Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya kwanza ya Kipindi cha Majilio, Mwaka Be wa
Kanisa
Mpendwa mwana wa Mungu unayetegea sikio Radio Vatican, ninakutakieni Dominika ya furaha
na mwanzo mzuri wa kipindi cha Majilio. Tunatafakari pamoja Neno la Mungu katika Dominika
ya kwanza ya majilio, ujumbe kutoka Neno la Mungu ukiwa ni ule unaonaokudai KUKAA
TAYARI KATIKA SALA KWA AJILI YA KUMSUBIRI MASIYA AJAYE KWA JINA LA BWANA.
Mpendwa, kwa
kawaida Majilio ni kipindi cha matayarisho kwa ajili ya kuzaliwa Masiha. Hata hivyo
Kanisa halitafakari tu kuzaliwa kwa Masiha na kuishia hapo bali pia hutafakari na
kuwatayarisha waamini kwa ajili ya ujio wa pili wa Bwana. Ndiyo kusema Dominika ya
kwanza hadi tarehe 16 Desemba, Mama Kanisa ametuwekea masomo ambayo hutuongoza katika
maandalizi ya ujio wa pili.
Kwa maana hiyo litrujia yatutaka kungoja kwa matumaini
yaliyojaa furaha na hamu kurudi kwake Yesu Kristu mara ya mwisho. Wote tunaalikwa
kuitengeneza njia ya Bwana mwaliko ambao Yohane Mbatizaji aliwapatia Waisraeli.
Sehemu
ya pili ya kipindi cha Majilio yaani kuanzia 17 Desemba hadi 25 Desemba yaani Sherehe
ya kuzaliwa Mkombozi, Liturujia yatutaka kutafakari, kujikusanya na kuweka mawazo
yetu katika kutayarisha sherehe hiyo ya Noeli. Kanisa linaimba daima Ewe mfalme, Ewe
EMANUELI UJE KUTUOKOA.
Katika kipindi cha majilio, Mama Kanisa akitumia mafundisho
ya Nabii Isaya atuhimiza kumtumaini Mungu na kuacha mambo ya kipagani, mwenendo mbaya
na hivi kumfuasa Kristo katika maisha ya utakatifu. Mafundisho haya kusema yatudai
kuongoka na kukaa tayari tukimsubiri Masiha. Kama Nabii Isaya alivyowatayarisha watu
wa kale kumtumaini Mungu ndivyo anavyotutayarisha kujiandaa kumpokea Bwana mioyoni
mwetu hivi leo.
Kama kielelezo cha matayarisho ya Noeli yaani ujio wa Bwana,
iko desturi ya kuwasha mishumaa minne, katika majuma manne kielelezo cha mwanga wa
Kristu na mishumaa hii huitwa mshumaa wa Nabii Isaya juma la kwanza, mshumaa wa Yohane
Mbatizaji, juma la pili. Wote twatambua nafasi ya Yohane Mbatizaji katika kuandaa
ujio wa Masiha, yeye ni mtangulizi mnyenyekevu ambaye anatualika kuitengeneza njia
ya Bwana kwa ujio wa pili. Anamtambulisha Masiha kwa watu na hivi kabla anawatayarisha
watu waongoke.
Katika juma la tatu tunawasha mshumaa wa Mtakatifu Yosefu.
Hatuwezi kuzungumza Masiha bila kumtaja Yosefu. Ni Baba mlishi wa Yesu Kristu ni mme
wa Bikira Maria. Ni Baba mnyenyekevu asiye na makuu na kwa namna hiyo basi, katika
unyenyekevu wake ametekeleza mpango wa Mungu kwa upendo na unyenyekevu.
Na
mwisho katika Dominika ya nne ya majilio, tunawasha mshumaa wa Mama Bikira Maria,
mama wa Mkombozi, Mama asiye na doa, mama anayetufundisha kujitoa kiaminifu pasipo
kujibakiza katika kutekeleza mapenzi ya Mungu na hivi anasema, “mimi ni mtumishi wa
Bwana nitendewe kama ulivyonena”.
Tunapofungua mwaka wa Kanisa (2014 - 2016)
kwa kipindi cha Majilio, tunayo furaha kuu pia, katika mwaka huu, Mama Kanisa anapofungua
Mwaka wa Watawa Duniani, maisha ya kujitoa bila ya kujibakiza mbele ya Mungu na jirani.
Katika mwaka wa Watawa Duniani, mwaliko kwanza kwa Watawa, ni kuwa tayari kuifanya
Injili ipenye katika maisha ya watu kwa njia ya unabii wao, wakijaribu kwa unabii
huo kujenga matumaini mapya.
Mama Kanisa anawaalika yakuwa uwepo wao uwe ni
njia ya kutangaza ufalme wa Mungu, ufalme ambao ni kwa ajili ya amani, mapendo, furaha,
imani na matumaini mapya tukikaribia mbingu mpya.
Mpendwa, jambo hili si tu
kwa ajili ya Watawa bali ni la Kanisa zima, kumbe, tunaalikwa nasi sote kuongozwa
na Injili ili kupeleka Neno la furaha na matumaini kwa watu. Huu ni wajibu wa kinabii,
wajibu ambao kama Manabii walivyotekeleza mwaliko wa Mungu na kupeleka habari hiyo
njema kwa watu, nasi tunaalikwa kuutekeleza mpango wa Mungu wa kupeleka furaha na
mapendo kwa mataifa.
Mpendwa mwana wa Mungu, katika somo la kwanza, wana wa
Israeli wako utumwani Babeli, wanahangaika na kuteseka na wanaona mateso yao yanatokana
na dhambi zao na hivi wanasali kwa kulalamika kwa nini Mungu amewaacha na hata wakaweza
kutenda dhambi ya kutokumcha yeye aliye Bwana! Wanajiuliza na kumwuliza Mungu je tutaokolewa?
Kutokana maswali haya wanafikia hitimisho na kusema mbele ya Mungu, hakika wewe u
Baba yetu sisi tu udongo nawe umfinyanzi, na sisi tu kazi ya mikono yako. Sala hii
yaonesha toba, yaonesha uongofu ambao Nabii Isaya anatualika tuutafute.
Katika
somo la II Mtume Paulo anamshukuru Mungu aliyewainua Wakorinto, akawapa utajiri wa
imani na mapendo na hivi wanaweza kukaa tayari kwa kutazamia kufunuliwa kwa Bwana
wetu Yesu Kristu. Huo ndio wito wa Majilio, kujiweka tayari kumsubiri Bwana atakayekuja.
Mwinjili
Matayo anaweka wazi mbele yetu, fundisho la kuwa macho tukikesha ili Bwana ajapo atukute
tu tayari. Anatumia mfano wa mtu mwenye nyumba yake, aliyesafiri na kuwaachia watumwa
wake nyumba na kila mtu na wajibu yake. Anatarajia akirudi hata muda usiojulikana
awakute watumwa hawa wakiwa macho wamefanya yote vema kama alivyowapangia. Kwako wewe
mwana wa Mungu umekabidhiwa talanta ambazo unaalikwa kuziweka katika uzalishaji ili
Bwana ajapo akukute unayo faida ndiyo kuwa macho na kukaa tayari. Kumbe kipindi cha
majilio ni kipindi cha kuungama, kupatana na waliotukosea na kujiweka safi daima kwa
virutubisho ndizo sakramenti na Neno la Mungu.
Ninakutakieni majilio njema
iliyojaa heri na ustawi wa upendo, msamaha na huruma kwa wote ukilenga katika ujio
wa Masiha. Tumsifu Yesu Kristo Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya,
C.PP.S.