Ziara ya kikazi ya Baba Mtakatifu Francisko huko Strasbourg, Ufaransa, hapo tarehe
25 Novemba 2014 imeacha changamoto nyingi zinazopaswa kufanyiwa kazi na Jumuiya ya
Ulaya kwa kushirikiana na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Ulaya,
CCEE, ambalo liliwakilishwa na viongoni wake wakuu chini ya Kardinali Peter Erdò,
Rais wa Baraza.
Baba Mtakatifu anaitaka Jumuiya ya Ulaya kuwa ni kikolezo
cha matumaini mapya yanayojikita katika misingi ya haki, amani na mshikamano wa dhati
kati ya Watu wa Mataifa. Wajumbe wamepokea changamoto zilizotolewa na Baba Mtakatifu
kwa mikono miwili kwani ni ujumbe ambao umegusa sakafu za mioyo yao, ndio maana hawakusita
kushangilia, pale ambapo waliguswa kwa namna ya pekee kutoka katika undani wa maisha,
shughuli na mikakati yao!
Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Balani
Ulaya linasema katika tamko lake kwamba, Baba Mtakatifu amewataka viongozi wa Jumuiya
ya Ulaya kufikiri na kutenda kwa kuzingatia kanuni maadili zinazojikita katika historia
ya Bara la Ulaya kama ilivyoasisiwa na waanzilishi wake waliotaka Bala la Ulaya lijengeke
katika misingi ya ukweli, mshikamano, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi
wake.
Haya ni mambo ambayo yanapaswa kufanyiwa kazi, kwa kutambua kwamba,
Kanisa pia lina mchango wake mkubwa katika mchakato wa maendeleo endelevu hususan
katika kukuza na kudumisha Injili ya Uhai; tunu msingi za maisha ya ndoa na familia
pamoja na kukuza na kudumisha utu na heshima ya binadamu. Ni matumaini ya Shirikisho
la Mabaraza ya Maaskofu Barani Ulaya kwamba, changamoto zilizotolewa na Baba Mtakatifu
Francisko wakati wa hija yake ya kichungaji huko Strausbourg, Ufaransa zitafanyiwa
kazi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wa Ulaya.