2014-12-17 12:02:24

Jumuiya ya Kimataifa haiwezi kuvumilia kuona tena machafuko Sudan ya Kusini!


Bwana Ban Ki-Moon Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anasema, umepita mwaka mmoja tangu machafuko ya kisiasa yalipoibuka Sudan ya Kusini na kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao, mambo ambayo kamwe hayawezi kukubalika na Jumuiya ya Kimataifa, kwamba, makundi mawili yanayomuunga mkono Rais Salva Kiir na Rijek Machar yanaendelea kusababisha maafa kwa wananchi wa Sudan ya Kusini.

Takwimu ambazo bado hazijakanushwa na Serikali zinaonesha kwamba, zaidi ya watu hamsini elfu wamepoteza maisha katika vita ya wenyewe kwa wenyewe Sudan ya Kusini katika kipindi cha mwaka mmoja na kwamba, waathirika zaidi ni wale wanaoishi katika maeneo yenye utajiri mkubwa wa nishati ya mafuta. Mapambano haya yanapania pamoja na mambo mengine kushikilia maeneo nyeti ya kiuchumi kwa ajili ya mafao ya makundi ya watu wachache nchini Sudan.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anasikitika kusema kwamba, mwaka mmoja tu na nusu tangu Sudan ya Kusini ilipojipatia uhuru wake kwa kura ya maoni, viongozi wamesahau mahangaiko na mateso ya wananchi wao, kiasi cha kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mafao yao binafsi. Ni viongozi hao hao waliokuwa wanapigania uhuru ambao ungesimikwa katika umoja na mshikamano wa kitaifa, uvumilivu na utawala bora; lakini msingi yote hii imetupwa kando, watu wanachakazana kwa risasi.

Kuna umati mkubwa wa wananchi wa Sudan ya Kusini unaohitaji huduma za kibinadamu kutokana na kukimbia makazi yao na kwamba, baa la njaa linaendelea kuwanyanyasa wananchi wengi, hali inaweza kuwa mbaya zaidi kwa siku za usoni, ikiwa kama amani na utulivu havitaweza kupatikana mapema iwezekanavyo. Serikali inapaswa pia kudumisha utawala wa sheria badala ya mtindo wa sasa wa wananchi kujichukulia sheria mikononi mwao.

Tarehe 15 Desemba 2014, Wananchi wote wa Sudan ya Kusini wamesali kwa ajili ya kuombea tena amani na utulivu nchini mwao. Askofu mkuu Paolino Lukudu Loro katika mahubiri yake kwenye Kanisa kuu la Jimbo kuu la Juba, amewakumbusha viongozi kwamba, uongozi unapaswa kuwa ni huduma inayotekelezwa kwa unyenyekevu kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watu. Ni dhamana inayofanyiwa kazi kwa muda maalum na wala si kutawala daima kama ambavyo baadhi ya viongozi wanatamani iwe!







All the contents on this site are copyrighted ©.