mazingira magumu. Baba Mtakatifu anawaalika kwa namna ya pekee, viongozi wa Serikali ya Italia kuondokana na hali ya kukosa uhakika katika masuala kijamii, kisiasa na kiuchumi; mambo ambayo yanayoweza kuitumbukiza nchi katika kinzani badala ya kujielekeza katika mshikamano, amani na utulivu kwa kuendelea kuwa na matumaini kwa kesho iliyobora zaidi, hasa miongoni mwa vijana.

Baba Mtakatifu katika hotuba yake amegusia hija yake ya kitume Barani Asia ambako anatembelea Sri Lanka na Ufilippini, tukio ambalo ni ushuhuda wa Kanisa linaloguswa na kujali maisha ya wananchi wa Bara la Asia. Ni matumaini yake kwamba, Korea ya Kaskazini na Kusini, zitaweza tena kuanza mchakato wa majadiliano, kwa kutambua kwamba, hizi ni nchi pacha!

Baba Mtakatifu anasema, licha ya hali ngumu inayojionesha sehemu mbali mbali za dunia, lakini matunda ya amani yameanza kuonekana huko Albania ambako madonda ya chuki na uhasama yameanza kuponyeka na watu wa dini na madhehebu mbali mbali wanaishi kwa amani na utulivu. Haya ni matunda ya majadiliano yanayojikita katika imani kwa Mwenyezi Mungu na kwa ajili ya kutafuta mafao ya wengi na kwamba, vita ni matokeo ya uelewa potofu wa dini. Majadiliano ya kidini na kiekumene yanamlenga binadamu na maendeleo yake; haya ndiyo yanayoendelea huko Uturuki na Yordan na kwamba, anatumainia kuwa Lebanon itaweza kupata ufumbuzi wa kudumu wa matatizo na changamoto za kisiasa.

Baba Mtakatifu anapongeza mchakato wa majadiliano ya kidiplomasia kati ya Marekani na Cuba, ambayo ni kwa ajili ya mafao ya wananchi wa pande hizi mbili. Anaipongeza pia Serikali ya Marekani kwa kuamua kufunga Gereza kuu la Guantanamo. Anaipongeza pia Serikali ya Burkina Faso inayoendelea kujielekeza katika ushirikiano na maendeleo na maridhiano yaliyofikiwa nchini Ufilippini, ili kukata mzizi wa chuki na uhasama nchini humo. Anaendelea kuwatia shime wote wanaojitaabisha kwa ajili ya kutafuta amani nchini Colombia, maridhiano huko Venezuela na mapatano kati ya Iran na Nchi tano zinazotumia nguvu za kinyuklia kwa ajili ya matumizi ya amani.

Baba Mtakatifu anahitimisha hotuba yake kwa kukumbushia kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha kumbu kumbu ya miaka sabini tangu Umoja wa Mataifa ulipoanzishwa kutokana na majivu ya Vita kuu ya Pili ya Dunia na wakati huo, Mwenyeheri Paulo VI alisikika akikemea uwepo wa vita tena duniani. Baba Mtakatifu Francisko anaangalia kwa matumaini utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo baada ya mwaka 2015, kwa kutoa kipaumbele cha pekee katika masuala ya tabianchi, kwani hapa ni chimbuko la amani ya kweli, toba na wongofu wa ndani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.