2014-11-27 09:16:04

Ogopa vitimbwi vya maisha!


Askari kama alivyo mlonda ni mlinzi wa nchi na raia wake dhidi ya maadui wakati mlonda ni mlinzi dhidi ya wevi. Kila mmoja wetu kwa namna fulani ni askari mlinzi au mlonda wa yeye mwenyewe na wa mali yake, yaani ni mpiga doria. Leo tunaanza mwaka mpya wa liturjia. Katika mwaka huu tutatanguzana na mwinjili Marko.

Majilio humaanisha ujio wa mara a kwanza wa Bwana Yesu Kristo miaka elfu mbili iliyopita alipofika kuidhihirisha nafsi ya Mungu hapa duniani; na yahusu pia atakapokuja tena mara ya pili. Lugha iliyotumika katika Injili ya leo inamwelekea zaidi askari mlinzi au mlonda. Lugha hiyo ya kiaskari ni ya kiufunuo. Aidha, siyo mfano, bali ni fumbo (Allegoria). Yesu anafananisha vituko vya maisha vinavyoweza kumjili binadamu na kutoa tahadhari.

Katika fasuli ya leo, Yesu anakichukua kituko cha kutisha cha kuangamizwa kwa Hekalu la Yerusalemu kilichotokea mwaka wa sabini baada ya kufa kwake na kukilinganisha na giza totoro. Halafu anakilisha tena giza hilo lililoikumba Yerusalemu na giza lile linaloweza kutanda mioyoni mwa watu waliogubikwa na kihoro na kitisho cha maisha maovu. Yesu anatuvutia taswira kama hiyo kwa kutumia lugha ya askari mlinzi au yaani mlonda, akisema: “Angalieni, kesheni (pigeni doria), kwa kuwa hamjui wakati ule utakapokuwapo.”

Kwa hoja kwamba, mlonda au bawabu (mngoja mlango) yambidi awe macho sana (kukesha) anapopiga doria kwa sababu hajui ni wakati gani kutatokea kitu gani au atatokea nani. Utafsiri uliozoeleka wa maneno hayo unaisha, kwa sababu unamwelewa Bwana kuwa hakimu mkali atakayekuja kuhukumu vikali. Bwana huyo ni kinyume na tangazo la furaha kwa wote tunalolisikia katika Injili.

Kadhalika neno hili “wakati au muda” linahitaji maelezo. Katika lugha ya kigiriki yanatumika maneno mawili yanayomaanisha muda, wakati au kitambo, lakini maana ya muda huo ni tofauti. Mathalani, kuna neno kronos, linamaanisha muda wa saa ya ukutani au mkononi, mfano saa nne asubuhi au saa tano usiku. Kisha kuna neno kairos lenye maana pia ya muda lakini muda kama fursa au wakati mwafaka, muda wa kubahatika, nafasi nzuri. nk.

Katika fasuli hii ya Injili Yesu ametumia neno hili kairos lenye maana ya fursa. Anataka kusema “Angalieni kesheni, kwa kuwa hamjui fursa, au wakati mwafaka, ua bahati nzuri itakapokuja”, vinginevyo kuna hatari ya kupoteza fursa. Waswahili wangesema: “Changamkia maswala, “Bahati haiji mara mbili”. Angalieni sana msipoteze fursa ile ya kuwa na furaha kwani Yesu atafika na habari njema ya furaha kuu.

Kisha anasema, “ni kama mtu mwenye kusafiri, ameiacha nyumba yake, amewapa watumwa wake amri na kila mtu kazi yake, naye amemwamuru bawabu akeshe.”
Huyo Bwana mwenye nyumba aliyeondoka ni Yesu mwenyewe. Lakini Yesu hajaondoka, yuko nasi ingawaje haonekani kwa macho ya kawaida, bali kwa namna iliyo dhahiri zaidi kama anavyosema mwenyewe: “Mimi niko nanyi hadi mwisho wa dunia”.

Watumishi (watumwa) wanaoambiwa kukesha, ni watu wale waliojizatiti kufuata sera na fikra za Bwana wao, kama asemavyo Mama Maria “Mimi ni mtumishi wa Bwana nitendewe ulivyonena”. Ni wale wanaofuata mapenzi ya Mungu. Ni watumishi wale waliolinganisha miradi, na maisha yao na fikra za Mungu. Nyumba inayotamkwa hapa ni jumuia ya wanafunzi yaani waumini walioingia katika Ufalme wa Mungu ili kuyaishi mapendekezo ya Heri Nane alizozipendekeza na alizoziishi Yesu Kristu mwenyewe. Kazi zote wameaminishwa wanafunzi, au watumishi wanaoendeleza mradi wa kuendelea kuijenga hiyo nyumba mpya.

Mlonda au bawabu anayeagizwa kukesha ni dhamiri ya kila mmoja wetu, inayotakiwa kuangalia na kumtambua yule anayetaka kuingia katika maisha yetu. Wako watu wengi wanaotaka kuingia, wakitoa ahadi nyingi na nzuri, kama vile furaha, amani, haki, upendo, kwa hiyo mlonda (dhamiri) yakubidi uwe makini sana kupambanua kitu kinachofaa na kile kisichofaa, kwani kuna wengine watafika wakijionesha kuwa wema kumbe ni wabakaji, hawaleti uzima bali husababisha maangamizo yako. Kwa hiyo kesheni pigeni doria.

Wakati huo wa ujio wake, umegawanyika sehemu nne: Kuna jioni; halafu usiku wa manane; kisha awikapo jimbi; na kuna wakati wa asubuhi. Nyakati zote ni za usiku. Mgawanyiko namna hii wa muda ni wa ulimwengu wa kigiriki na wa kirumi. Kumbe Bwana atafika usiku wakati kuna giza nene, usiku huo ni wa kibiblia. Katika biblia usiku kwanza uliokuwa ule wa kabla ya kuumbwa ulimwengu. Bwana aliposema “na uwe mwanga”.

Usiku wa pili ni ule ambapo Mungu alimwita Abrahamu aliyekuwa tayari na miaka mia moja na Sara mkewe akiwa na miaka tisaini, na kumwambia: “Toka nje kwenye gizani na angalia nyota za angani. Uzao wako utakuwa wingi zaidi kupita nyota za mbinguni.” Usiku wa tatu ni ule walipokombolewa waisraeli toka utumwani kwa Farao huko Misri. Na usiku wa nne ni ule atakapofika Masiha na kuvunjavunja minyororo yote ya chuma, na kutazaliwa ulimwengu mpya wa Masiha.

Kwa hiyo usiku huo wa nne ndiyo hili giza letu. Giza hilo ndiyo dhambi, ukosefu wa haki, uovu na madhulumu, magonjwa, kifo nk. Yabidi kuwa makini sana na kuvumilia wakati tunausubiri mwanga huo. Kwa hiyo ujumbe tunaoletewa hapa siyo wa woga, bali ni wa furaha, kwani Masiha anafika kuleta mwanga na kulitokomeza giza hilo la ulimwengu. Ili kuweza kupokea mwanga huo na kuufaidi, yatubidi kwanza tutambue kwamba tunaishi katika giza la usiku, yaani giza la madhulumu, kukoseana haki, vita, udanganyifu, rushwa, uonevu, giza kwa wale wasiokuwa na uhakika wa maisha ya kesho, giza la maadili yaliyopotoka, mfumo wa upendo wa uwongo, nk.

Tunaweza pia kuzungumza juu ya giza lililotanda ndani ya Kanisa, kama vile makwazo mbalimbali, chuki kwa Wakleri na kwa watu wa dini, kuna giza ndani ya vijana wanaosusia imani yao. Bila kutambua kuwa tuko gizani hatuwezi kuthamini mwanga, kwani “aliyetota hajui kutota.” Katika giza hilo, tusikate tamaa bali tukeshe daima. Hapa ndipo unapokuja umuhimu wa bawabu, yaani dhamiri. Yabidi bawabu au dhamiri iwe macho daima ili kumtambua na kumpokea Masiha anayefika, na siyo kuwa na dhamiri inayomwachia aingie bora mtu anayejionesha kuwa ni masiha na kuahidi mambo.

Dhamiri budi iwe safi inayokesha, na isilewe na maadili ya ulimwengu huu. Ni rahisi sana kuvutwa na kile unachosikia na kuona katika luninga, katika magazeti hatimaye unachanganyikiwa na hatimaye huelewi kinachoendelea, hujui kitu gani ni cha kweli na kitu gani ni uwongo.

Umuhimu na mkazo wa fasuli ya leo upo kwenye dhamiri, na kwenye sala, hasa sala ile ya kuwasiliana daima na Bwana katika kutafakari Maandiko Matakatifu. Bwana anaingia katika kila usiku na giza linalomkumba binadamu, ili aweze kumtia mwanga wa matumaini na amani hasa pale binadamu anapokuwa katika giza la uchungu, giza la hasira, majuto, giza la kutaka kulipa kisasi, giza la upweke unapojisikia kuachwa na kila mtu na usiku wa kutoona maana ya maisha. Umruhusu Bwana aingie katika maisha yako ili akuangazie mwanga wa matumaini. Katika giza aina hiyo yabidi kusali sala ile iliyo mwisho wa kitabu cha ufunuo ‘Njoo Bwana Yesu.”

Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.