Caritas Mbeya yapongezwa kwa kufanikisha utoaji wa huduma!
Mkurugenzi wa Idara ya Caritas na maendeleo Jimbo Katoliki la Mbeya, Tanzania, Edgar
Mangasila amewapongeza wafanyakazi wote wa Idara hiyo kwa kushirikiana kwa pamoja
katika kufanikisha adhma ya Idara hiyo katika utume kwa jamii kwa ari na kasi.
Akizungumza
katika kikao cha wafanyakazi wote kilichofanyika Ijumaa, tarehe 19 Desemba 2014 lengo
likiwa ni kufunga ofisi kwa ajili ya mapumziko ya siku kuu ya Noel ikiwemo nafasi
ya kujitathmini kwa mwaka mzima katika utume wa Idara hiyo, Mangasila amesema, wakati
tunaelekea kufunga mwaka ni vema kujitathmini na kujipanga upya mwaka ujao.
Mkurugenzi
huyo amesema, watumishi tunapaswa kujipongeza kwa kufikia malengo ya utume wa Caritas
katika jamii na kwamba pongezi hizo ziwaendee na wenzi wao ambao kwa namna moja ama
nyingine wamesaidia kufanikisha malengo hayo. "Hata hivyo niwasihi sana tujipange
upya kwa mwaka 2015 katika utume wetu...upande wa nidhamu nawashukuru mnafuata maadili
mema kadiri Mwenyezi Mungu anavyotuongoza katika maeneo yote katika makazi tunayoishi
na maeneo ya kazi,"amesema.
Ameongeza,"Sisi ni watumishi wa watu na sote tupo
kwa ajili ya watu na tuendelee kudumisha ushirikiano kama tulivyoonesha mwaka huu
na tujitume zaidi,ili jamii yenye wahitaji iendelee kunufaika zaidi."
Ni utamaduni
wa Idara ya Caritas Jimbo Katoliki la Mbeya kwa idhini ya Mhashamu Baba Askofu Evaristus
Marcus Chengula (IMC) wa Jimbo Katoliki la Mbeya watumishi kupumzika kwa ajili ya
kusherehekea Siku kuu ya NOeli na Mwaka Mpya ikiwemo nafasi ya kujitafakari na kujipanga
upya kwa ajili ya utume wa Kanisa katika jamii.
Hata hivyo Mkurugenzi Mangasila
amesema licha ya kupumzika watumishi wasijisahau katika utume wao wa kila siku katika
familia na Kanisa; utume ambao haupumziki moja kwa moja kwani pale wanapohitajika
wanapaswa kuwa wepesi na kuitikia wito mara moja kwa kutoa huduma hitajika haraka
iwezekanavyo.