2014-11-21 09:06:40

Umoja na mshikamano katika maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu!


Sekretarieti ya Sinodi ya Maaskofu, hivi karibuni imehitimisha mkutano wake wa nane, uliopembua kwa kina na mapana maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya familia, yaliyofanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 5 hadi tarehe 19 Oktoba 2014. Wajumbe wameanza kudonoa kauli mbiu itakayofanyiwa kazi na Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kuanzia tarehe 4 hadi tarehe 25 Oktoba 2015, kwa kuongozwa na kauli mbiu "Wito na utume wa Familia katika Kanisa na Ulimwengu mamboleo".

Wajumbe walipata bahati ya kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko, aliyekazia pamoja na mambo mengine, umuhimu wa maadhimisho ya Sinodi kama kielelezo cha mshikamano wa Maaskofu na Familia; mambo makuu yanayoendelea kufanyiwa kazi na Mama Kanisa katika maadhimisho ya Sinodi hizi mbili.

Kardinali Lorenzo Baldisseri katika hotuba yake ya ufunguzi, amefafanua mambo makuu yaliyojitokeza wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya kwanza ya Maaskofu kuhusu familia kwamba, wajumbe wameonesha ukomavu, ukweli na mshikamano wa kidugu, kiasi kwamba, Mababa wa Sinodi waliweza kutoa mchango wao. Hati ya Mababa wa Sinodi inaonesha mawazo makuu yaliyojitokeza katika maadhimisho ya Sinodi hii ya Maaskofu.

Wajumbe wanasema, wakati huu, Familia ya Mungu inapojipanga kuadhimisha Awamu ya Pili ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu Familia, kuna haja ya kuendeleza majadiliano katika ngazi mbali mbali kuhusiana na tema zilizotolewa wakati wa maadhimisho ya Sinodi, bila kusahau changamoto na magumu yaliyopo. Wadau mbali mbali wanaojihusisha na masuala ya familia, washirikishwe kikamilifu, bila kusahau mchango wa vyombo vya mawasiliano ya jamii.

Wajumbe wa Sekretarieti wametumia muda mrefu zaidi kwa ajili ya kuandaa "Mwongozo wa Kazi" "Lineamenta" kwa ajili ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya familia. Hati hii itatumwa kwenye Mabaraza ya Maaskofu Katoliki, ili kufanyiwa tafakari ya kina, mwanzoni mwa Mwezi Desemba 2014, ili majibu yake yaweze kurejeshwa na kuanza kuandaa "Hati ya kutendea Kazi" yaani "Instrumentum Laboris" kabla ya kipindi cha kiangazi cha Mwaka 2015.







All the contents on this site are copyrighted ©.