2014-11-25 09:40:40

Neno kutoka kwa Watanzania wanaoishi Diaspora!


Ifuatayo ni Risala ya Watanzania wanaoishi Italia iliyotolewa na Mwenyekiti wa Watanzania wanaoishi Diapora Bwana Nsangu Kagutta Maulidi kwa niaba ya: Jumuiya ya Watanzania Italia, Jumuiya ya Watanzania Roma, Jumuiuya ya Wanafunzi Wakatoliki Roma, kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dr. Mohamed Gharib Bilal, tarehe 18 Novemba 2014 Jijini Roma, nchini Italia. RealAudioMP3

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Mh Mohamed Gharib Bilal. Mh. Balozi wa Tanzania Italia, Dkt James Alex Msekela, Waheshimiwa waliongozana na msafara wa Makamu wa Rais, Maofisa wa ubalozi, Viongozi wa Jumuiya za watanzania, Mabibi na Mabwana.

Kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia kukutana hapa. Siku ya leo itabaki katika kumbukumbu zetu kwani ni mara ya kwanza sisi Watanzania hapa Italy kupata nafasi hii ya kukutana na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Mohamed Gharib Bilal.

Tunapenda kukushukuru kwa kutenga muda wako ili kukutana nasi, tunafarijika sana kuona kuwa serikali yetu,pamoja na kuwa tunaishi ughaibuni lakini bado inatuhitaji na kututambua. Tunaipongeza serikali yetu kwa kuweka utaratibu huu mzuri.

Mh. Makamu wa Rais,
Tunaomba utufikishie salaam zetu za pole kwa Rais Dkt Jakaya Kikwete, tunamshukuru MwenyeziMungu kwa kupokea dua zetu kwani hali yake inaendelea kuimarika zaidi. Tunamuomba Mungu amponye kwa haraka ili aweze kurudi kazini kwenye majukumu mazito ya taifa letu. Nachukua nafasi hii pia kwa niaba ya Watanzania wote hapa Italia kumshukuru sana balozi wetu Dkt James Msekela kwa
kuanza kwa kasi kuyafanyia kazi matatizo na kero za watanzania mara tu baada ya kukutana na kamati ya uongozi wa Diaspora, mwezi Juni mwaka huu 2014. Tumeshuhudia kuja kwa maofisa wa uhamiaji na tayari wamekwisha anza kazi.

Mh. Makamu wa Rais
tunatoa pongezi kubwa kwa serikali kwa utekelezaji wa ahadi kwa kiasi kikubwa. Tumeona maendeleo ya miundo mbinu, barabara, maji ,umeme elimu ya awali mpaka ya juu. Ingawa bado inasikitisha jinsi gani ajali za barabarani zilivyo ongezeka kwa kiasi kikubwa,tofauti na wakati barabara zetu zilivyo kuwa hazina kiwango cha lami.

Hii inaonesha kuwa bado lipo tatizo kwa waendeshaji wa magari hasa ya abiria na mizigo na utendaji wa maofisa wetu wa usalama barabarani. Tunaomba Serikali kuwa wakali zaidi katika hili kwani ajali zimekuwa nyingi kiasi ukisikia ndugu yako au mzazi anasafiri unakuwa huna raha kabisa mpaka afike. Pamoja na hayo lakini pia tumeshuhudia nchi yetu ikipiga hatua katika utawala bora na kuzidi kuendeleza demokrasia ya kweli.Tunaipongeza serikali yetu pia kwa kuendelea kuhakikisha nchi yetu inakuwa na amani na kushiriki kimataifa katika kuimarisha amani hasa katika Bara letu.

Mh. Makamu wa Rais,
Tunatoa pongezi zetu za dhati kwa Rais Dkt Jakaya Kikwete na Serikali kwa jumla kwa kufanya maamuzi ya kihistoria ya kukubali kuifanyia mabadiliko katiba ya jamhuri ya muungano wa Tanzania kwa manufaa ya nchi yetu. Pamoja na changamoto nyingi lakini bunge maalum la katiba kwa usimamizi wa viongozi wetu mahiri wameweza kukamilisha katiba inayopendekezwa.

Kama tunavyofahamu kuwa mapema mwakani kutakuwa na kura ya maoni itakayo pigwa na wananchi wote kuikubali au kuikataa katiba iliyo pendekezwa na Bunge maalum. Sote tunakumbuka katika mchakato wa kukusanya maoni kwa ajili ya rasimu ya katiba kulitengenezwa utaratibu na tume ya Mzee Warioba wa kuwawezesha watanzania waliopo nje kuchangia maoni. Tunaomba tusinyimwe haki yetu ya kidemokrasia ya kupigia kura katiba iliyopendekezwa.

Mh. Makamu wa Rais,
Mwaka 2007 alikuja Rais Dkt Jakaya Kikwete hapa Italy, na tulipata nafasi kama hii ya kukutana nae,Moja kati ya maswali ambayo tuliuliza lilikuwa suala la kuwepo na utaratibu wa kupiga kura kwa Watanzania ughaibuni, tunakumbuka alisema kuwa ikiwa nchi zingine zinaweza kuwafanya wananchi wake walioko nje kupigakura kwa nini Tanzania ishindwe?

Tanzania ni moja ya nchi mfano katika bara la AFRIKA kwa utawala wa kidemokrasia, hivyo kutopewa nafasi ya kupiga kura katika uchaguzi mkuu ,kwa Watanzania walioko nje nikuwanyima haki yao kubwa ya kidemokrasia. Tunaomba serikali yetu tukufu kulifanyia kazi jambo hili kabla ya uchaguzi mkuu 2015 ili na sisi tuweze kushiriki katika maamuzi makubwa ya nchi yetu,tupige kura kumchagua Rais wa awamu ya tano.

Mchakato wa uraia pacha tunaona haukupatiwa jibu sahihi lakini sio sababu ya kuwa limesahaulika, tunaamini ni jambo zito linahitaji kufanyiwa taratibu stahiki, ila serikali isiangalie hasara zake tu bali iangalie na faida zake. Katika awamu ya nne, serikali imetoa kipaumbele kwa diaspora na kuweka mikakati mingi itakayoweza kuwawezesha diaspora kuchangia maendeleo ya taifa kiuchumi na kijamii. Huku ugahibuni kuna wasomi wengi ambao wanaweza kusaidia katika nyanja mbalimbali katika maendeleo ya taifa.

Tunaomba serikali iliangalia hili kwa makini zaidi, kwani tunaamini serikali inatumia pesa nyingi katika kuwalipa wataalaamu (expertise) kutoka nje, wakati wapo Watanzania ambao wana ujuzi huo au zaidi, wangeweza kufanya kazi hiyo kwa gharama tofauti ikiwa tu wangeruhusiwa kurudishiwa urai wao. Kuna watoto wengi sana ambao wamezalia huku na kupata elimu za juu, ambao ni hazina kubwa ya taifa letu ikiwa tutaweka mipango mizuri .

Mh. Makamu wa Rais,
Watanzania walioko nje wana mapenzi sana na taifa lao, ndio maana hata watoto waliozaliwa na Watanzania hao huku nje wana mapenmzi hayo hayo au zaidi, tusiwaache hawa wakatumiwa na wengine kwa maendeleo ambayo haya takuwa na tija na taifa letu. Mbali ya wasomi pia wapo wanamichezo ambao nao pia ikiwa watapewa uraia wetu wataweza kutuwakilisha kimataifa, hasa ukizingatia taifa letu katika michezo tumezidi kurudi nyuma. Mfano wa wenzetu kama Kenya na nchi zingine za AFRIKA wanao wanamichezo wao ambao wanaishi nje lakini inapofikia mashindano ya kimataifa huwa wanawakilisha nchi zao za asili. Kwa mifano hiyo na mingine tunaomba suala la urai pacha lisisahaulike.

Changamoto ughaibuni:
Mh. Makamu wa Rais,
Jumuiya za watanzania huku ughaibuni zinaendeshwa kwa kujitolea. Tuna changamoto nyingi sana,hasa inapofikia kwenye matatizo ya maradhi au vifo. Tukizungumzia maradhi kuna maradhi na maradhi, kwani upande huo huku kuna unafuu mkubwa hasa katika matibabu ya uhakika, lakini wakati mwingine inafikia mgonjwa anahitaji kuwa karibu na wazazi na ndugu zake ili aweze kupata nafuu ya haraka. Nakumbuka tumesha wasafirisha wagonjwa wengi tu kwa ridha yao wenyewe na wazazi wao, na wengi wanapofika nyumbani wanapona au kupata nafuu kubwa.

Misiba: Ni muda mrefu sana tangu hatuja kuwa na jumuiya hizi, Watanzania wamekuwa wakiishi katika tamaduni zile zile za nyumbani za kuwa pamoja wanapofikwa na misiba. Lakini haikuwa rahisi kama tulivyokwisha unda jumuiya za watanzania.jumuiya zimekuwa ndio chombo maalum cha kuwaunganisha Watanzania wote bila kujali itikadi zetu,Tumeweza kwa pamoja kusafirisha miili ya marehemu wetu wengi sana kwenda nyumbani kwa mazishi.

Kwa kufanya hivyo tumewapa faraja sana wazee kule nyumbani. Kwani wengi wa hao marehemu walikuwa wana msaada mkubwa sana na familia zao.Naomba nitoe pongezi mbele ya Makamu wa Rais ,Kwa niaba ya diaspora committee, kuwapongeza viongozi wote wajumuiya za Watanzania,wanajumuiya na watanzania wote kwa kuwa na moyo wa kujitolea na kushirikiana kwa kila hali.

Mh. Makamu wa Rais,
Kama ambavyo serikali yetu inavyo tambua na kuthamini mchango mkubwa unaotolewa na diaspora kwa taifa letu,tunaona wakati umefika sasa kwa wizara husika kutenga fungu la kusaidia diaspora kwenye matatizo ya maradhi na misiba.
Tumeona kuwa katika hili wapo wadau wa NSSF ambao wana bima ya Westadi kwa diaspora, lakini bado tunaona haitoshelezi katika kutuwezesha. Kwa sababu ni ya mmoja mmoja,linapomfika jambo ambae hayumo na NSSF bado linakuwa ni tatizo la Jumuiya zetu ambazo ni jumuiya za kujitolea.na huko NSSF hakuna suala la huduma kwa diaspora ambaye anataka kurudi nyumbani, aidha kwa maradhi au kwa kuwa na ugumu fulani.

Tunaomba NSSF waangalie upya utaratibu wao wa Bima ya Westadi,ikiwezekana kuwepo na bima ya pamoja yaani kwa Wanajumuiya waliojiandikisha kwa mujibu wa katiba zetu. Jumuiya zetu zina mchango mkubwa sana hasa kwa balozi zetu, jumuiya zinarahisishia kujua wapi wapo Watanzania, matatizo yao, na pia kupata taarifa za haraka pale inapohitajika. Pia zinasaidia ubalozi pale unapo hitaji kufikisha taarifa kwa Watanzania, nk.Kwa uwajibikaji huo wa jumuiya zetu tunaomba serikali iangalie uwezekano hata wa kuzitumia ofisi za jumuiya zetu kama balozi za heshima, na kuzisaidia gharama ndogo za uendeshaji.

Mh. Makamu wa Rais,
Tumeshuhudia kwenye awamu hii ya nne kuwepo kwavitengo maalum vinavyo shughulikia masuala ya diaspora kwenye wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa na pia kwa waziri mkuu,Tunaona umefika wakati wa kuona umuhimu wa kuwepo muwakilishi wa diaspora katika bunge la Jamhuri ya muungano wa Tanzania kama ilivyofanyika katika bunge maalum lakatiba. Kwa kufanya hivyo itasaidia kupendekeza mbinu nyingi za kuwashirikisha diaspora katika maendeleo ya nchi. Suala la diaspora nchi yetu ndio kwanza imelitilia mkazo kwa hiyo tunahitaji kushirikishwa zaidi ili kuongeza ufanisi katika nyanja mbalimbali hata kubuni utaratibu wetu wenyewe wa kutuma remittance , kwani yanafaidika sana makampuni ya nje katika hili.

Mh. Makamu wa Rais,
Tunamaliza kwa kukushukuru sana wewe binafsi, na Mh. Balozi, kwa kutupa nafasi hii adimu, kukutana nawe na kusema machache, na zaidi tuna hamu sana ya kukusikiliza, utupe salaam zetu nasi utakaporejea nyumbani utupelekee salaam zetu.
Ahsante sana.

MUNGU IBARIKI AFRIKA.
MUNGU IBARIKI TANZANIA.








All the contents on this site are copyrighted ©.