Barua ya Papa Francisko katika Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani 2014 - 2016
Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, uliotishwa na Baba Mtakatifu Francisko yanazinduliwa
rasmi katika maadhimisho ya Jumapili ya Kwanza ya Kipindi cha Majilio, tarehe 30 Novemba
2014 sanjari na Jubilee ya miaka 50 ya Waraka wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican,
Fumbo la Kanisa, "Lumen Gentium" inavyojulikana na wengi kama Mwanga wa Mataifa, hati
ambayo imefafanua kwa kina na mapana nafasi ya Watawa ndani ya Kanisa.
Baba Mtakatifu
Francisko katika maadhimisho haya amewaandikia Watawa Barua ya Kichungaji inaobainisha
Malengo ya Mwaka wa Watawa; Matarajio na Mwelekeo wa Mwaka wa Watawa utakaohitimishwa
hapo tarehe 2 Februari 2016, Siku kuu ya Kutolewa Yesu Hekaluni, sanjari na Siku ya
Watawa Duniani, kama ilivyoelekezwa na Mtakatifu Yohane Paulo II katika Waraka wake
wa kichungaji kuhusiana na Maisha ya Kitawa.
Katika lengo la kwanza, Baba Mtakatifu
anatawaka watawa kuthamini uzoefu watakaoupata katika maadhimisho ya Mwaka wa Watawa
Duniani, kwa kuangalia maisha yaliyopita kwa moyo wa shukrani. Mwaka wa Watawa Duniani,
iwe ni fursa kwa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume kuangalia kwa kina na mapana
historia na maendeleo ya Shirika, kwani simulizi la historia ya Mashirika haya ni
sehemu ya mchakato wa kutaka kupyaisha utambulisho wao ili kujenga na kuimarisha umoja
na mshikamano kati ya wanashirika, kwa kutambua na kuthamini asili yao.
Baba
Mtakatifu anawataka watawa kuchunguza dhamiri zao ili kuangalia kwa kina na mapana
jinsi ambavyo wamejitahidi kumwilisha karama ya Shirika lao katika nyakati mbali mbali
za kihistoria; wameonesha ugunduzi gani uliowasaidia kusonga mbele kwa imani na matumaini;
ni matatizo na vikwazo gani walivyokutana navyo na jinsi walivyojitahidi kuvipatia
ufumbuzi.
Hii ni nafasi ya kuangalia pale ambapo Shirika limepindisha karama
yake kama sehemu ya mapungufu ya kibinadamu au wakati mwingine kwa kutokumbuka mambo
msingi katika karama ya Shirika. Hapa anasema Baba Mtakatifu ni kuona jinsi ambavyo
Shirika limethubutu katika kipindi cha miaka 50 iliyopita tangu baada ya Maadhimisho
ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, ulioleta ari na mwamko mpya kutoka kwa Roho Mtakatifu
ndani ya Kanisa.
Lengo la pili anasema Baba Mtakatifu ni kuhakikisha kwamba
watawa wanaishi wakati huu kwa hamasa na moyo mkuu, kwa kutambua na kung'amua asili
ya maisha na utume wa Shirika. Kwa Waanzilishi, anasema Baba Mtakatifu, Injili imekuwa
kwao ni kanuni msingi na kwamba, Katiba za Mashirika yao ilikuwa ni sehemu ya mchakato
wa kumwilisha Injili katika utimilifu wake, huku Yesu Kristo akipewa kipaumbele cha
kwanza na kushikamana naye, hata kudiriki kusema pamoja na Mtakatifu Paulo "... kwangu
mimi kuishi ni Kristo..." Nadhiri zilimaanisha kuonesha upendo wao wa dhati kwa Kristo.
Hii
ndiyo hali inayopaswa kuwasukuma watawa kujiuliza wakati huu wa Maadhimisho ya Mwaka
wa Watawa, jinsi gani wanavyotekeleza mashauri ya Kiinjili katika maisha na utume
wao na ikiwa kama kweli nadhiri zimekuwa ni mwongozo na dira ya maisha ya kila siku
katika uchaguzi wa mambo ambayo wanapaswa kuyatekeleza. Yesu anawataka kutekeleza,
kumwilisha Neno lake pamoja na kusikia huruma yake, kwa kutambua kwamba, upendo hauna
mipaka, bali umeendelea kufungua njia ili kupeleka upepo wa Injili katika tamaduni
pamoja na medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu.
Mwaka wa Watawa Duniani
ni fursa ya kujiuliza maswali msingi ikiwa kama kweli watawa wamekuwa waaminifu kwa
utume waliokabidhiwa na Mama Kanisa, ikiwa kama wameutekeleza kwa moyo wa umoja hata
pale ambapo kuna utofauti na kinzani, kwani waanzilishi wa Mashirika haya waliguswa
kwa namna ya pekee na umoja uliooneshwa na Mitume walipokuwa wanamzunguka Yesu
Leo
hii katika ulimwengu mamboleo, kuna kinzani nyingi ambazo zinagumisha maisha ya pamoja
kati ya watu wenye tamaduni mbali mbali, kwa kuwanyanyasa wanyonge; kwa kukazia tofauti
ambazo si jambo la msingi sana; watawa wanachangamotishwa kwa namna ya pekee kuhakikisha
kwamba, wanajenga jumuiya ambayo ni mfano unaotambua utu na heshima ya kila mtu pamoja
na kushirikisha karama zao mbali mbali sanjari na kujenga mahusiano ya kidugu.
Lengo
la tatu, la Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani ni kukumbatia maisha yajayo kwa
matumaini. Matatizo na changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika maisha ya kitawa
na kazi za kitume zimepelekea kupungua kwa miito hasa kutokana na baadhi ya watu kuwa
na mawazo mepesi mepesi. Ni katika mawazo kama haya anasema Baba Mtakatifu Francisko,
watawa wanapaswa kujenga matumaini yao, ambayo kimsingi ni matunda ya imani kwa Bwana
wa historia anayerudia kusema "... Usiogope ... maana mimi nipo pamoja nawe". Haya
ni matumaini anasema Baba Mtakatifu ambayo hayakujengwa katika idadi wala kazi, bali
kwa yule ambaye wamemwekea matumaini yao kiasi kwamba, hakuna lisilowezekana na kwamba,
haya ni matumaini yasiyodanganya kamwe.
Baba Mtakatifu anawaalika watawa wasitumbukie
katika kishawishi cha idadi ya watawa au kazi wanazozifanya au kwa kujiaminisha katika
nguvu zao wenyewe. Watawa vijana wanahimizwa kwa namna ya pekee kuwa ni wadau wakuu
katika Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani kwa kuanzisha mchakato wa majadiliano
na watawa wazee ambao wamewatangulia katika utumishi. Kwa njia ya mshikamano wa kidugu
wanaweza kutajirishana uzoefu na mang'amuzi pamoja na kuwashirikisha mawazo ambayo
pengine tangu mwanzo hayakufahamika na wengi, ili kutoa mwelekeo na ari mpya, ili
kwa njia nyingine tena kuweza kumwilisha Injili, jibu makini linalokidhi mahitaji
ya ushuhuda na utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu.
Baba Mtakatifu Francisko
katika Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa, analialika Kanisa kuonesha furaha inayobubujika
kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kurutubishwa na udugu unaomwilishwa katika jumuiya kwa
watawa kujisadaka katika huduma ndani ya Kanisa, kwenye Familia, kwa Vijana, Wazee,
Maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Baba Mtakatifu anaonya kwamba,
jamii inayokumbatia utamaduni wa ufanisi, ubora na mafanikio yanayowatenga maskini
na wale wasiokuwa na mwelekeo, ionjeshwe ushuhuda kwa ya njia maisha na kweli kutoka
katika Maandiko Matakatifu... Maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu.
Baba
Mtakatifu anakumbusha kwamba, Kanisa haliwezi kukua kwa kuwaongoa watu, bali kwa kuonesha
mvuto wenye mguso na mashiko. Hivi ndivyo ilivyo pia kwa maisha ya kitawa ambayo kamwe
hayawezi kutegemea ufanisi pamoja na nguvu ya nyenzo zake. Thamani ya Kanisa inapata
msingi wake kwa kuishi Injili na kutoa ushuhuda wa imani tendaji.
Kanisa ni
chumvi na mwanga wa dunia linachangamotishwa kuonesha ile chachu ya uwepo wa Ufalme
wa Mungu kwanza kabisa, kwa njia ya ushuhuda unaojikita katika upendo wa kidugu, mshikamano
pamoja na kushirikishana, katika kushuhudia unabii, mwaliko kwa watawa kuamsha tena
ulimwengu. Nabii anasema Baba Mtakatifu anapata uwezo wa kupembua historia anamoishi
na kuipatia tafsiri sahihi.
Nabii ana uwezo kung'amua pamoja na kukemea dhambi
na maovu ya kijamii na ukosefu wa haki kwa sababu ni mtu huru anayewajibika moja kwa
moja mbele ya Mwenyezi Mungu na wala hana mpango na mambo mengine, isipokuwa Mwenyezi
Mungu peke yake. Nabii daima ni mtu anayejishikamanisha na maskini, wasiokuwa na sauti
kwani anatambua kwamba, Mwenyezi Mungu daima yuko upande wao.
Baba Mtakatifu
Francisko anawataka watawa kuondokana na dhana ya kuishi kwenye ombwe na badala yake
wawe na uwezo wa kujenga maeneo ambamo wanaweza kuishi mantiki ya zawadi ya Kiinjili,
yanayojikita kwa namna ya pekee katika udugu, kupokea utofauti sanjari na kuonjeshana
upendo. Watawa ni watu wanaotambulikana kuwa ni mabingwa wa umoja, changamoto na mwaliko
wa kuonesha tunu hii wakati wa Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa, ili kukuza udugu uliooneshwa
na Waanzilishi wa Mashirika ili uweze kukua na kuenea zaidi. Umoja ujioneshe katika
jumuiya husika, ndani ya Shirika ambamo mara nyingi kuna kinzani, maseng'enyo, wivu
usiokuwa na maendeleo, chuki na hasira.
Baba Mtakatifu anawaalika watawa kuonesha
ushuhuda wa kinabii katika Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa, kwa kutoka katika mazingira
ya Mashirika husika ili kuibua pamoja na Mashirika mengine, mbinu mkakati katika ngazi
ya Makanisa mahalia na lile la Kiulimwengu; kuhusu: malezi, uinjilishaji na huduma
za kijamii, kwa kujitambua katika ukweli pamoja na kugundua mahitaji mapya kwa watu
wa nyakati hizi bila kugubikwa na ugonjwa wa kwa Mashirika haya kujitafuta yenyewe.
Baba
Mtakatifu Francisko anasema, anapenda kuona utekelezaji halisi wa mikakati inayopania
kuwasaidia na kuwahudumia wakimbizi; uwepo wao wa karibu kwa maskini na wote wanaosukumizwa
pembezoni mwa jamii; kuonesha kipaji cha ugunduzi katika Katekesi, utangazaji wa Neno
la Mungu pamoja na maisha ya sala; kwa kufanya marekebisho katika miundo mbinu, kwa
kutumia majengo kwa ajili ya kutoa huduma kadiri ya mahitaji ya Uinjilishaji na huduma
ya mapendo, kwa kusoma alama za nyakati.
Baba Mtakatifu Francisko katika Barua
yake kwa Mwaka wa Watawa Duniani, anawaalika waamini walei wanaoshiriki katika karama
na utume wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, kujitahidi kuuishi Mwaka huu kama
kipindi cha neema, ili kutambua zawadi waliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu. Anawaalika
kuuadhimisha Mwaka wa Watawa kwa kushirikisha Familia nzima, ili kukua na kujibu kwa
pamoja wito wa Roho Mtakatifu kutoka katika jamii mamboleo.
Katika Maadhimisho
ya Mwaka wa Watawa, wakati watawa watakapokuwa wanakutanika kati yao, wajitahidi hata
wao kushiriki kikamilifu ili kuonesha zawadi hii kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ili kuonja
karama kutoka kwa Mashirika mengine na vyama vya kitume, ili kuweza kutajirishana
na kusaidiana kwa pamoja.
Kwa moyo wa unyenyekevu, Baba Mtakatifu Francisko
anawaalika watawa waliojiweka wakfu na washirika wa Mashirika tofauti na Makanisa
tofauti na Kanisa Katoliki kushirikishana umoja na udugu, ili majadiliano ya Kiekumene
katika maisha ya kitawa, yasaidie mchakato wa ujenzi wa umoja kati ya Makanisa pamoja
na kukoleza moyo wa kuishi kwa amani na utulivu Mashirika yenye tamaduni na mapokeo
mbali mbali.
Baba Mtakatifu anahitimisha Barua yake katika Maadhimisho ya Mwaka
wa Watawa Duniani kwa kuwaalika Maaskofu kuendeleza na kukuza karama mbali mbali katika
Makanisa yao: kwa kupokea na kukumbatia karama mpya na zile za zamani, kwa kuwasaidia,
kuwahamasisha na kuwaongoza, daima wakionesha ukaribu wao kwa njia ya upendo kwa wale
wanaoteseka na wanyonge; ili waweze kupata watawa wengine watakaosaidia kuendeleza
"Jahazi la Kristo". Maaskofu wawasaidie Watu wa Mungu kwa njia ya Mafundisho yao kuhusu
umuhimu wa Maisha ya Kitawa, ili utakatifu uweze kung'aa ndani ya Kanisa.
Imehaririwa
na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.