2014-11-24 08:24:15

Familia ziwe ni kitovu cha maadili na adabu njema!


Mpendwa Msikilizaji wa kipindi chetu cha Kanisa la nyumbani, Tumsifu Yesu Kristo. Kwa mara nyingine tena tunakukaribisha katika kipindi chetu cha Kanisa la nyumbani, ambapo kwa wakati huu tunazipitia kwa ufupi hati za Mtaguso wa pili wa Vaticani ili kutokamo tuweze kuchota vichocheo vya imani katika familia zetu. RealAudioMP3
Leo tunaitazama hati ya kichungaji inayoitwa “Gaudium et spes”, maneno yanayomaanisha ‘Furaha na Matumaini’. Imesheheni mambo ya kiimani na ya kijamii, na pia inalenga zaidi kulielezea Kanisa katika ulimwengu wa kisasa. Hii ni hati ya kichungaji kwa sababu inatoa aina ya mwongozo kwa ajili ya maisha ya watu katika uhalisia wa nyakati zetu.
Kwa namna ya pekee hati hii inamwalika mwamini kuishi sasa, huku akisoma ishara za nyakati na wakati huohuo bila kupoteza mwelekeo wa kufaa katika kumtafuta Mungu na kupata wokovu. Kwa maneno na ndani, hati hii inatuweka macho, ili tusilemewe na ulimwengu huu na tukapoteza lengo letu kikomo.
Kanisa halijioni tena mbali na ulimwengu, wala dhidi ya ulimwengu, bali ndani ya ulimwengu. Kifungu cha kwanza cha hati hii ya Kikatiba kinaanza kwa kusema, ‘furaha na matumaini, uchungu na fadhaa ya wanadamu wa nyakati zetu, hasa ya masikini na ya wale wote wanaoteswa, yote ni furaha na matumaini, uchungu na fadhaa ya wafuasi wa Kristo pia. Aya hii inatuambia kuwa sisi Wakristo tunasafiri duniani pamoja na binadamu wenzetu, tukishiriki shida na mateso ya nyakati mbalimbali.
Furaha na mateso vinavyowakumba waana wa ulimwengu, vivyo hivyo hukumbwa pia waana wa Kanisa; kwa sababu waana wa Kanisa wapo pia ulimwenguni. Wito kwa waana wa Kanisa; kuishi ulimwenguni, kushiriki shughuli za kijamii na yote yasiyopingana na mafundisho ya imani na maadili yetu ya Kikristo.
Sehemu ya kwanza kabisa, inaeleza hadhi ya binadamu yeyote. Pamoja na kumtazama binadamu kama kiumbe bora kuliko viumbe vyote duniani, Kanisa linaenda mbele zaidi kwa kumtazama binadamu huyu kama sura na mfano wa Mungu mwenyewe. Hata baada ya kuathiriwa na dhambi, dhambi haikuondoa hadhi hiyo ya ndani kabisa ya mwanadamu. Ni katika msingi huo binadamu mbele ya macho ya jamii adilifu, anastahili heshima ya utu wake mkamilifu, kiroho na kimwili.
Kanisa linafundisha kuwa, mtu huyu aliye sura na mfano wa Mungu, anaweza kujitambua kuwa ni kiumbe wa pekee kwa sababu anashiriki nuru ya fikra ya Mungu. Na kwa akili zetu tunafanya ugunduzi mbalimbali wa kisayansi ambao kwa kiasi kikubwa unasaidia kufanya maisha kuwa mepesi zaidi.
Kanisa linatuelekeza kwamba, ili akili za mwanadamu zimuongoze katika furaha ya kweli, tunahitaji hekima na dhamiri ya kimaadili. Akili nyingi peke yake, isiyo na uadilifu wala hekima ya kimungu, akili hiyo huwa ni akili angamizi kwa mtu binafsi na kwa ulimwengu pia. Leo hii tunashuhudia vilio vingi vya familia ya mwanadamu, vinavyotokana na mifumo angamizi ya sera za kiuchumi, afya, elimu, mawasiliano na mifumo ya siasa chafu.
Yote hayo hutokana na matumizi ya akili isiyojua uadilifu wala dhamiri wajibifu mbele ya Mungu na watu wake. Hivyo wenye akili wengi, badala ya kuchangia katika furaha na matumaini ya mwanadamu, wanachangia katika kuleta majanga, vilio namahangaiko makuu ya mwanadamu.
Pamoja na mambo megine mengi, hati hii inatuelekeza pia juu ya wajibu wetu wa kutegemezana katika jamii na kutenda mambo kwa manufaa ya wote huku tukilenga zaidi heshima kwa binadamu. Hati hii ya kichungaji ambayo ni ndefu kuliko zote, imegusa maeneo mengi sana ya maisha ya mwanadamu. Lakini kwetu sisi tunaolipepea kanisa la nyumbani, tuyachote machache ambayo yatatusaidia sisi wanafamilia kama Kanisa la nyumbani, tuwe shule ya utu, hekima na ushirikiano mwema na majirani zetu.
Kama tunavyoalikwa na kile kifungu cha kwanza, nasi wanafamilia tuiweke hivi: furaha na matumaini, uchungu na fadhaa ya familia majirani zetu, yote ni furaha na matumaini, uchungu na fadhaa ya familia yetu pia. Hati hii kwa wakati huu, ilete mambo makubwa matatu katika familia yetu.
Kwanza kabisa, kujali utu. Katika hili tunataka kusema, familia zetu ziwe ni shule za utu. Tunu za utu na maadili mema zifundishwe katika familia zetu. Watoto wetu na wote wapitao kwetu, wajifunze juu ya utu kama kitu cha thamani kubwa sana. Watoto wafunzwe namna ya kujitunza, kujithamini na kuthamini binadamu wenzao kama viumbe wa Mungu, walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu mwenyewe. Hili ni jukumu la wazazi, wote wenye dhamana ya malezi na Kanisa pia kwa upande wake. Huku wakilenga kuheshimu utu, watumie akili zao zote katika kujenga na kulinda utu wao. Na sisi watu wazima tuwaoneshe mfano wa kujali utu ne heshima ya mwanadamu kwa kujijali na kujiheshimu sisi wenyewe.
Jambo la pili tunaloletewa na hati hii katika Kanisa la nyumbani, ni wajibu wetu wa kumtazama jirani. Kama kilio cha jirani ni kilio chetu pia, basi hapo tunaalikwa kwa dhati kabisa kupiga vita kila maelekeo ya ubinafsi na ubaguzi. Wakati mwingine tunafunikwa na uchoyo-mkorofi ambao tunashindwa kabisa kuona mahitaji na kilio halali cha jirani. Tunajiziusha ili tusisikie kabisa kilio cha jirani.
Tunajipofusha ili tusione kabisa mahangaiko ya jirani. Kwa hali hiyo, tunachangia katika mahangaiko makubwa zaidi kwa jirani. Tuamini kwa dhati kwamba, hali njema ya mwanadamu haitajengwa na jamii ya kimataifa peke yake, tuanze sisi wenyewe ndani ya familia na katika ujirani wetu.
Kutokana na tabia ya uchoyo, ubinafsi, wivu na roho mbaya, mara nyingi tumechangi kukomaa kwa mahangaiko ya jirani. Halafu huyo jirani akifikia hatima ya majanga yake, tunajifanya kushangaa na kuililia serikali au jumuiya ya kimataifa. Kabla ya kufikia huko, sisi wenyewe tujiulize tu, tunafanya nini katika kushiriki furaha na matumaini, kilio na fadhaa za jirani zetu.
Tunaamini kwa dhati kabisa kwamba, sisi wakristo tutakuwa wakristo kweli, endapo tu tutaweza kwa roho ya upendo, kuelekeza sikio letu kwa kilio cha jirani, kufungua macho yetu kutazama mahangaiko ya jirani na kukunjua mikono yetu kwa ukarimu ili kumsaidia jirani yetu bila kujali anatoka wapi, anaabudu nini au anaamini nini. Na ukarimu huo, unafundishwa kuanzia katika familia na mashuleni. Ukarimu unaofundishwa katika familia huzama moyoni mwa mtu na baadaye huwa ndiyo tabia yake.
Jambo la tatu tunaloelekezwa na hati hii katika familia zetu, ni kuwa makini na mambo ya kisasa. Sote kwa akili safi tunakiri kwamba, usasa una mambo yake na baadhi ni mazuri sana. Lakini tunaomba turudie tena lile neno letu: sio kila kitu kizuri kinafaa. Na sio kila kitu kizuri ni kizuri kwa kila mtu na kila mahali na kila wakati.
Akili zetu tambuzi kwa msaada wa hekima ya kimungu, zitusaidie kupemmbua mambo vizuri, ili usasa usitupeleke dhambini hadi tukajikuta tumejihaini sisi wenyewe na mwisho tumemwasi Mungu wetu.
Tunaiahirisha hati hii kwa kutoa mwaliko binafsi: ewe msikilizaji unafanya nini cha ziada ili kushiriki katika kuleta hali njema kwa jirani? Na sisi wenye familia, tunafanya nini ili kuwafundisha watoto wetu utu na upendo kwa jirani? Na zaidi ya hayo, tunajisikiaje jirani zetu wanapopatwa na majanga mbalimbali? Basi ni mwaliko kwetu sote, kila mmoja wetu na awe wa msaada kwa mwenzake. Familia yetu na iwe ya msaada kwa familia majirani. Ni kwa njia hiyo tu, sisi tunakuwa wakristo kweli, tunaotangaza na kuuishi upengo wa Mungu.
Kutoka katika Studio za Radio Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.