2014-12-19 16:28:07

Michezo iwe ni chanzo cha udugu, urafiki, maridhiano, amani na utulivu!


Katika Kipindi cha Karne moja, Kamati ya Olimpic ya Italia, C.O.N.I, imeratibu, kusimamia na kuongoza shughuli za michezo nchini Italia kwa kukazia pia umuhimu wa michezo kijamii, kielimu na kitamaduni. Shughuli zote hizi zinatoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu katika makuzi yake; ulinzi wa utu na heshima yake pamoja na kuendeleza mchakato wa kuiwezesha dunia kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi pasi na vita wala kinzani; kwa kuwafunda vijana kuondokana na tabia ya ubaguzi, ili kukuza na kudmisha urafiki, mshikamano na uhalisia wa maisha!

Baba Mtakatifu Francisko ameyasema haya wakati alipokutana na wanamichezo na wajumbe wa Kamati ya Olipic ya Italia, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican mara baada ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kama kilele cha maadhimisho ya Jubilee ya miaka mia moja tangu Kamati hii ilipoanzishwa. Michezo daima imekuwa ni chanzo cha udugu na urafiki, maridhiano na amani kati ya watu wa mataifa, kwa kuheshimiana, kuvumiliana na kuridhiana hata katika tofauti zao.

Baba Mtakatifu anasema michezo ya Olimpic Kimataifa imekuwa ni tukio linalowakusanya watu kutoka mataifa, tamaduni, dini na tunu msingi za maisha zinazotofautiana, ili kuanza mchakato wa njia mpya unaovuka uvunjaji wa haki msingi za binadamu. Ni michezo inayolenga mbali zaidi, kwa kujikita katika ubora na nguvu, changamoto kubwa si tu kwa wanamichezo bali kwa kila mtu kuweza kupokea mateso na sadaka ili kufikia malengo makubwa zaidi katika maisha; kwa kukubali karama na mapungufu binafsi pamoja na kutafuta njia ya kuweza kukabiliana kikamilifu na kasoro hizi.

Baba Mtakatifu anaitaka Kamati ya Olimpic Italiakuendeleza mafunzo shuleni; kwa kuonesha mshikamano wa upendo na wafanyakazi; daima wakitoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; michezo iwe ni fursa ya kuwakumbatia watu wote pasi na ubaguzi, kwa kujikita katika maisha ya binadamu, ili kuonesha moyo wa majitoleo.

Kanisa litaendelea kuwasaidia wanamichezo kutekeleza dhamana yao katika maisha ya kiroho, kwani hata watakatifu wengi walitambua umuhimu wa michezo, ndiyo maana Mtakatifu Paulo anamwambia Timoteo kwamba, kwa maana kujizoeza kupata nguvu za mwili kwa faa kidogo, lakini utauwa hufaa kwa mambo yote; yaani unayo ahadi ya uzima wa sasa, na ya ule utakaokuwepo baadaye. Baba Mtakatifu anawatakia maandalizi mema, Mji wa Roma unapojiandaa kuwa ni Mwenyeji wa Michezo ya Olimpic kwa Mwaka 2024. Mwishoni, amewatakia wote Noeli Njema.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.