2014-11-27 12:16:51

Wananchi wanapenda kuona Ulaya inayojali utu na heshima ya binadamu!


Jumuiya ya Ulaya na Kanisa zinakabiliana na changamoto ambazo zinapaswa kushughulikiwa kwa njia ya ushirikiano na mfungamano wa pamoja baina ya taasisi hizi mbili, zinazolenga kumhudumia mtu mzima: kiroho na kimwili, kwa kuzingatia tunu msingi za maisha ya binadamu.

Tunu hizi ni pamoja na uvumilivu kati ya watu; haja ya kuheshimiana na kuthaminiana kwani wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; usawa na wala si usawasawa, kwani Mwenyezi Mungu amemuumba mwanaume na mwanamke, ili waweze kukamilishana katika hija ya maisha yao hapa duniani.

Mshikamano unaofumbatwa katika kanuni ya auni ni muhimu sana katika mikakati ya maendeleo endelevu yanayojikita katika msingi wa amani, ambao kwa sasa ni jina jipya la maendeleo. Bwana Martin Schulz, Rais wa Bunge la Ulaya anasema kwamba, Baba Mtakatifu amewachangamsha kuhakikisha kwamba, wanaibua mbinu mkakati mpya utakaowawezesha tena wananchi kuhamasika kuendelea kuunga mkono Jumuiya ya Ulaya ambayo kwa sasa inaonekana kuwa kama Kikongwe, kiasi cha kuwafanya baadhi ya wananchi wa Bara la Ulaya kutokuwa na imani na Taasisi hii tena.

Baba Mtakatifu katika hotuba yake amekazia tunu msingi za maisha ya Kikristo na kiutu, mambo ambayo yanapaswa kufanyiwa kazi katika maisha ya hadhara Barani Ulaya, changamoto kwa wananchi wote wa Bara la Ulaya. Baba Mtakatifu Francisko kwa mwono wa kichungaji amegusia hali ya upweke hasi inayoendelea kuwaandama wananchi wengi Barani Ulaya. Hii ni changamoto ya kweli inayopaswa kuzingatiwa na watu wote wenye mapenzi mema.

Bwana Martin Shulz anasema, Baba Mtakatifu amewakumbusha wote kwamba, wanahitaji uwepo endelevu wa Bara la Ulaya linalosimikwa katika tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu; kwa kuheshimu na kuzingatia utu wa binadamu; kwa kujenga na kudumisha usawa kati ya watu; kwa kuhakikisha kwamba, Ulaya inawajengea vijana matumaini ya kesho iliyo bora zaidi kwa kuwapatia fursa za ajira na ujira mzuri; kusimama kidete kulinda na kutetea demokrasia ambayo kwa sasa inakabiliwa na changamoto nyingi.

Hotuba ya Baba Mtakatifu Francisko mjini Strasbourg ni ushuhuda wa maisha na utume wake, changamoto na mwaliko wa kujifunga kibwebwe kupambana na baa la umaskini linaloendelea kuwaandama wananchi wengi wa Bara la Ulaya kutokana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa. Utu wa binadamu na kuheshimiana ni mambo msingi sana katika mchakato wa ujenzi wa Jumuiya ya Ulaya sanjari na kuendelea kumwilisha mawazo ya waasisi wa Jumuiya y Ulaya, kwa kuendelea pia kufanya marekebisho, ili kweli Jumuiya ya Ulaya ilete mguso na mvuto kwa watu wake.







All the contents on this site are copyrighted ©.