2014-12-17 09:44:06

Usawa wa kinga ya jamii katika sekta ya elimu!


Serikali ya Tanzania inaendelea vema na mpango wake wa kutoa elimu ya msingi kwa watoto wote waliofikia umri wa kwenda shule nchini. Hayo yamesemwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dkt. Shukuru Kawambwa wakati akiwasilisha mada yake inayohusu “Namna Tanzania inavyoboresha Usawa wa Kinga ya Jamii katika sekta ya elimu” katika kongamano la kimataifa linaloendelea katika siku ya pili jijini Arusha kuhusu Kinga ya Jamii.


Dkt. Kawambwa alisema kuwa mpango huo unaanzia elimu ya awali, shule ya msingi na sekondari ambapo kila mtoto mwenye umri wa kwenda shule apate elimu ambayo ndiyo msingi wa kinga ya jamii nchini tofauti na awali ambapo elimu ya msingi ilikuwa kwa watoto wenye umri kuanzia miaka 7 hadi 14. Dkt. Kawambwa alisisitiza kuwa mpango huo wa kinga ya jamii nchini unaenda sanjari na Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) ambao Tanzania imeanza kuutekeleza mwezi Aprili, 2013 ambapo unatarajiwa kuhitimishwa 2017.


Ili kufikia malengo ya kuboresha mpango wa kinga ya jamii nchini, Dkt. Kawambwa aliwaambia wajumbe wa kongamano hilo kuwa mbinu zinazotumiwa na Tanzania katika kutekeleza mpango wa BRN na kuboresha kinga ya jamii ni pamoja na kuboresha vifaa vya kujifunza na kufundishia shuleni, kusimamamia mpango wa wanafunzi kujua kusoma, kuandika na kuhesabu na kuboresha ufaulu wa wanafunzi katika mitihani ya ndani na ya taifa.



Mbinu nyingine ni kuwapa motisha walimu, kutoa motisha kwa shule zilizofanya vizuri katika mitihani ya taifa kwa shule zote iwe ya msingi au sekondari na kuwawezesha walimu na wanafunzi kujua wajibu wao kwenye sekta ya elimu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa kwa ufanisi ili kuongeza nguvu kazi ya wataalam ambao ndio msingi wa kuboresha kinga ya jamii na hivyo kupunguza tatizo la umaskini nchini.


Aidha, Dkt. Kawambwa alisema kuwa viashiri ambavyo vinaonesha Tanzania inaendelea kupata mafanikio katika kuimarisha sekta ya elimu na kuimarisha kinga ya jamiina ni pamoja na kuongezeka ufaulu katika mitihani ya taifa ambapo mwa 2013 ufaulu kwa shule za msingi na sekondari ulikuwa zaidi ya asilimia 60, mwaka 2014 kwa asilimia zaidi ya 70 na inatarajiwa 2015 ufaulu huo utaongezeka kufikia asilimia 80.


Akijibu swali la Katibu Mkuu Wizara ya Kazi, Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na Huduma Ali N. Ismail kutoka Kenya aliyetaka kujua kwanini Tanzania bado inatumia mpango wa kupanga shule katika madaraja ambao unaweza kupunguza morali kwa baadhi za shule ambazo inaweza kuwa chanzo cha kupunguza uwezekano wa kutoboresha mpango wa Kinga ya jamii.


Dkt. Kwambwa alisema kuwa Serikali inasimamia mpango huo kwa kuwahusisha wanafunzi wote na shule zote bila kubagua na kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum, walimu wamepata mafunzo ambayo yanawawezesha walimu hao kusimamia wanafunzi wenye mahitaji maalum kulingana na hali zao na amesema Tanzania ipo tayari kujifunza kutoka Kenya namna wanavyofanikiwa kuacha na mpango wa kupanga shule katika madaraja.


Kwa upande wa wanafunzi wenye ulemavu wa ngozi, Waziri Kwawambwa alisema kuwa kwenye suala la mitihani wanafunzi hao wamepewa kipaumbele kwenye suala la muda ambapo wao huongezewa baada ya muda wa kawaida wa mtihani kuisha na mitihani yao imeandikwa kwa maandishi makubwa zaidi ili kuwasaidia kusoma vizuri zaidi.


Kongamano la kimataifa linalohusu Kinga ya Jamii linaloendelea jijini Arusha limeandaliwa na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Fedha, Idara ya Kuondoa Umaskini kwa kushirikiana na UNICEF, ILO, UNAIDS na EPRI ambapo washiriki wa kongamano hilo wanatoka katika nchi za Kenya, Uganda, Bangladesh, Afghanistan, Msumbiji, Lesotho, Malawi, Afika Kusini, Ghana, Ethiopia, Zambia, Sudani kusini na mwenyeji Tanzania.








All the contents on this site are copyrighted ©.