2014-11-26 07:52:35

Dawa ya mapigano kati ya wakulima na wafugaji inachemka!


Dr. Titus Mlengeya Kamani, Waziri wa mifugo na maendeleo ya uvuvi nchini Tanzania, hivi karibuni alipokuwa anazungumza na Watanzania wanaoishi nchini Italia, alifafanua kwa kina na mapana sababu zinazopelekea mapigano ya mara kwa mara kati ya wakulima na wafugaji nchini Tanzania. RealAudioMP3

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iemanza kutekeleza mikakati mbali mbali ili kudumisha misingi yahaki, amani na utulivu miongoni mwa jamii, kwa kutambua kwamba, wote wanategemeana, wanapaswa kuvumiliana, kuheshimiana na kuthaminiana kwa dhati, ili kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa!.

Sababu kubwa inayopelekea migogoro kati ya wafugaji na wakulima nchini Tanzania ni ongezeko kubwa la watu wanaohitaji eneo kubwa la kilimo na kulishia mifugo. Kutokana na maboresho ya maisha nchini Tanzania, idadi ya watu inaendelea kuongezeka maradufu, lakini eneo ni lile lile lililokuwepo hata kabla ya Tanzania kujipatia uhuru wake. Wafugaji wengi nchini Tanzania wameendelea kutumia ufugaji wa asili wa kuhamahama na mifugo yao, ili kutafuta malisho na maji, hali ambayo imekuwa wakati mwingine ni kero na sababu ya mapigano kati ya wakulima na wafugaji.

Ardhi nchini Tanzania ni mali ya Serikali na kutokana na mantiki hii, ardhi imekuwa inamilikuwa kwa ujumla, hali ambayo imesababisha wakati mwingine kinzani na migogoro ya ardhi.

Dr. Titus Mlengeya Kamani anasema, Serikali imeanza kutoa elimu kwa wafugai kuhusiana na upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya malisho pamoja na athari zinazoendelea kusabishwa na mabadiliko ya tabia nchi, ili kuzifahamu na kuzifanyia kazi. Serikali imetunga sheria ya mwaka 2010 ya malisho na rasimali ya chakula cha mifugo. Lengo ni kutambua maeneo ya ufugaji kisheria, ili yaweze kulindwa, kutunzwa na kuendelezwa kikamilifu.

Wafugaji wanaendelea kuhamasishwa kuelewa kwamba, mifugo yao kwa sasa inapaswa kuwa ni mazao, yanayoweza kuboreshwa kwa kupata mbegu bora zaidi; mazao yanayoweza kuvunjwa na kuongezewa thamani, ili kuongeza pato la wafugaji na hatimaye wafugaji kuweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa pato ghafi la taifa. Sekta ya mifugo kwa sasa inachangia kwa kiasi kidogo, ikilinganishwa na idadi ya mifugo iliyoko nchini Tanzania.

Serikali imeanza kulivalia njuga suala hili kwa kuanzisha vituo vya kitaifa na kikanda kwa ajili ya kuzalisha mbegu bora zaidi sanjari na kuwahamasisha watu binafsi kushiriki katika mpango huu ambao ni mkubwa na unahitaji ushirikiano mkubwa kutoka kwa wadau mbali mbali.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kupima maeneo kwa ajili ya shughuli za ufugaji, ili kuwamilikisha wafugaji, ili maeneo haya yasiingiliwe na shughuli nyingine, kuepusha kinzani na migogoro kati ya wakulima na wafugaji nchini Tanzania.

Lakini kubwa zaidi ni kuendelea kuwafunda wakulima kutambua kwamba, wanapaswa kuongeza thamani ya mifugo yao na kuachana kabisa na ufugaji wa asili ambao kwa sasa hauna tija wala maendeleo kwa wafugaji wenyewe kutokana na ukweli kwamba, mifugo kwa watanzania wengi haijawaeletea ukombozi unaotarajiwa. Wengi wana mifugo, lakini bado wanaogelea katika dimbwi la umaskini na hali mbaya ya kiuchumi!

Dr. Titus Mlengeya Kamani anasema, Serikali inaendelea kuhamasisha wawekezaji kutoka ndani na nje ya Tanzania kuwekeza katika mchakato wa maboresho ya mifugo nchini Tanzania kwa kuongeza thamani ya mazao ya mifugo ili kuachana na mtindo wa sasa wa kuuza mazao ya mifugo kama malighafi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.