Sekta ya uvuvi duniani inakabiliwa na changamoto nyingi kiasi kwamba, wavuvi wenyewe
hawaridhiki na mafanikio yanayopatikana kutokana na jitihada wanazofanya kila siku.
Hili ni kundi la watu linalotumia muda wake mwingi kwa ajili ya kazi, kiasi kwamba,
hata wakati mwingine wanakosa muda wa kukaa pamoja na familia zao. Ni kundi ambalo,
halijapewa kipaumbele cha pekee katika shughuli na mikakati ya kichungaji na Makanisa
mahalia.
Hii ni sehemu ya ujumbe kutoka kwa Baraza la Kipapa la wahamiaji na
watu wasiokuwa na makazi maalum katika maadhimisho ya Siku ya Wavuvi Duniani, inayofanyika
kila mwaka ifikapo tarehe 21 Novemba. Sekta ya utume wa bahari, inakumbusha kwamba,
sekta ya uvuvi inatoa ajira kwa watu zaidi ya millioni 58.3, kati yao asilimia 37%
wana ajira ya kudumu, changamoto kwa Makanisa mahalia kuhakikisha kwamba, yanawashughulikia
wavuvi katika mikakati yao ya shughuli za kichungaji, bila kuwatenga.
Sekta
ya uvuvi ni kati ya kazi zenye hatari kubwa duniani, kwani kuna maelfu ya watu wanakufa
maji baharini kila mwaka na wengine kupata vilema vya kudumu wakiwa kazini. Wavuvi
ni watu ambao wananyonywa na kudhulumiwa kwa urahisi sana na wakati mwingine wamekuwa
ni wahanga wa biashara haramu ya binadamu na kazi za sulubu, kama ambavyo inajionesha
kwenye taarifa za vyiombo vya habari.
Ikiwa kama nchi mbali mbali duniani zitaweza
kuridhia mkataba wa Shirika la Kazi Duniani, ILO wa Mwaka 2007, matatizo haya yanaweza
kupewa ufumbuzi wa kudumu na wavuvi wakaanza kutekeleza wajibu wao katika mazingira
bora zaidi. Itifaki inapania pamoja na mambo mengine ni kuhakikisha kwamba, wavuvi
wanakuwa na maisha bora zaidi wanapokuwa kazini, wawe na makazi, huduma bora za afya,
chakula bora na usalama kazini. Utume wa Bahari kwenye Makanisa mahalia unapaswa kusaidia
kuhamasisha Serikali katika nchi husika kuridhia Itifaki hii.
Shirika la Kilimo
na Chakula la Umoja wa Mataifa linabainisha kwamba, kuna uvuvi wa kupindukia, kiasi
cha kuhatarisha kutoweka kwa baadhi ya samaki. Uvuvi haramu umepelekea kuharibu mazalia
ya Samaki, hali ambayo inachangiwa pia na athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja
na uchafuzi wa mazingira. Lakini ikumbukwe kwamba, sekta ya uvuvi inachangia kwa kiasi
kikubwa katika ustawi na maendeleo ya binadamu. Hapa uvuvi unapaswa kuheshimu mazingira.