Papa ni mjumbe wa mshikamano wa upendo na udugu kati ya Makanisa!
Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox anasema, hija ya kiekumene ya
Baba Mtakatifu Francisko nchini Uturuki katika maadhimisho ya Siku kuu ya Mtakatifu
Andrea Mtume, inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 30 Novemba,
ni fursa makini ya kutangaza na kushuhudia kwa matendo upendo na mshikamano wa kidugu
miongoni mwa Wakristo.
Patriaki Bartolomeo akihojiwa na Jarida la “Famiglia
Cristiana” anasema, kwa miaka mingi Makanisa haya mawili yamekuwa yakituma wajumbe
katika maadhimisho ya Siku kuu ya Watakatifu Petro na Paulo mjini Vatican na ile ya
Mtakatifu Andrea inayofanyika mjini Costantinopoli, matukio ambayo yanaonesha kwa
kiasi kikubwa Makanisa haya yanapania kushirikiana na kushikamana kwa dhati, ili kushuhudia
umoja na udugu kwa Kristo na Kanisa lake.
Baba Mtakatifu Francisko anatembelea
Uturuki nchi ambayo haina dini rasmi, changamoto na mwaliko kwa waamini wa dini mbali
mbali kuendelea kushikamana na kusaidiana kama ndugu na kwamba, tofauti zao za kidini
na kiimani zisiwe ni mwanzo wa chuki na vita kama inavyotokea sehemu mbali mbali za
dunia. Baba Mtakatifu atajionea utajiri na kuonja ukarimu wa wananchi wa Uturuki atakapotembelea
mjini Ankara na Istanbul.
Ni hija fupi ya Kiekumene, lakini inalenga kuimarisha
ujumbe kwa watu kuishi kwa amani na udugu. Uturuki ina historia kubwa katika maisha
na utume wa Kanisa. Hapa ni mahali ambapo Mababa wa Mitaguso kadhaa ya Kanisa walikutana
na kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa katika Karne za mwanzo mwanzo kabisa. Ni haki kabisa
kwa Makanisa kutambua na kuthamini mchango uliotolewa na Kanisa la Kiorthodox katika
maisha na utume wa Kanisa, lakini pia hata katika historia ya binadamu.
Baba
Mtakatifu Francisko ni mtu wa kawaida, anayeonesha upendo na mshikamano kwa maskini
na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Anaheshimiwa na kuthaminiwa na Makanisa
ya Mashariki kwa kukazia kwamba, yeye ni Askofu wa Roma. Ni kiongozi anayelifahamu
Kanisa la Mashariki, ndiyo maana anaendelea kuwashangaza wengi kwa kuteuwa Makardinali
nane watakaomsaidia kufanya maamuzi makubwa katika maisha na utume wa Kanisa, kielelezo
cha mchakato wa Sinodi.
Baba Mtakatifu Francisko anataka kuliongoza Kanisa
kwa mfumo wa Kisinodi, dhana inayoweza kurahisisha majadiliano ya Kiekumene na Kitaalimungu
ambayo yanazidi kusonga mbele miongoni mwa Makanisa haya mawili. Mahusiano kati ya
viongozi wakuu wa Makanisa na kati ya waamini yameendelea kuimarika mwaka hadi mwaka,
ili kwa pamoja, waweze kuwatangazia watu wa kizazi hiki, Injili ya Furaha na Matumaini
yanayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake, kwa njia ya ushuhuda wa upendo na
mshikamano wa kidugu!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili
ya Radio Vatican.