Tarehe 10 Januari Vatican kufanya mkutano maalum kwa ajili ya Haiti!
Kardinali Robert Sarah, aliyekuwa Rais wa Baraza la Kipapa linaloratibu misaada ya
Kanisa Katoliki Cor Unum, kuanzia tarehe 25 hadi tarehe 29 Novemba 2014 yuko nchini
Haiti, kutembelea Haiti ambayo miaka mitano iliyopita ilikumbwa na tetemeko la ardhi
na kusababisha watu laki mbili na thelathini kufariki dunia na wengine zaidi ya millioni
tatu kuathirika vibaya sana kutokana na tetemeko hili.
Lengo la safari hii
ya kichungaji ni kuonesha mshikamano wa Kanisa na wananchi wa Haiti katika mchakato
wa ujenzi wa Haiti mpya pamoja na kuzindua shule mpya iliyojengwa kwa msaada wa Kanisa
mahalia kwa kushirikiana na Ubalozi wa Vatican nchini Haiti. Akiwa nchini Haiti, Kardinali
Sarah anakutana na kuzungumza na viongozi wawakilishi wa Shirika la Misaada la Kanisa
Katoliki nchini Haiti, Caritas Haiti, ili kuangalia hali ya utoaji wa misaada ya Kanisa
nchini Haiti. Itakuwa ni nafasi kwa Kardinali Sarah kukutana na kuzungumza na viongozi
wa Serikali nchini Haiti.
Tarehe 28 Novemba, Kardinali Sarah atakutana na kuzungumza
na Familia ya Mungu nchini Haiti; watu wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kuwahudumia
jirani zao walioathirika kwa tetemeko la ardhi, lililoikumba nchi hiyo, miaka mitano
iliyopita. Wote hawa watafikishiwa salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu
Francisko.
Kutokana na kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya wananchi wa
Haiti, Baba Mtakatifu Francisko ameonesha nia ya kuitisha mkutano utakaofanyika mjini
Vatican hapo tarehe 10 Januari 2015, ili kuzungumzia matatizo na changamoto zilizopo
katika ujenzi wa Haiti mpya baada ya kuharibiwa vibaya na tetemeko la ardhi. Mkutano
huu utaandaliwa na Tume ya Amerika ya Kusini kwa kushirikiana na Baraza la Kipapa
linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki Cor Unum pamoja na Maaskofu mahalia.