Umoja kamili miongoni mwa Wakristo ni kipaumbele cha kwanza kwa Kanisa Katoliki
Kuanzia tarehe 18 hadi tarehe 21 Novemba 2014, Baraza la Kipapa linalohamasisha umoja
wa Wakristo linafanya mkutano wake wa mwaka sanjari na maadhimishoya Jubilee ya miaka
50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipochapisha hati inayokazia
majadiliano ya kiekumene miongoni mwa Wakristo, inayojulikana kwa lugha ya Kilatini,
Unitatis redintegratio.
Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa washiriki
wa mkutano huu, anasema, Kanisa lina kila sababu ya kummshukuru Mungu kwani changamoto
ya majadiliano ya kiekumene imepokelewa na Makanisa mengi na kwamba, katika kipindi
cha miaka ya hivi karibuni, imekuwa ni kikolezo cha majadiliano ya kiekumene yanayojikita
katika Maandiko Matakatifu na Mapokeo ya Kanisa.
Makanisa mbali mbali yamepembua
kwa kina na mapana na kwamba, chuki na uhasama uliosababisha madonda makubwa miongoni
mwa Wakristo ni kurasa chungu zilizopitwa na wakati, sasa Wakristo wanaendelea kushikamana
kwa dhati, huku wakitambuana kuwa ni ndugu, umoja unaofumbatwa kutoka katika Sakramenti
ya Ubatizo.
Wakristo wamepata mabadiliko makubwa ya mwelekeo na mawazo, dhana
ambayo imesambazwa pia hata katika mikakati ya maisha ya shughuli za kichungaji katika
Makanisa mahalia, kwa kuendelea kusali kwa ajili ya kuombea umoja wa Kanisa, ili wote
wawe wamoja! Hata hivyo, bado kuna haja kwa Makanisa kuendelea kutafuta njia nyingine
zaidi za ushirikiano kwani hadi sasa kumekuwepo na tafsiri ya Biblia Takatifu kwa
pamoja; huduma za kijamii pamoja na kusimama kidete kulinda na kutetea maisha, utu
na heshima ya binadamu; kulinda na kutunza mazingira pamoja na kupambana na mambo
yote yanayotatiza haki msingi za binadamu.
Khalifa wa Mtakatifu Petro ni kielelezo
cha upendo wa Kanisa. Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza
wale wote waliojibidisha kujenga na kukuza huduma ya upatanisho, umoja na mshikamano
miongoni mwa wakristo, lakini zaidi wale walioshirikiana kwa karibu zaidi na Baraza
la Kipapa la kuhamasisha umoja wa Wakristo.
Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba,
bado kuna utengano ndani ya Kanisa unaosababishwa na tema za kibinadamu na kimaadili;
mambo yanayogumisha hija ya umoja kamili, lakini hakuna haja ya kukata tamaa, bali
kuendelea kumtumainia Mwenyezi Mungu, anayepandikiza mbegu ya upendo na umoja, ili
kukabiliana na changamoto za kiekumene katika ulimwengu mamboleo. Hapa kuna haja ya
kujenga na kukuza majadiliano ya kiekumene yanayosimikwa katika maisha ya kiroho kwa
kuthamini uekumene wa damu na kutembea katika njia ya Injili.
Uekumene wa maisha
ya kiroho kilele chake ni juma la kuombea umoja wa Kanisa, dhamana inayotekelezwa
katika ngazi mbali mbali za maisha na utume wa Kanisa, ili kujenga upendo na umoja
kwa njia ya tafakari ya Neno la Mungu. Mitandao ya kijamii iwasaidie Wakristo kufahamiana
zaidi. Wakristo waendelee kuthamini Uekumene wa damu, kwa Wakristo walioyamimina maisha
yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, mbegu ya ushuhuda wa maisha yao, ulete toba
na wongofu wa ndani, ili kukuza na kudumisha udugu, kwani dhuluma na nyanyaso za kidini
haziwabagui Wakristo kwa madhehebu yao.
Baba Mtakatifu anasema, kuna hamu kubwa
mioyoni mwa watu kutembea, kusali, kufahamiana na kumpenda Kristo kwa pamoja sanjari
na kuendelea kushirikiana na kujenga mshikamano kwa ajili ya huduma kwa maskini na
wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hii ni hija ya pamoja inayotekelezwa kwa
nguvu ya Roho Mtakatifu. Umoja kamili ni changamoto endelevu inayopewa kipaumbele
cha kwanza na Kanisa Katoliki, kwa kutambua kwamba, umoja ni zawadi kutoka katika
Fumbo la Utatu Mtakatifu.