2014-11-25 14:50:01

Kiti moto! Bunge la Tanzania!


Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Anne Makinda amesema mjadala ndani ya Bunge kuhusu sakata la akaunti ya Escrow upo pale pale na hakuna mhimili mwingine wowote unaoweza kulizuia Bunge kufanya hivyo. ‘’Wabunge msiishi kwa wasiwasi sisi kanuni zetu zipo wazi hakuna mtu au muhimili unaoweza kutuzuia kufanya kazi yetu ya kibunge, hiyo haipo,’’ alisema Makinda.

Spika alitoa mwongozo huo baada ya kuombwa na Mbunge wa Bariadi Mashariki John Cheyo (UDP) mara baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu. Katika mwongozo wake kwa mujibu wa kanuni ya 68(7) Cheyo alisema kuna taarifa kuwa sula hilo la Escrow ambalo Bunge linatakakujadili kwa sasa limepelekwa Mahakamani ili kuzuia Bunge kuendelea kujadili suala hilo.

‘’Mheshimiwa Spika sasa naona hii tabia hapa nchini imekuwa imeshamili kukiwa na jambo ambalo Bunge linashughulikia watu wengine kiujanja unjanja wanakimbilia mahakamani kulizuia Bunge kufanya kazi yake naomba muongozo wako katika hili,’alisema Cheyo.

Akitoa muongozo wake Spika aliwataka wabunge kuacha kuishi kwa wasiwasi kwa kuwaeleza kuwa hakuna mtu anayeweza kulikataza bunge kufanya kazi yake. Spika alisema hapo awali waliambiwa kuwa kuna kesi nyingi mahakamani ambazo zinahusiana na suala hilo la akaunti ya Escrow. Alisema hata hivyo baada ya kufuatilia kesi hizo zote hakuna kesi mahususi inayohusu jambo ambalo Bunge linaenda kujadiliana juu ya sakata hilo la Escrow.

Spika Anne alisema Bunge lina sheria zake za kinga na kama kutakuwa na muhimili mwingine ambao unakuwa na uwezo wa kuzuia bunge kufanya kazi yake basi hakutakuwa na Bunge.’ ‘’Mjadala wetu upo pale pale na kwa sasa nasubiri kama Kamati yetu ya PAC imekamilisha kazi yake ili nao watuletee taarifa yao hapa bungeni tuijadili’’

Hata hivyo Spika alisema mpaka Jumatatu asubuhi alikuwa bado hajapata taarifa kutoka kwa Mwenyekiti wa PAC Zitto Kabwe kama wamekamlisha kazi yao kwani kikanuni ni lazima wakikamilisha kazi hiyo hutakiwa kumtaarifu Spika kwa barua ilinaye aingize katika shughuli za Bunge. Aidha Makinda alisema pamoja na kuendelea na mjadala huo pia wabunge jana watapewa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa majina.


Spika alisema nia ya kugawa taarifa hiyo ya CAG kwa majina ni kuepukana na taarifa hizo kuwafikia watu wengine ambao si wabunge. Alisema taarifa kutoka Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali PAC itagawiwa leo mara baada ya kamati hiyo kuwasilisha bungeni taarifa yao.‘’Hatuwezi kuweka mezani taarifa ya CAG kwani tukiweka hivyo Kamati haiwezi kuleta tena taarifa yao hivyo tunagawa taarifa hiyo ya CAG kwa majina ili taarifa ya kamati ndiyo itawekwa mezani mara nitakapopata taarifa kuwa wamemaliza kazi yao,’’alisema. Alisema taarifa hiyo ya CAG itatumika kama kiambatanishi baada ya kutolewa kwa taarifa ya kamati ya PAC ambayo inatarajiwa kutolewa leo bungeni.

Naye kwa upande wa John Mnyika (Ubungo-Chadema) alimpongeza Spika kwa uamuzi wake wa kusisitiza kuingizwa bungeni kwa taarifa hizo mbili.Mnyika alisema hayo alipokuwa akioomba muongozo wa Spika kuhusiana na kesi iliyofunguliwa katika Mahakama Kuu kuhusiana na Akaunti ya Tegeta Escrow. ‘’Kwanza nikupongeze kwa uamuzi wako wa kusema kwamba hakuna jambo ambalo litazuia bunge kuletewa hiyo ripoti na kuijadili lakini mheshimiwa Spika ningependa utuhakikishie hili’’.

‘’Mimi nina taarifa ndio maana nasema utuhakikishie,naomba nikusomee Pan African Power wamefungua kesi ‘’High court’’ kuzuia mjadala wa Escrow bungeni walengwa wakiwa ni pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu, CAG, PCCB, na Wizara ya Nishati na Madini, mheshinmiwa spika mimi naomba muongozo wako,’’ alisema Mnyika.

Alisema ni vyema Ofisi ya Spika ikachunguza kama taarifa hiyo ni ya kweli au la lakini hata kama ikichunguza na hata kama jambo hili ni kweli bunge lisikubali kwa namna yoyote madaraka yake na mamlaka yake kuingiliwa. ‘’Mheshimiwa Spika naomba mwongozo mahususi kabisa katika eneo hili mjadala huu lazima ufanyike na ututangazie kwamba, mjadala huu unaanza kujadiliwa,’’alisema. Katika kujibu mwongozo huo Spika alirejea kauli yake kuwa hawezi kutamka rasmi kwamba leo Mjadala huo utaanza ila anasubiri taarifa kutoka kwa Mwenyekiti wa PAC kama wamemaliza kazi yao.









All the contents on this site are copyrighted ©.