Kanisa liko tayari kuanzisha mchakato wa majadiliano ili kuboresha mahusiano kati
ya Serikali na Kanisa
Askofu mkuu Hubertus Matheus Maria Van Megen, Balozi wa Vatican nchini Eritrea, hivi
karibuni alianza utume wake kwa kuwasilisha hati zake za utambulisho kwa viongozi
wa Serikali ya Eritrea. Alipowasili nchini Eritrea, Askofu mkuu Van Megen amekaribishwa
na viongozi wa Serikali na Kanisa.
Hati zake za utambulisho zilipokelewa na
viongozi wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa nchini Eritrea. Viongozi
hawa wamejadili kuhusu uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Eritrea sanjari
na mchango wa Kanisa katika ustawi na maendeleo ya wananchi wa Eritrea katika ujumla
wao, hususan katika sekta ya elimu, afya na maendeleo ya mtu mzima: kiroho na kimwili.
Huu ndio Uinjilishaji wa kina unaofanywa na Mama Kanisa, Barani Afrika na sehemu mbali
mbali za dunia.
Rais Isaia Afwerki, amemkaribisha Askofu mkuu Van Megen nchini
Eritrea, kwa kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko, Vatican na Kanisa katika ujumla
wake kwa kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu; ustawi, maendeleo
na mafao ya wengi; mambo msingi yanayojikita katika amani, utulivu na maelewano kati
ya watu. Serikali ya Eritrea itaendelea kukuza na kudumisha utamaduni na mapokeo yake
pamoja na kutoa fursa kwa waamini wa dini mbali mbali kuweza kukiri na kushuhudia
imani yao katika hali ya usalama, kwa mafao ya wengi.
Askofu mkuu Hubertus
Matheus Maria van Megen kwa upande wake, amewashukuru wananchi wa Eritrea kwa kuonesha
upendo na mshikamano. Ametumia fursa hii, kuwasilisha salam na matashi mema kutoka
kwa Baba Mtakatifu Francisko, kwa kusema kwamba, Kanisa liko tayari kuanzisha mchakato
wa majadiliano, ili kuboresha uhusiano kati ya Serikali na Kanisa, kwa ajili ya ustawi
na maendeleo ya wengi.
Askofu mkuu Megen pamoja na Familia ya Mungu nchini
Eritrea waliweza kuunganisha kwa pamoja, ili kumshukuru Mungu kwa zawadi ya Mtakatifu
Daniel Comboni, mtume hodari kwa Kanisa Barani Afrika.