Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi
maalum, linatangaza kwamba, tarehe 8 Februari 2015 itakuwa ni siku maalum ya kuhamasisha
uelewa juu ya biashara haramu ya binadamu; siku ambayo Mama Kanisa anaadhimisha Siku
kuu ya Mtakatifu Josephine Bakhita, kutoka Sudan aliyetekwa nyara na kupelekwa utumwani
na baadaye kuokolewa na Wasamaria wema waliomwezesha kukumbatia imani ya Kikristo,
leo hii ni mfano bora wa kuigwa.
Itakumbukwa kwamba, alitangazwa na Baba Mtakatifu
Yohane Paulo II kuwa Mtakatifu kunako mwaka 2000, Kanisa lilipokua linaadhimisha Jubilee
kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo.
Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa
wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum kwa kushirikiana na Shirikisho la Wakuu
wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, wataandaa Siku ya kupinga biashara haramu
ya binadamu na kwa mara ya kwanza itaadhimishwa kwenye majimbo mbali mbali hapo tarehe
8 Februari 2015.
Itakumbukwa kwamba, biashara haramu ya binadamu ni kati ya
mambo yanayodhalilisha utu na heshima ya binadamu katika karne ya ishirini na moja.
Umoja wa Mataifa unabainisha kwamba, kuna zaidi ya watu millioni ishirini na moja
ambao wametumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo. Hili ni
kundi linalotoka katika nchi maskini na kutokana na umaskini huu, watu wengi kwa kupewa
ahadi za uwongo wanajikuta wakiwa wametumbukizwa kwenye biasha haramu ya binadamu
na utumwa mamboleo.
Ni watu wanaochomolewa viungo vyao, ili kuuzwa kwenye
soko la biashara haramu ya viungo vya binadamu, linaloendelea kukua na kuongezeka
maradufu kila mwaka. Baadhi ya wasichana na watoto wanafanyishwa kazi za sulubu, kiasi
kwamba, wanajuta kwanini wamekimbia kutoka nyumbani kwao kwa tamaa ya kupata nafuu
ya maisha, lakini huko wanafanyishwa kazi kama Punda pasi na utu! Baadhi ya wasichana
na wanawake wanajikuta wakilazimika kuingia kwenye ndoa za shuruti hata pasipokuwa
na ridhaa yao.
Takwimu zinaonesha kwamba, kila mwaka zaidi ya watu millioni
2.5 wanatumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo, kati yao
asilimia 60% ni wanawake na watoto. Hii ni biashara inayotunisha mifuko ya watu ambao
dhamiri zao zimekufa, kwani inaingiza kwa mwaka kiasi cha dolla za Kimarekani billioni
32. Hii ni biashara ya tatu kimataifa inayopata faida kubwa sana, ikifuatiwa na biashara
haramu ya dawa za kulevya na biashara ya silaha duniani.
Kanisa limekuwa mstari
wa mbele kupambana na biashara haramu ya binadamu pamoja na kuwasaidia waathirika
wa biashara hii kwa hali na mali. Kanisa kwa kutumia Mashirika ya kitawa na kazi za
kitume, limeendelea kuwahabarisha na kuwahamasisha watu kufahamu njama zinazotumika
katika biashara hii haramu na madhara yake kwa utu na heshima ya binadamu. Baba Mtakatifu
Francisko, amelivalia njuga tatizo hili, kwani linakwenda kinyume kabisa cha utu na
heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.
Kuna haja kwa Jumuiya
ya Kimataifa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu,
utu na heshima ya binadamu, kwa wahanga wote wa biashara haramu ya binadamu. Wahusika
wanapaswa kutambuliwa na kukamatwa ili sheria iweze kuchukua mkondo wake, kwa kugeuza
watu kuwa kama bidhaa inayoweza kuuzwa na kununuliwa kutoka madukani na kusahau kwamba,
hawa ni binadamu, wana utu na heshima yao.
Siku ya kupambana na biashara haramu
ya binadamu ni muhimu sana, wakati huu Mama Kanisa anaposherehekea Mwaka wa Watawa,
kwani haya ndiyo “majembe” yaliyoko mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya biashara
haramu ya binadamu na utumwa mamboleo.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.