2014-11-30 08:27:22

Watawa waamsheni walimwengu!


Kardinali Joao Braz de Avis, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, Jumamosi usiku tarehe 29 Novemba 2014, kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu lililoko mjini Roma, amezindua rasmi mwaka wa Watawa Duniani.

Baba Mtakatifu Francisko katika tukio hili amewatumia watawa wanaotekeleza dhamana na utume wao sehemu mbali mbali za dunia ujumbe wa heri na matashi mema katika Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Dunian, utakaofungwa rasmi hapo tarehe 2 Februari 2016, Kanisa litakapokuwa linaadhimisha Siku kuu ya Yesu kutolewa Hekaluni, sanjari na Siku ya Watawa Duniani.

Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa watawa anawataka kuuamsha ulimwengu, kwa kutambua na kuthamini zawadi kubwa ambayo watawa wamekirimiwa na Mwenyezi Mungu kwa njia ya wito na maisha ya kitawa. Anawataka kumpatia Yesu Kristo kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wao, kwani maisha ya kitawa yanajipambanua kwa kushikamana na Kristo pamoja na Kanisa lake. Watawa watumie fursa hii kuhakikisha kwamba wanasaidia kuleta mabadiliko katika maisha ya watu kwa njia ya huduma makini wanayoitoa kwa Yesu Kristo, Neno wa Mungu aliyefanyika mwili.

Baba Mtakatifu anawaambia kwamba, hii ni changamoto endelevu inayowataka watawa kujiachilia mikononi mwa Yesu mwenyewe ili aweze kuwagusa, kuwaongoza, huku wakiwa makini kusikiliza sauti yake pamoja na kuwasindikiza kwa njia ya neema yake. Lakini watawa wanaweza kupata msaada mkubwa kutoka katika Injili, kwa kuimwilisha katika maisha na utume wao kati ya watu, kwa moyo wa unyenyekevu na ukweli kwa kuachana na kishawishi kinachoweza kuwatumbukiza katika dhana ya kufikirika.

Baba Mtakatifu anasema, maisha na utume wa watawa hayana budi kujikita katika kuwaendea na kuwatafuta wale ambao wanasukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na hali ya maisha yao. Kwa kukutana na Kristo, watawa waweze kukutana pia na maskini na wote wanaohitaji msaada wao. Watawa wajifunge kibwebwe kwenda pembezoni mwa jamii, ili kuwapelekea watu mwanga wa Injili, ili waendelee kukesha pamoja na kutambua mazingira yao, ili kupata mang'muzi mapana zaidi, ili kuganga na kuponya madonda ya Yesu Kristo mteswa, yanayojionesha kati ya watu.

Baba Mtakatifu anawataka watawa kuona ukweli na changamoto wanazokabiliana nazo bila ya kupoteza ile furaha, ujasiri na majitoleo yanayosheheni matumaini. Katika utume huu, Bikira Maria, Mama wa Kanisa na Msimamizi wa Wamissionari atawaongoza kwa jicho lake la kimama.







All the contents on this site are copyrighted ©.