Uchu wa mali na madaraka kisiwe ni chanzo cha majanga na kinzani!
Kardinali John Onaiyekan, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Abuja, Nigeria, ameiomba Serikali
ya Nigeria chini ya uongozi wa Rais Goodluck Jonathan kuhakikisha kwamba, uchaguzi
mkuu unaotarajiwa kufanyika nchini humo, unakuwa huru na wa haki bila kutumia nguvu
ya dolla kupita kiasi, jambo ambalo mara nyingi limekuwa ni sababu ya watu kutaka
kulipizana kisasi.
Ni wajibu wa kila Chama cha kisiasa nchini Nigeria kutekeleza
vyema wajibu wake kwa kuendesha kampeni zinazopania kujenga na kuimarisha umoja na
mshikamano wa kitaifa badala ya kuendekeza udini na ukabila, chanzo kikuu cha majanga
na maafa kwa wananchi wa Nigeria. Mchakato mzima wa upigaji kura, tangu wakati wa
kampeni, siku yenyewe ya kupiga, zoezi la kuhesabu kura na hatimaye kutangaza washindi,
hauna budi kusimamiwa vyema kwa kuzingatia misingi ya ukweli, uwazi na uwajibikaji.
Ikiwa kama wanasiasa watachakachua matokeo ya uchaguzi, kuna hatari kubwa
kwamba, wananchi wakaamua kuchukua sheria mikononi mwao ili kutafuta haki ilipotea!
Huu utakuwa ni mwanzo wa machafuko na umwagaji wa damu ya watu wasiokuwa na hatia.
Serikali kuu ihakikishe kwamba, uchaguzi unakuwa huru na wa haki, ili kweli demokrasia
iweze kuchukua mkondo wake.
Kardinali Onaiyekan anawataka wanasiasa kuachana
na siasa za chuki na kampeni za kinyongo kwa kutishia usalama na maisha ya watu, ikiwa
kama baadhi yao watashindwa kupata ridhaa ya kuongoza nchi, kwani asiyekubali kushindwa
huyo si mshindani.
Kwa wale watakaoshinda na kupewa ridhaa ya kuongoza nchi,
waoneshe shukrani kwa kutekeleza ahadi zao na wale watakaoshindwa, basi wajenge uvumilivu
kwa kujipanga vyema zaidi katika chaguzi nyingine zijazo. Umefika wakati kwa wananchi
wa Nigeria kuhakikisha kwamba, utawala wa sheria na demokrasia vinashika mkondo wake.
Uchu wa mali na madaraka ni chanzo cha majanga na maafa makubwa Barani Afrika.
Wanasiasa wanapaswa kutambua kwamba, cheo ni dhamana wanayopewa na wananchi ili kuchochea
mchakato wa maendeleo. Fedha isiwe ni kisingizio cha kuvunja misingi ya haki, amani,
ustawi na maendeleo ya watu.