Mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ebola Barani Afrika bado hayajafanikiwa kupata ushindi
unaotarajiwa, mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kusaidia kuchangia kwa hali na mali
katika mchakato wa mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ebola ambao kwa sasa ni tishio kubwa
la maisha, ustawi na maendeleo ya watu wengi duniani.
Ni kilio kilichotolewa
hivi karibuni na Bwana Anthony Banbury, Mratibu wa ugonjwa wa Ebola kutoka Umoja wa
Mataifa, alipokuwa anazungumza na wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa,
katika kikao chake kilichokuwa kinafanyika mjini New York. Taarifa za Shirika la Afya
Duniani zinaonesha kwamba, kuna watu zaidi ya 5, 459 na watu wengine 15, 351 wameambukizwa
ugonjwa wa Ebola. Hali bado ni mbaya nchini Guinea, Liberia na Sierra Leone.
Nigeria
imeondolewa kwenye orodha ya nchi zenye ugonjwa wa Ebola. Mali na Senegal bado zinaangaliwa
kwa tahadhari zaidi. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon anazitaka nchi
mbali mbali ambazo zina wagonjwa wa Ebola kujifunza kuwa makini zaidi kutoka katika
nchi ambazo zimeathirika kutokana na ugonjwa huu, ili kuokoa maisha ya watu.
Wagonjwa
wapewe huduma muhimu zinazohitajika sanjari na kudhibiti kuenea kwa ugonjwa wa Ebola
kwa watu wengine. Na habari zaidi zinasema kwamba, Italia, Jumanne, imepokea mgonjwa
wa kwanza wa Ebola, Daktari aliyekuwa anafanya kazi ya kutibu wa wagonjwa wa Ebola
nchini Sierra Leone.