2014-11-25 15:23:38

Ziara ya Papa kwa Bunge la Ulaya: himizo na matumaini kwa bara la Ulaya


Baba Mtakatifu Francisko Jumanne 25 Novemba 2014, amefanya ziara ya Kichungaji ya kimataifa ya tano kwa kwenda Starsbourg Ufaransa, kwa madhumuni ya kulihutubia Baraza la Bunge la Ulaya. Papa Francisko katika ziara hii ameuvunja ukimya wa miaka 26, tangu Papa Yohane Paulo II alipotembelea na kulihutubia Bunge hilo tarehe 11 Oktoba 1988. Baraza la Bunge la Ulaya lililoanzishwa miaka 65 iliyopita na wajumbe wake ni wawakilishi kutoka mabunge ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya , Wawakilishi wa Nchi wanachama, Wanasheria kutoka Mahakama ya Haki za Binadamu na Taasisi zake mbalimbali.
Papa Francisko, kama mchungaji, amepeleka ujumbe wa shime na matumaini , kwa watu wa Bara la Ulaya, kujenga Ulaya mpya, bila kusahau sifa yake, iliyosimikwa katika mizizi ya historia yake ya nyuma yenye kulinda na kutetea tunu na hadhi ya binadamu. Amekumbusha kwamba, Mababa waanzilishi wa Umoja wa Ulaya, waliweka utu wa binadamu kuwa kituo rejea katika mipango yao yote ya utendaji si tu kwa watu wa Ulaya , au katika mitazamo ya kiuchumi lakini katika kujali ukuu na hadhi ya mtu, mahali popote duniani. Papa aliendelea kueleza kwamba, baada ya Vita Kuu ya II, kwa kweli, ilionekana hamu dhahiri katika kuhakikisha kwamba, utu wa mtu unakuwa kiini cha haki za binadamu, dhamiri ya thamani kubwa, katika uwepo wa usawa na ubinafsi wa kila binadamu. Ni wazi Baba Mtakatifu Francisko ameifanya ziara hii katika hali halisi kwamba, miaka 26, tangu Yohana Paulo II alipohutubia Bunge la Umoja wa Ulaya, kumetokea mabadiliko makubwa, nchi na mataifa zikiwa zimeungana zaidi, katika utandawazi, uliowezesha mataifa zaidi ya Ulaya kujiunga katika Umoja wa Ulaya tofauti na ilivyokuwa miaka ya zamani.
Katika hali hiyo ya watu mbalimbali kukaribiliana zaidi, Papa Francisko amesema, hivyo leo hii , jukumu la kukuza haki za binadamu, linapaswa kuchukua nafasi ya kwanza muhimu katika ahadi za utendaji wa Umoja wa Ulaya. Lakini kwa bahati mbaya, bado kuna hali nyingi mno ambapo binadamu anachukuliwa kama vile ni vitu au bidhaa isiyokuw ana thamani, hasa katika kubuni mipango ya maendeleo yenye kutanguliza faida binafsi. Mipango kama hiyo, baadhi ya watu hupuuzwa kwa sababu wao kuwa wanyonge, wagonjwa au wazee.
Papa aliendelea kueleza jinsi makundi ya watu hawa wanyonge, wanavyonyimwa au kukosa uhuru wa kueleza mawazo yao, au kukiri dini yao bila kikwazo, kutokana na kukosekana kwa mfumo wa kisheria wazi, yenye kuwa na uwezo wa kuweka mipaka katika nguvu za mamlaka za utawala na sheria ya kushinda dhuluma za mabavu na ubaguzi wa watu. Papa alieleza na kuhoji kuna utu gani , kwa mtu ambaye hana hata namna ya kupata chakula chake , au kuwa hata na namna ya kupata mahitaji yake ya lazima katika maisha na mbaya zaidi kufanyisha kazi zisizo heshimu utu wake?
Papa alizungumzia hadhi ya mtu katika asili yake, kuwa ni “dira" iliyochapishwa na Mungu katika kila moyo wa mtu tangu ulimwengu kuumbwa. Awali ya yote, ni hitaji la binadamu kuwa na mahusiano na binadamu mwingine. Leo , barani Ulaya, alionya Papa, kuna ugonjwa mkubwa wa upweke, kuna watu wengi wanaoteseka kwa sababu ya kukosa mahusiano haya . Upweke unaochochewa zaidi na mgogoro wa kiuchumi. Kuna hisia ya jumla ya uchovu na kuzeeka. Maadili ya Ulaya yanaonekana kupoteza nguvu yake ya kuvutia, kutokana na mifumo ya kiufundi inayozua ukiritimba katika taasisi. "Tunaona kwa masikitiko maambukizi ya kiufundi na kiuchumi katikati ya mjadala wa kisiasa ambamo hadhi ya mwanadamu inapunguzwa na kuwa kama vile ni kitu tu cha kujadiliwa kama bidhaa ya kutumika na kuondolewa bila kusita. Papa alieleza kwa kutoa mifano ya kesi ya wagonjwa mahututi, wazee kutelekezwa bila huduma na , watoto kuuawa kabla ya kuzaliwa. Pia aligusia Utamaduni wa taka na ulaji, unao vuruga ukamilifu mbinu za utendaji wa binadamu wenye kudumisha hadhi ya mtu, na dhamana ya maisha ya binadamu.
Hotuba ya Papa iliendelea kuzungumzia suala la amani, akirejea nyaraka za Mtangulizi wake Papa Paul VI, alidokeza kwamba hali ya ufanisi wa taasisini lazima kuendana na taratibu za sheria za kimataifa kwa ajili ya udumishaji wa amani. Amani haiwezi kupatikana kwa kufanya vita , lakini ni lazima kufikia amani kwa maafikiano na maridhiano kiroho. Ni kufundisha amani katika maana kuondoa utamaduni wa migogoro, wenye kujenga hofu ya nyingine ya ubaguzi au maisha tofauti. Migogoro iliyopo ni itazamwe mtazamo mpana bila kupoteza hisia za umoja katika hali halisi, au kuanguka katika kishawishi cha kuzua mapigano kama njia ya kufikia amani. Mivutano mara nyingi hujeruhi amani katika mengi ya dunia, na pia kama ilivyo barani Ulaya.
Papa Francisko, ameeleza na kusisitiza kuwa aina ya migogoro kama vile inayofanywa kwa mtindo wa ugaidi wa kimataifa kwa kisingizio cha dini, ni dharau ya kina kwa maisha ya binadamu. Dharau hii inashamirishwa na biashara ya silaha, zinazotengenezwa katika nchi zenye kuwa na utulivu. Amani pia leo hii inakiukwa kupitia aina mpya ya mfumo wa utumwa wa wakati wetu,ikiwemo usafirishaji haramu wa binadamu, biashara na ajira zenye kudhalilisha utu wa mtu na zenye kuwaondolea waathirika heshima zote za utu wao.
Miongoni mwa mambo mengine muhimu, aliyozungumzia Papa Francisco kwa lengo la kutoa matumaini kwa bara la Ulaya, ni haja kidharura kwa bara la Ulaya kurejesha utu wa kufanya kazi. Hii ina maana, anasema Papa kutafuta njia mpya yenye kuchanganya mabadiliko katika soko na mahitaji, kwa ajili ya utulivu na uhakika wa matarajio ya kazi, lakini wakati huohuo pia kuendeleza mazingira sahihi kijamii, yenye kuzuia unyonyaji wa watu, bali kuhakikisha, kwa njia ya kazi , uwezekano wa kujenga familia imara na utoaji wa elimu watoto wote.

Aidha, Papa Francisko inazungumzia suala uhamiaji kwamba ni jambo lisilo vumilika kuona Bahari inakuwa eneo la makuburi ya watu wengi. kwa hili, lazima kupendekeza wazi utambulisho wa utamaduni na kutunga sheria sahihi, ambazo zinaweza kulinda haki za raia wa Ulaya na wakati huohuo kuhakikisha mapokezi mazuri kwa wahamiaji na wakimbizi wanaofuta hifadhi mpya. Ni lazima na muhimu pia kwa Ulaya kupitisha sera thabiti za kusaidia nchi ya wanakotoka wakimbizi na wahamiaji, kuweza kukabiliana na migogoro ya ndani ya nchi, kijamii na kisiasa.
Papa alieleza na kutaja jinsi watu wengi wanavyoteswa na migogoro ya ndani, na shinikizo la imani kali za kidini na ugaidi wa kimataifa. Kama wabunge wa Ulaya, wana wajibu wa kuhifadhi na kukuza utambulisho wa Ulaya, ambao ni kuimarisha imani na uadilifu wa umma, na pia katika taasisi za Umoja wa Ulaya na jitihada zote zinazo lenga kujenga amani na amani na urafiki kati ya binadamu.

Papa alirejea pia historia ya Ukristo akisema, imeandika miaka elfu mbili, lakini bado kuna mengi ya kutenda kwa ajili ya kujenga kwa pamoja Ulaya yenye maridhiano, si tu katika uchumi, lakini pia uadilifu wa binadamu na , maadili yake yasiyoweza kuhamishika. Kujenga Ulaya mpya iliyo imara zaidi, iliyosimikwa katika misingi ya ujasiri wake wa tangu zama za kale, uliosimikwa katika mizizi ya Ukristo, yenye kuonyesha matumaini yake kikamilifu katika ukuu wa utu wa mtu, hata kwa siku za baadaye.
Papa hatimaye alizungumzia utayari wa Vatican na Kanisa Katoliki kwa ujumla, kupitia Tume ya Mabaraza ya Maaskofu ya Ulaya, COMECE, kushiriki kikamilifu katika kazi na majadiliano wazi na Taasisi za Umoja wa Ulaya. Na alionyesha kushawishika kwake kwamba, Ulaya ambayo daima hutambua mizizi yake ya kidini na kwa ushuhuda wa matunda ya uwezo wake , itaweza katika hali zote kupambana na kila aina ya ubabe wa kupindua, ulioanza kuenezwa duniani leo hii , kama matokeo ya utupu mkubwa kiroho kama inavyoshuhudiwa sasa katia nchi za Magharibi. Matunda ya binadamu kumwasi Mungu na kujitegenezea miungu wengine , na hivyo badala yake ni kuzuka kwa ghasia.
Papa amewahimiza Wabunge wa Ulaya kwamba, umefika wakati wa kujenga Ulaya yenye kukumbatia kwa ushupavu historia yake ya nyuma na kutazama kwa matumaini hali yake ya baadaye kwa ajili ya ukamilifu wa maisha na kwa matumaini ya siku za baadaye. Umefika wakati wa kuachana na wazo la kuwa na Ulaya yenye hofu , iliyojifungia yenyewe katika utendaji wa kisayansi, kisanii, Muziki na tunu za kiutu, na pia imani, lakini ni kuwa na Ulaya yenye mwamko katika kulinda na kutetea binadamu wote, Ulaya inayotembea duniani kote kwa uhakika kama kituo rejea cha ubinadamu wote.









All the contents on this site are copyrighted ©.