Tanzania yasaka soko la watalii kutoka katika Falme za Kiarabu!
Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda amesema Serikali ya Tanzania imeamua kutafuta
soko la utalii kutoka nchi za Ghuba na Mashariki ya Kati ili kuongeza idadi ya watalii
nchini na kukuza pato la Taifa kupitia sekta hiyo. Ametoa kauli hiyo Jumatano, Desemba
17, 2014 wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufungua Kongamano
la siku mbili la Utalii na Uwekezaji lilionza siku ya Jumatano kwenye hoteli ya Le
Meridien, jijini Dubai, Falme za Kiarabu.
“Tunao mkakati wa kukuza utalii
nchini lakini wengi wameskuwa wakitoka Ulaya na Marekani. Eneo ambalo tumeona tuwekeze
kwa nguvu kwa maana ya kuongeza idaidi ya watalii ni hili la nchi za ghuba na Mashariki
ya Kati,” alisema. Waziri Mkuu alisema kimahusiano Tanzania iko karibu na nchi hizi
za ghuba lakini pia wanao uwezo wa kifedha wa kuwekeza kwenye maeneo mbalimbali ya
utalii. “Amani ya nchi yetu ni kivutio kingine kikubwa cha uwekezaji, sisi tuko tayari
kuwasaidia wafike huko tunakotaka,” alisema.
Alitoa wito kwa makampuni yanayotaka
kuwekeza nchini yaangalie fursa zilizopo kwenye ujenzi wa hoteli za kawaida, hoteli
za mahema (tented camps) na hoteli zenye kutoa huduma za vyakula (special cuisine
restaurant). Hata hivyo, aliwataka wawekezaji watakaokuja wafanye juhudi ya kushirikiana
na Watanzania wazawa ili nao wajione ni sehemu ya uwekezaji huo.
Mapema, akifungua
mkutano huo, Waziri Mkuu alisema katika kipindi cha miaka mitano, Tanzania imeweza
kuongeza idaidi ya watalii kutoka 714,367 mwaka 2009 hadi kufikia watalii 1,095,884
kwa mwaka 2013. “Kiwango cha mapato ya watalii hao kiliongezeka kutoka dola za Marekani
bilioni 1.2 hadi kufikia dola za Marekani bilioni 1.8 katika kipindi hicho hicho cha
miaka mitano,” alisema na kuongeza kuwa sekta hiyo inaajiri watu zaidi ya 400,000
kuchangia asilimia 17 kwenye pato la Taifa.
Naye Waziri wa Maliasili na Utalii,
Bw. Lazaro Nyalandu akizungumza na washiriki wa kongamano hilo kabla ya kumkaribisha
Waziri Mkuu alisema Tanzania ni nchi ya pili duniani kwa kuhifadhi rasilmali zake
na kuzitumia kwa utalii. “Nchi inayoongoza duniani ni Brazil,”alisema. Akiainisha
fursa za uwekezaji zilizopo Tanzania, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Utalii
nchini (TTB), Bi. Devothe Mdachi alisema Tanzania ina fursa nyingi za uwekezaji kupitia
sekta ya utalii zikiwemo uendelezaji wa fukwe, michezo ya majini na utalii wa mikutano
(conference tourism).
“Kwenye kumbi za mikutano, Tanzania inahitaji kumbi kubwa
zenye uwezo wa kuchukua watu kati ya 5,000 na 10,000 na hasa kwenye miji mikubwa kama
Arusha, Dar es Salaam na Mwanza,” alisema.
Naye Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji
nchini (TIC), Bibi Julieth Kairuki aliwaeleza washiriki wa kongamano hilo kwamba utalii
una fursa kubwa ya uwekezaji kama ilivyo kwenye sekta nyingine za madini na uchimbaji
gesi. “Uwekezaji hivi sasa umepanuka, na soko la utalii nchini Tanzania ni fursa
kubwa sana ya kuwekeza. Tunawasihi watu wenye mitaji mikubwa waangalie fursa hiyo
na kuichangamkia kama njia mojawapo ya kuwekeza nchini Tanzania,” alisema.