Siku ya Kimataifa ya kupambana na nyanyaso na dhuluma dhidi ya wanawake na wasichana
duniani!
Dhuluma na nyanyaso za kijinsia dhidi ya wasichana na wanawake ni vitendo vinavyokwamisha
juhudi za ujenzi wa usawa kati ya watu sehemu mbali mbali za dunia. Dhuluma na nyanyaso
ni vitendo ambavyo havibagui wala kuchagua: rangi, mahali anapotoka mtu, cheo, hali
yake ya kiuchumi, kijamii na kitamaduni.
Takwimu zinaonesha kwamba, kati ya
wanawake watatu, kuna mwanamke mmoja ambaye amekwishawahi kunyanyaswa kijinsia, vitendo
ambavyo vinafanyika ndani ya familia, katika maeneo ya kazi na kwenye mitandao ya
kijamii.
Hii ni sehemu ya ujumbe Bwana Ban Ki-Moon, Katibu mkuu wa Umoja wa
Mataifa katika maadhimisho ya Siku ya Kupambana na Vitendo vya Unyanyasaji wa kijinsia
kimataifa; siku inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 25 Novemba. Jumuiya ya Kimataifa
inaadhimisha Siku hii, wakati kuna wasichana zaidi ya mia mbili waliotekwa nyara na
kunyanyaswa kijinsia huko Nigeria.
Kuna ushahhidi wa kutosha kwamba, wanawake
na wasichana nchini Iraq wanadhulumiwa utu na heshima yao kutokana na nyanyaso za
kijinsia. Mambo si shwari huko India na Marekani kwani bado kuna vitendo vya unyanyasaji
wa kijinsia vinavyofanywa kwenye timu za michezo na kwenye maeneo ya vyuo vikuu. Kwa
bahati mbaya wahusika wa vitendo hivi wanaendelea "kula kuku kwa mrija" bila ya kufikishwa
kwenye mkondo wa sheria! Maadhimisho haya pamoja na mambo mengine yanapania kukomesha
vitendo hivi na kuvunjilia mbali ukimya unnaoendelea kuhatarisha maisha ya wanawake
na wasichana.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anabainisha kwamba, kila mtu
anawajibu wa kuzuia pamoja na kupambana fika na vitendo vyote vinavyowanyanyasa na
kuwadhulumu wanawake. Tabia ya kuendekeza mfumo dume imepitwa na wakati; wale wote
wanaobainika kuhusika na vitendo hivi wafikishwe mbele ya sheria, ili kuunda na kujenga
mazingira ya usawa katika maeneo ya kazi na majumbani, ili kuleta mabadiliko katika
maisha ya wanawake na wasichana.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anasema, hivi
karibuni amezindua kampeni inayopania kujenga na kuimarisha mshikamano, usawa, ili
watu waweze kusaidiana, daima wakitafuta mafao ya wengi. Kila mtu atekeleze dhamana
na wajibu wake, ili ubaguzi uweze kukomeshwa na wavunjaji wa sheria kufikishwa kwenye
mkondo wa sheria pamoja na kuondokana na mila na desturi ambazo zimepitwa na wakati
kwa kuendelea kuwanyanyasa na kuakandamiza wanawake na wasichana.