2014-12-19 07:59:53

Mchango wa Vatican katika ujenzi wa mahusiano ya kidiplomasia kati ya USA na Cuba!


Jumuiya ya Kimataifa inashangilia kuona ujasiri uliofanywa na Serikali ya Marekani na Cuba kwa kuanzisha tena uhusiano wa kidiplomasia baada ya pazia la chuma kuzitenganisha nchi hizi mbili kwa takribani miaka 53 ya vita baridi iliyosababisha mateso na mahangaiko makubwa kwa wananchi wengi wa Cuba.

Tukio hili la kihistoria ni sehemu ya mchakato wa kidiplomasia uliofanywa na Mababa Watakatifu kuanzia kwa Mtakatifu Yohane XXIII hadi kwa Papa Francisko, ambao kamwe hawakukata tamaa kuona Cuba ikiwa katika ramani ya Jumuiya ya Kimataifa.

Mababa Watakatifu wamekuwa ni wajenzi wa madaraja yanayowaunganisha watu badala ya kuendekeza kinzani na migogoro ambayo kwa sasa imepitwa na wakati. Kwa kipindi cha miaka 53, Vatican kwa kushirikiana na Kanisa Mahalia pamoja na Mabalozi wa Marekani na Cuba wameendelea kufanya kazi hii ya kidiplomasia kwa imani na matumaini, huku utu, heshima, haki msingi za binadamu na mafao ya wengi vikipewa msukumo wa pekee.

Kunako mwaka 1962 Marekani na Cuba zilitunishiana misuli kwa vitisho vya mashambulizi ya makombora, huo ukawa ni mwanzo wa vita baridi iliyochachushwa na kinzani, chuki na uhasama kati ya Serikali hizi mbili, lakini kwa namna ya pekee Cuba ambayo ilikuwa inaungwa mkono na Urussi, iliathirika vibaya. Mtakatifu Yohane XXIII tarehe 25 Oktoba 1962, akawataka Marais wa Marekani na Cuba kuachana na vitisho na hatimaye vita kwa kuchuchumilia majadiliano, ili kujenga na kudumisha amani duniani, vinginevyo, madhara ya vita yangekuwa ni makubwa duniani, kwani vita haina pazia!

Marais wa Marekani na Urussi wakasikiliza sauti ya Kinabii kutoka kwa Baba Mtakatifu Yohane XXIII na huo ukawa ni cheche za Waraka wake wa kichungaji, Amani Duniani, "Pacem in Terris" unaowataka wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano kati ya watu badala ya kuendekeza kinzani na vita.

Miaka thelathini na sita baadaye, Mtakatifu Yohane Paulo II akatia nanga nchini Cuba, hapo tarehe 21 Januari 1998, Rais Fidel Castro akampokea kwa heshima na taadhima, tukio ambalo lilisaidia kuimarisha mchakato wa majadiliano kati ya Cuba na Jumuiya ya Kimataifa. Papa Yohane Paulo II katika mahubiri na hotuba zake nchini Cuba alisema kwamba, Wananchi wa Cuba walikuwa na haki ya kushuhudia imani yao hadharani bila ya kuingiliwa na mfumo wowote ule wa kisiasa.

Cuba ilitakiwa kuwa ni sehemu ya Jumuiya ya Kimataifa kwa kufungamana na mataifa mengine badala ya kuendelea kutengwa, jambo ambalo liliwatendea sana wananchi wa Cuba. Papa Yohane Paulo II alizitaka Serikali za Marekani na Cuba kuanza mchakato mpya wa kidiplomasia, ili kumaliza mgogoro ambao ulikuwa umepitwa na wakati, kwani watu walikuwa wana matumaini mapya, katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo!

Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI alitembelea Cuba kunako mwaka 2011 akakutana na kuzungumza na Rais RaĆ¹l Castro wa Cuba pamoja na viongozi waandamizi wa Serikali ya Cuba. Kwa macho makavu kabisa, Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI alisema kwamba, vikwazo vya kiuchumi vilikuwa na madhara makubwa kwa familia na maskini zaidi nchini Cuba na kwamba, ilikuwa inahitaji kuoneshwa ushirikiano na mfungamano wa kimataifa, kwa kujikita katika msingi wa uhuru na udugu kati ya Marekani na Cuba.

Leo hii, historia inaonesha kwamba, diplomasia ya Vatican ni moto wa kuotea mbali, hata kama itachukua miaka mingi, lakini iko siku, matunda yataonekana!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.